Ubalozi wa Saudia unasema mwanamke huyo 'bado ana passpoti yake'

Uwanja wa ndege wa Bangkok Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rahaf Mohammed al-Qunun anasema paspoti yake ilichukuliwa katika uwanja wa ndege wa Bangkok

Mwanamke mmoja raia wa Saudi Arabia ameripotiwa kukwama katika uwanja mkuu wa ndege wa Bankok ambako amekuwa akizuiliwa kwa kukosa tiketi ya ndege ya kurudi n yumbani, wanasema maafisa wa Saudi Arabia.

Rahaf Mohammed al-Qunun, 18, hata hivyo anasema kuwa anajaribu kutoroka familia yake nchini humo na kwamba mamlaka ya Saudia imechukua paspoti yake alipowasili nchini Thailand.

Lakini katika taarifa ubalozi wa Saudia mjini Bangkok umesema kuwa amezuiliwa kwa kukosa tiketi ya ndege ya kurudi nyumbani.

Taarifa hiyo pia imesema kuwa mwanamke huyo bado ana paspoti yake.

Bi Mohammed al-Qunun alikua safarini siku mbili zilizopita akijaribu kutoroka familia yake na kuingia nchini Australia kupitia Bangkok.

Ameiambia BBC kwamba amejitoa katika dini ya Kiislam na kwamba alikuwa na hofu huenda akalazimishwa kurudi Saudi Arabia na kuawa na familia yake.

Mwandishi wa BBC mjini Bankok, Jonathan Head anasema Bi Mohammed al-Qunun alionekana kuwa na wasiwasi na mwenye msongo wa mawazo.

Anasema kuwa ana visa ya Australia lakini paspoti yake imechukuliwa na mwanadiplomasia wa Saudia katika uwanja wa ndege wa Suvarnabhumi.

Ubalozi wa Saudia mjini Bangkok umesema kuwa amezuiliwa katika uwanja wa ndege "kwasababu hakuwa na tiketi ya ndege ya kurudi nyumbani" na kwamba atarudishwa Kuwait "ambako wengi wa watu wa familia yake wanaishi".

Mamlaka ya Saudia haina idhini ya kumzuilia katika uwanja wa ndege au mahali pengine popote, ilisema taarifa iliyotolewa na ubalozi wake.

Maafisa wanajaribu kuwasiliana na baba yake, iliongeza taarifa hiyo.

Mkuu wa polisi nchini Thailand Meja Jenerali Surachate Hakparn, ameimbia BBC kuwa Bi Mohammed al-Qunun alikuwa akitoroka kuolewa.

Kwa sababu hakuwa na kibali cha kuingia nchini Thailand, polisi imemzuilia kuingia nchini humo na kwamba ilikuwa katika harakati ya kumrudisha nyumbani kwa kutumia ndege ya Kuwait Airways aliyosafiria nayo kufikia Jumatatu asubuhi.

Jenerali Surachate amesema hakuwa na ufahamu wowote kuhusiana na tukio la paspoti yake kuchukuliwa.

Ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kesi hiyo ni "matatizo ya kifamilia" na kwamba mwanamke huyo "hakuwa na stakabadhi zilizokamilika kama vile tiketi ya ndege ya kurudi nyumbani au hela".

Hata hivyo naibu mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights barani Asia, Phil Robertson ameiambia BBC kwamba: "Huenda serikali ya Thailand inatunga hadithi kuwa alijaribu kuomba visa lakini hilo halikukubaliwa...ukweli ni kwamba alikuwa na tiketi ya kusafiri kuelekea Australia, na hakuwa na haja ya kuingia Thailand."

Alidai kuwa ni wazi mamlaka ya Thailand ilishirikiana na maafisa wa Saudia na ndio maana walifanikiwa kufikia ndege iliyokuwa imembeba Bi Mohammed al-Qunun ilipotua.

Bi Mohammed al-Qunun aidha ameiambia BBC kuwa sasa yuko katika hoteli akisubiri kurudishwa nyumbani..

Alisema : "Nilielezea kisa changu na kuchapisha picha zangu katika mtandao wa kijamii na baba yangu alikasirishwa sana na hatua yangu hiyo... Siwezi kusoma na kufanya kazi katika nchi yangu, kwa hiyo Nataka kuwa huru kusoma na kufanya kazi kama ninavyotaka."

Bi Mohammed al-Qunun aliandika katika mtandao wake wa Twitter kwamba aliamua kusambaza maelezo kumhusu mtandaoni kwa sababu hakuwa na sababu ya ''kujutia hatua hiyo'' kwa sasa.

Pia alichapisha picha ya paspoti yake na kuandika "kwasababu Nataka kuthibitisha kwamba niko hai".

Tweet nyingine ilisema: "Naogopa familia yangu itaniua."

Kisa hiki kinahusiana na kingine kilichotokea mwezi Aprili mwaka 2017 ambapo mwanamke mwingine raia wa Saudi Arabia alizuiliwa katika uwanja wa ndege alipokuwa safarini kuelekea nchini Australia.

Dina Ali Lasloom, 24, alikuwa akitoka Kuwait kupitia nchini Ufilipino lakini alikamatwa na familia yake katika uwanja wa ndege wa Manila na kurudishwa Saudia.

Alitumia simu ya mtalii mmoja wa Canada kutuma ujumbe wa video kwenye mtando wa Twitter, akisema familia yake itamuua.

Hataima yake baada ya kuwasili nchini Saudi Arabia haijulikani mpaka sasa.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii