Sudan: Je mapinduzi ya kijeshi yanaongezeka Afrika?

Soldiers in Sudan

Chanzo cha picha, Getty Images

Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, amepinduliwa na jeshi kufuatia maandamano makubwa ya kupinga utawala wake.

Jeshi linasema sasa litasimamia utawala wa miaka miwili wa mpito utakaofuatiwa kwa uchaguzi mkuu.

Rais al-Bashir mwenyewe alidhibiti uongozi kupitia mapinduzi ya kijeshi mnamo 1989 na kabla ya hapo kumeshuhudiwa majaribio kadhaa ya mapinduzi nchini Sudan, baadhi yakifanikiwa huku mengine yakifeli.

BBC inatathmini ukweli wa mambo kwa kutazama nyuma katika historia ya mapinduzi ya kijeshi ya Sudan, na taswira nzima katika bara la Afrika.

Sudan imewahi kushuhudia majaribio ya mapinduzi zaidi ya taifa jingine barani Afrika.

Ikiwemo wa hivi karibuni, kwa jumla ni majaribio 15 - kati yao 5 yamefaulu kwa kujumuishwa sasa kutimuliwa kwa Omar al Bashir.

Lakini je, bara la Afrika linaondokana na umaarufu wake wa mapinduzi ya serikali kwa mtutu wa bunduki?

Ni wakati gani mapinduzi ya serikali yanakuwa mapinduzi?

Tangu mwaka 1950, kumekuwepo na jumla ya matukio 204 ya kuipindua serikali za nchi mbali mbali katika bara la Afrika. Baadhi yalifanikiwa na mengine yaliishia kuwa majaribio tu, hii ni kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na wanasayansi wa siasa raia wa Marekani, Jonathan Powell na Clayton Thyne, ambao walikuwa katika chuo kikuu cha Florida na chuo kikuu cha Kentucky.

Tafsiri yao ya mapinduzi ni majaribio yasiyo halali yanayofanywa na jeshi ili kuing'oa madarakani serikali au kiongozi wa serikali kumtoa madarakani kiongozi mkuu wa serikali aliyekuwepo.

Hata hivyo tafsiri ya mapinduzi imekuwa ikitazamwa kwa namna mbalimbali, na huko nyuma viongozi wa jeshi walikataa kuwa hawafanyi mapinduzi ya kijeshi.

Kwa mfano ukiangazia Zimbabwe mwaka 2017. Jeshi lilliibua vuguvugu la kumaliza utawala wa miaka 37 wa Robert Mugabe. Kwa kipindi hicho afisa mkuu wa jeshi Meja Jenerali Sibusiso Moyo, alienda kwenye televisheni ya Taifa na kukataa kufanyika kwa mapinduzi ya kijeshi.

"Viongozi wa mapinduzi hayo ya kijeshi walikua wakikataa kufanya tukio hilo ili ionekane kuwa ni halali," anasema Powell.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Furaha baada ya jeshi la Zimbabwe kuingilia kati utawala wa Mugabe 2017.

Katika bara la Afrika kumekuwapo na mapinduzi ya kijeshi 104 yaliyofanikiwa na 100 ambayo hayajafanikiwa.

Sudani imekuwa na matukio mengi zaidi ya mapinduzi, 14. Burkina Faso ndiyo ambayo inashika nafasi ya kwanza kwa mapinduzi kufanikiwa, ambapo mara saba jeshi liling'oa serikali iliyopo madarakani.

Je Afrika inaanza kuwa na mapinduzi machache ya kijeshi?

Afrika kwa hakika imekuwa na idadi kubwa ya mapinduzi ya kijeshi, lakini njia hii ya kulazimisha mabadiliko inapotea.

Maelezo ya picha,

Idadi ya majaribio ya mapinduzi ya kijeshi barani Afrika

Kati ya 1960-1999, kulikuwa na mapinduzi ya kijeshi kati ya 39 na 42 kila mwongo mmoja. Tangu kipindi hicho mapinduzi hayo yamepungua sana. Miaka ya 2000 kulikuwa na mapinduzi ya kijeshi 22, na muongo huu ni mapinduzi 16 tu.

Powel anasema sio jambo la kushangaza kutokana na hali ambayo nchi za Afrika zilikumbana nazo baada ya Uhuru.

"Nchi za Afrika zimekuwa na hali ambazo hupelekea mapinduzi kama vile umasikini na hali mbaya ya kiuchumi," anasema Powell.

Taswira ya ulimwengu.

Ulimwenguni jumla ya mapinduzi ya kijeshi ni 475.

Hivyo Afrika imekumbana na idadi kubwa ya mapinduzi ya kijeshi ukilinganisha na sehemu nyengine.

Inayofuata ni Amerika ya Kusini ambapo imekuwa na majaribio ya kuipindua serikali 95 na mapinduzi ya kijeshi yaliyofanikiwa ni 40.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Maandamano Venezuela kupinga jaribio la kumng'oa Rais Chaves madarakani.

Hata hivyo kwa miongo miwili iliyopita majaribio ya jeshi kuipindua serikali yamepunguua sana Amerika ya Kusini. Mapinduzi ya mwisho yalikuwa Venezuela mwaka 2002 ambapo walitaka kumtoa madarakani Hugo Chaves, lakini jaribio hilo lilishindwa.

Powell amebainisha kuwa kumalizika kwa Vita Baridi ambayo ililazimisha Marekani na Umoja wa Usovieti kuingilia mambo ya ndani ya nchi za Amerika ya Kusini na utayari wa Jumuiya ya Kimataifa kuziwekea vikwazo nchi zinazofanya mapinduzi, kama ilivyofanyika kwa Haiti mwaka 1994, kumepelekea kupungua kwa mapinduzi ya kijeshi.

Bara la Asia pia limeshuhudia kupungua kwa majaribio ya mapinduzi ya kijeshi.