John Magufuli: Rais wa Tanzania asema mawaziri hawana likizo, hata yeye hajaenda likizo

Rais Magufuli Haki miliki ya picha IKULU, TANZANIA

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amesema Mawaziri na Makatibu Wakuu wa wizara hawatachukua likizo kwa sababu watanzania wanaowatumikia hawajachukua likizo.

Kauli hiyo ya rais ni majibu kwa Spika wa Bunge Job Ndugai ambae awali ameonekana kuwaombea likizo viongozi hao, katika hafla ya uapisho wa viongozi wapya Ikulu jijini Dar es Salaam mapema leo Jumatano.

"Nilikuwa naangaliana na waheshimiwa mawaziri naona wamechoka. Nikajiuliza hivi mawaziri hawana likizo? Nawaombea likizo mheshimiwa Rais, mmoja mmoja angalau mwezi kidogo. Lakini umewapa wasaidizi wa kuwasaidia na mimi kwasababu nafanya nao kazi kwa ukaribu kule bungeni kwakweli nashuhudia wanachapa kazi ambayo haijawahi kuonekana kabisa," spika wa bunge Job Ndugai alisema.

Hata hivyo, rais Magufuli amewataka mawaziri na Makatibu wa Wakuu kukaza buti na kuwatumikia watanzania, wakati huo huo, akikiri kwamba hata yeye yuko hoi kwa sababu hajachukua likizo.

"Kwa makatibu wakuu na wizara najua mna majukumu makubwa na ndio maana muheshimiwa spika anazungumza hapa hamjachukua likizo, hata mimi sijachukua likizo hapa nilipo nipo hoi kweli lakini utaichukua likizo wakati wananchi unao waongoza hawana likizo kwasababu ukiangalia, wakulima wafanyakazi wavuvi wafugaji katika sekta mbalimbali watanzania hawa wote milioni 55 hawana likizo katika shughuli zao kwahiyo saanyingine inatuwia vigumu sisi kuchukua likizo wakati wale walio tuchagua hawana likizo wao wanataka maendeleo wanataka yale ambayo tuliahidi tunatekeleza," amesema.

Katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri Rais Magufuli amempandisha cheo aliyekuwa Naibu Waziri wa Madini Doto Mashaka Biteko kuwa waziri mpya wa madini. Aliyekuwa Waziri wa Madini Anjellah Kairuki ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji ambao ni wadhifa mpya.

Wizara ya Nishati na Madini, ambayo awali ilikuwa na manaibu waziri wawili, hivi sasa imesalia na naibu mmoja.

Haki miliki ya picha IKULU TANZANIA
Image caption Rais Magufuli akimuapisha Dotto Biteko kuwa waziri wa Madini

Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa na utendaji wa Wizara ya Madini hususani katika udhibiti wa utoroshaji wa madini na hivyo amemtaka Biteko na taasisi zilizo chini ya wizara yake kushirikiana na Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania kuanzisha vituo vya ununuzi wa madini ili kudhibiti utoroshaji na kuiwezesha Benki Kuu kuwa na hifadhi ya dhahabu.

"Tumewaruhusu wawekezaji na wachimbaji wadogo wachimbe dhahabu, Je Wizara ya Madini mmeshajiuliza dhahabu inayochimbwa inauzwa wapi? Na je kama wanachimba na wanauza sisi tunapata asilimia ngapi? Hili suala ni la Wizara ya Madini, halikuwa suala la Bunge kujiuliza, wala halikuwa suala la Waziri Mkuu au Rais kujiuliza.

"Kwenye sheria ya madini nina hakika kuna mahali imeelekeza kuanzishwa kwa vituo vya kuuzia madini, je vimeanzishwa vituo vingapi? viko wapi? Kwa sababu vingeanzishwa vituo hivi tungejua dhahabu inayosafirishwa, wapi imeuzwa na inawezekana tungekuwa na taarifa za kila wiki, lakini hakuna" amesemaRais Magufuli.

Mada zinazohusiana