Mikakati ya kupanga mkutano mwingine kati ya rais Kim Jong un na rais Donald Trump inaendelea.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un na mke wake Ri Sol-ju wanajiandaa kuelekea China Kutoka Pyongyang, Januari 7 mwaka 2019 Haki miliki ya picha EPA
Image caption Bwana Kim anazuru China akiandamana na mke wake Ri Sol-ju,kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, ameanza ziara nchini China kwa mazungumzo na Rais wa nchi hiyo Xi Jinping.

Ripoti zinasema Bwana Kim ambaye ameandamana na mke wake Ri Sol-ju atakuwa China hadi Januari 10.

Ziara hiyo inakuja wakati ambapo mikakati ya kupanga mkutano wa pili kati ya rais Kim Jong un na rais wa Marekani Donald Trump zikiendelea.

Wawili hao walikutana mwezi Juni mwaka uliyopita hatua ambayo ilikuwa ni ya kwanza kwa rais wa Marekani aliye madarakani.

Siku ya Jumatano kulikuwa na madai kuwa bwana Kim huenda akatumia trani yake maalum kusafiri hadi China.

Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini ambaye pia anaandamana na maafisa wake kadhaa, anazuru Uchina kwa mara ya nne katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja.

Jumanne inaripotiwa kuwa siku ya kuzaliwa kwa kiongozi huyo ambaye anasherehekea miaka 35 ya siku yake ya kuzaliwa japo tarehe ya siku hiyo haijathibitishwa na Pyongyang.

China ni mshirika muhimu wa kidoplomasia wa Korea Kaskazini na moja ya vyanzo vikuu vya biashara na misaada.

"[Bwana] Kim anapania kuukumbusha utawala wa Tramp kwamba taifa lake lina njia mbadala ya kujikimu kiuchumi tofauti na ile inayotolewa na Washington na Seoul," Harry J Kazianis, mkurugenzi wa taasisi ya masomo ya ulinzi aliiambia shirika la habari la Reuters.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ziara ya kwanza ya Kim nchini China ilifanyika mwezi machi mwaka jana

Bwana Kim hakuwahi kukutana na Xi katika miaka sita ya kwanza ya uongozi wake nchini Korea Kaskazini.

Lakini mwaka jana alizuru China mara tatu na hakuna hata ziara moja kati ya hizo zilitangazwa kabla zifanyike.

Mwandishi wa BBC Laura Bicker aliyepo mjini Seoulanasema mbili kati ya ziara hizo zilifanyika kabla ya mkutano wa kihistoria kati ya viongozi wa Korea Kaskazini na Marekani.

Kiongozi wa Korea Kusini Moon Jae-in na rais Trump, walionekana wakipanga mikakati kuelekea mkutano huo.

Mkutano huu wa sasa huenda ukazua uvumi kwamba mkutano mwingine kati ya Marekai na Korea Kaskazini utafanyika hivi karibuni.

Mapema wiki hii ,Bwana Trump alisema mkutano mwingine utatangazwa hivi karibuni, lakini vikwazo dhidi ya Pyongyang vitaendelea kutekelezwa.

Katika hotuba yake ya mwaka mpya wiki iliyopita, bwana Kim alisema kuwa amejitolea kukabiliana na zana za nuklia, lakini akaonya kuwa huenda akabadisha msimamo ikiwa Marakani itaendelea kuiwekea nchi yake vikwazo.

Hatua za kidiplomasia kati ya rais Trump na mwenzake Kim zimekwama tangu viongozi hao walipokutana nchini Singapore.

Pande zote mbili wakati huo ziliafikiana kumaliza salaha za nuklia katika rasi ya Korea japo haikubainika yale yaliyokuwemo kwenya mkataba waliyotia saini.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii