Tundu Lissu: Mnadhimu Mkuu wa upinzani Tanzania asema 2019 ni mwaka wa kurudisha demokrasia, haki za binadamu na utu wa Watanzania

Tundu Lissu Haki miliki ya picha Getty Images

Mbunge wa Singida Mashariki kupitia chama cha upinzani Chadema ameanza mwaka 2019 kwa kuandika waraka anaohamasisha Watanzania "kurudisha demokrasia, haki za binadamu na utu..."

Katika waraka huo, Lissu ambaye alishambuliwa kwa zaidi ya risasi 30 Septemba 7 2017 amechapisha waraka huo mitandaoni Jumapili Januari 6 2018 na kuendelea kuhoji Bunge na Serikali ya Tanzania kutogharamia matibabu yake na pia kukwama kwa uchunguzi na kukamatwa kwa watu waliomshambulia.

Mbali na kudai gharama za matibabu ya Bunge, Lissu amelalamika kutotembelewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai wala watumishi wa Bunge licha ya kuahidiwa.

"Hadi ninapoandika maneno haya, bado Spika Ndugai hajatimiza ahadi yake hiyo. Hakuna mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge, au afisa yeyote wa Bunge, aliyefika hospitalini kuniona na kunijulia hali," amesema.

Lissu amesema kuwa anaanza mwaka 2019 aikiendelea kutibiwa na kutunzwa kwa michango na fadhila ya Wasamaria Wema, wa Kitanzania na wasiokuwa Watanzania.

"Kwangu mimi, hili ni jambo la heshima kubwa na la kujivunia sana. Ninaamini Wasamaria Wema hawa wamejitolea kunitibu na kunitunza muda wote huu, kwa sababu wanafahamu na kuunga mkono msimamo wangu wa kisiasa wa miaka yote: kujenga nchi na jamii isiyotegemea matakwa na fadhila za mtu mmoja mwenye mamlaka; bali jamii na nchi inayoongozwa na misingi na kanuni za demokrasia, haki, ubinadamu na ukweli,"ameandika Lissu.

Awali Bunge na serikali ya Tanzania walisema hawakuweza kugharamia matibabu ya mbunge huyo kwa sababu hakufuata utaratibu rasmi wakati akisafirishwa nje ya nchi kwa matibabu.

Image caption Tundu Lissu akizungumza na mwandishi wa BBC, Zuhura Yunus

Gazeti la Mwananchi la Tanzania limemnukuu Spika Job Ndugai kuwa amemjibu Lissu akimtaka arejee Tanzania waweke mambo mezani kisha Watanzania wapime nani asiye na shukrani.

"Katika shambulio hili, hakuna anayeshukiwa na Jeshi letu la Polisi hadi sasa. Hakuna aliyehojiwa na wapelelezi mahiri wa Jeshi letu la Polisi. Hakuna aliyekamatwa na kwa hiyo, hakuna aliyeshtakiwa" alidai Lissu.

Watu wasiojulikana

Lissu ambaye hivi karibuni ameeleza nia yake ya kugombea urais mwaka 2020 kupitia Chadema amelizungumzia suala la watu wasiojulikana akidai watu hao "wameendelea kuwatesa Watanzania."

"Tulimaliza mwaka 2017 na tumemaliza mwaka jana taifa letu likiwa kwenye hofu kubwa...Hofu ya kutekwa nyara na kupotezwa kabisa, ama kuteswa na baadae kuachiliwa bila uchunguzi wala sababu zozote kutolewa na Serikali yetu," amedai Lissu.

Lissu amerejelea mikasa maarufu iliyotekelezwa na 'watu wasiojulikana kama kutekwa na kupotea kwa aliyekuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Ben Saanane aliyepotea tangu Novemba 2016. Azory Gwanda, mwandishi wa gazeti la Mwananchi, aliyechukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake mwishoni mwa mwaka 2017 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Simon Kanguye, aliyepotea baada ya kukamatwa nyumbani kwake.

"...Matukio yote haya bado hayana majibu yoyote ya maana kutoka kwa Serikali ya Rais Magufuli na vyombo vyake vya usalama," ameandika Lissu.

Maendeleo Kiafya

Huwezi kusikiliza tena
Tundu Lissu akosa msaada kutoka serikali ya Tanzania

Lissu alipelekwa nchini Ubeligiji Januari 6, 2018 kupata matibabu zaidi baada ya kutibiwa nchini Kenya kwa takribani miezi minne ambapo alikimbizwa kutoka Dodoma siku hiyohiyo aliyoshambuliwa.

"Tuliuanza mwaka jana 2018 nikiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya. Kwa wakati huo, tayari nilikuwa nimeshafanyiwa operesheni 17 katika sehemu mbali mbali za mwili wangu. Tumeuanza Mwaka Mpya 2019 nikiwa hospitalini tena, mara hii katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Campus ya Gasthuisberg, mjini Leuven, nchini Ubelgiji. Hii ni kwa sababu, siku ya mwisho ya mwaka jana, yaani tarehe 31 Disemba, 2018, nimefanyiwa operesheni ya 22 mwilini mwangu, kutokana na majeraha ya risasi nilizopigwa siku hiyo ya Septemba 7."

Katika waraka wake huo, Lissu amesema tofauti na mwanzoni mwa mwaka jana, amerudi hospitali mara hii ili kumalizia safari ya tiba.

"Tayari nimeshaongezewa kasi ya mazoezi ya kutembea, na muda si mrefu nitaanza mazoezi ya kutembea kwa miguu yangu mwenyewe bila kutumia magongo," amesema na kumalizia "Ni sahihi, kwa hiyo, kusema kwamba, pamoja na ukweli kwamba matibabu yangu bado yanaendelea, nimeanza Mwaka Mpya nikiwa na Mguu Mpya!!!"

Mada zinazohusiana