Juma Nkamia: Mswada wa kuongeza muhula wa urais na wabunge na maana yake Tanzania

Rais Magufuli hajafurahishwa na wazo hilo la Bw Nkamia Haki miliki ya picha IKULU, Tanzania
Image caption Rais Magufuli hajafurahishwa na wazo hilo la Bw Nkamia

Jina la Mbunge wa jimbo la Chemba mkoani Dodoma kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho kinachotawala sasa, Juma Nkamia limerudi kwa mara ya pili katika duru za kisiasa huku akisimamia ajenda ya kuongezwa muda wa muhula wa ubunge na urais nchini Tanzania kutoka miaka mitano hadi saba.

Nkamia aliwasilisha kwa mara ya kwanza hoja binafsi kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Bunge mnamo Septemba 2017 mbele ya Spika Job Ndugai.

Hoja yake ilikuwa ni ukomo wa ubunge ambao ndani yake kulihusisha ukomo wa muhula wa urais nchini Tanzania kutoka miaka mitano hadi saba.

Mbunge huyo aliwasilisha notisi yake kwa Bunge, kabla ya baadaye kuiondoa hoja hiyo kwa madai ya kushauriwa na baadhi ya wabunge wenzake na chama chake cha CCM.

Nkamia alirejea hoja ya ukomo wa urais na ubunge kwa mara ya pili Desemba mwaka 2018 akisisitiza kuwa miongoni mwa mipango yake katika siasa kwa mwaka 2019 ni kuwasilisha upya hoja yake ya ukomo wa ubunge na urais.

Duru za kisiasa zimesema kuwa Nkamia amejipanga kukabiliana na wakosoaji huru ndani ya chama na nje ya chama chake pamoja na baadhi ya wabunge wenzake ambao hawakubaliani na mpango huo.

Gharama ya uchaguzi na wabunge kuhama vyama

Duru za kisiasa zinaonyesha kuwa msingi wa hoja binafsi ya Juma Nkamia ambayo hajataja muda wa kuwasilisha tena bungeni mbele ya Spika, Job Ndugai, msingi wake wa kutaka kusogezwa kwa muda wa kufanya uchaguzi kutoka miaka 5 ya sasa hadi miaka 7 unatokana na gharama za uchaguzi.

Nkamia anasema kuwa Tanzania imekuwa ikiingia kwenye gharama nyingi za kufanya uchaguzi wa mara kwa mara yaani kila baada ya miaka mitano, hivyo anasisitiza ni vyema kuongezwa muda wa kukaa madarakani.

Lakini katika hoja hiyo hajagusia suala la wabunge waliohama na wala sheria inayoruhusu kufanyika uchaguzi mdogo iwapo mbunge au diwani wa eneo husika amefariki dunia au kujiuzulu wadhifa wake na kuhamia chama kingine au kuachana kabisa na siasa kama ilivyowahi kutokea kwa Mbunge wa zamani wa Igunga mkoani Tabora, Rostam Aziz.

Nkamia anaona muda wa ubunge wa miaka mitano hautoshi, kwa hivyo ingefaa kufanyiwa mabadiliko ya kisheria na Bunge lilitamke kuwa muda wa ubunge utakuwa miaka 7 sambamba na urais.

Msimamo wa Magufuli

Mara baada ya kuibuka hoja ya Mbunge Nkamia, wengi walisubiri kauli ya rais Magufuli kuhusiana na mpango huo ili kusafisha hali ya hewa kisiasa ambayo ilitafsiriwa kuchafuliwa kutokana na nia ya kutaka kubadili Katiba.

Haki miliki ya picha IKULU, Tanzania
Image caption Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM jijini Dar Es salaam kikiendelea Desemba mwaka 2018

Rais Magufili ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM mnamo Januari 13, mwaka 2018 aliweka wazi kutofurahishwa na hakupenda mjadala uliokuwa ukiendelea kuhusu mabadiliko ya Katiba na kuongeza muda wa ukomo wa uongozi kutoka miaka mitano ya sasa na kwenda miaka saba.

Kwa mujibu wa taarifa ya iliyotolewa siku hiyo na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, alisema kuwa Rais Magufuli haoni umuhimu wowote katika mjadala huo na kwamba ameelekeza nguvu,akili na malengo yake ni kujenga uchumi wa Tanzania.

Magufuli amelazimika mara mbili kutoa kauli ya kufuta uvumi uliojaa katika duru za kisiasa juu ya kufanya mabadiliko ya Katiba ya kuongeza muhula wa urais.

Ilikuwa Novemba mwaka 2017 ambapo kwa mara ya kwanza Rais Magufuli alilazimika kutoa kauli kutokana na mjadala huo, kwamba hana mpango wowote wa kuongeza muda wa muhula wa urais. Alisisitiza kuwa alikula kiapo cha kuheshimu na kuilinda Katiba.

Wosia wa Nyerere

Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuonya juu ya hatua za kuongeza muhula wa urais. Kupitia kitabu chake cha "Uongozi Wetu na Hatima ya Nchi yetu," Mwalimu Nyerere anasema, "Rais alieleza kuwa walikuwa wamekubaliana kwamba vipindi vya kuwa Rais ni lazima vitamkwe, lakini walikuwa hawajaafikiana uamuzi viwe vipindi vingapi. Awali baadhi ya viongozi wa Chama walikuwa wameanza kampeni za kutaka Rais Mwinyi aongezewe vipindi vya muda wa kuwa Rais."

"Nilipotambua hivyo nilikuwa nimekwenda mara moja kwa Rais na kumsihi azizime kampeni hizo; na viongozi wahusika nilitafuta nafasi nao nikawaomba wasilifufue jambo hili. Nikadhani tumeelewana hivyo. Kwa hiyo nilistuka niliposikia kuwa kumbe suala hilo la vipindi vya urais bado linazungumzwa, na ati bado uamuzi wa vipindi vingapi haujafikiwa."(Uk.9).

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Sanamu ya Mwalimu Nyerere katika mgahawa mmoja wa ufuoni Entebbe, Uganda

Mwalimu anaendelea kuonya tena, "Suala hili lilikwishakuamuliwa zamani, na sasa ni sehemu ya Katiba yetu. Uamuzi huo inafaa uheshimiwe. Rais Mwinyi ndiye Rais wa kwanza kuchaguliwa kwa mujibu wa katiba hiyo. Yeye akisema kuwa vipindi viwili havitoshi, na akataka viwe vitatu; Rais wa pili atasema vipindi vitatu havitoshi, na atataka viwe vinne na kadhalika mpaka tufikie Ngwazi (rais wa milele) wa Tanzania," (uk.10).

Wingi wa wabunge

Kama hoja binafsi ya Juma Nkamia ikipokelewa na kujadiliwa na Bunge hili kisha kupigiwa kura, ina maana CCM kitakuwa na nafasi kubwa ya kushinda na kupitishwa hoja hiyo kutokana na idadi ya wabunge wake.

CCM wana jumla ya wabunge 231 kutoka majimbo ya uchaguzi na wale wa viti maalumu. Aidha, CCM kina wabunge wengine 9 wanaoteuliwa na rais, hii ina maana chama hicho kina jumla ya wabunge 240 ambao wanaweza kutimiza akidi ya matakwa ya kisheria. Hili ni jambo la hatari na si la kushangiliwa.

Miaka mitano haiwatoshi wabunge?

Katika upande mwingine wa hoja ya Juma Nkamia inatuletea swali, kwamba je, ni kweli miaka mitano ya ubunge na urais haitoshi kuwatumikia wananchi?

Kwamba kama muda wa rais kubaki madarakani ukiongezwa, utachochea maendeleo nchini au utadhoofisha? Je, iwapo muda wa Mbunge kuwa madarakani utaongezwa ni jawabu la ufanisi na utekelezwaji wa ahadi zao kwa wananchi?

Kwamba kwakuwa Mbunge anakuwa na miaka mitano, ina maana haitoshi kukamilisha ahadi zake kiasi cha kuhitaji nyongeza ya miaka miwili tena, ikiwa na maana mihula miwili itakuwa miaka 14 na baadaye tutakuwa na wabunge 'haambiliki'?

Kwa mfano, Nkamia anaitumia utaratibu wa nchi ya Rwanda kama mfano wake. Lakini Rwanda walikuwa na sababu za msingi kutokana na historia ya nchi yao hivyo ikakubaliwa uongozi uwe wa miaka 7.

Haki miliki ya picha IKULU, Tanzania

Katiba sasa imebadilishwa, kuanzia mwaka 2024 Rwanda itakuwa na ukomo wa urais wa miaka mitano na sio 7 tena. Hii ina maana Rwanda wanatamani kuwa kama Tanzania halafu Tanzania yenyewe inao viongozi aina ya Juma Nkamia wanaotaka kuwa kama Rwanda wakati hatulingani historia zetu za kisiasa.

Dalili ya mvua

Wahenga walipata kusema dalili ya mvua ni mawingu. Zogo hilo la ukomo wa urais limewahi kuibuliwa wakati wa awamu ya pili ya uongozi wa Ali Hassan Mwinyi, na sasa Juma Nkamia anapita njia ileile ambayo ni dalili tosha za kuamia kama jambo hilo halitafanyika sasa, basi lipo njiani na wananchi wa Tanzania kuna siku watashuhudia mabadiliko ya katiba kuongeza muhula wa rais.

Duru za kisiasa zinaonyesha kuwa miongoni mwa waanzilishi wa ajenda ya kufanya mabadiliko ya katiba tangu awamu hii ianze ni kampeni ya "Magufuli baki" iliyoanzishwa na Lawrence Mabawa, ambaye alipanga kuzunguka nchi nzima kueneza ajenda hiyo. Mwanasiasa huyo amewahi kuomba kuteuliwa kugombea ubunge ndani ya CCM mwaka 2015.

Aidha, suala hili linaweza kuleta mjadala mwingine kuwa muhula wa urais na ubunge unapoongezwa una uhusiano gani na mafanikio ya maendeleo ndani ya nchi?

Hii haina tofauti na kuandaa visingizio kila tunaposhindwa kutekeleza wajibu wetu kwa wananchi.

Kuleta maendeleo kwa nchi sio suala la miaka 5 au 7 bali dhamira, sera, sheria, kanuni, taratibu, vita dhidi ya ulaji rushwa, ufisadi, upendeleo pamoja na kulinda maslahi ya nchi. Mwalimu Nyerere alikaa madarakani miaka 24, je muhula wa miaka 7 ndio chanzo cha taifa kuwa na maendeleo hafifu?

Muda utaongea.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii