Trump alitaja mkutano kati yake na viongozi wa Democratic kama hatua ya "kupoteza muda"

Rais wa Marekani Donald Trump Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais wa Marekani Donald Trump

Rais wa Marekani Donald Trump ameondoka katika mkutano wa viongozi wa chama Democratic baada ya mazungumzo kati yao kutibuka.

Hatua hiyo inajiri huku huduma za serikali zikiendelea kulemazwa wa siku ya 19 mfululizo.

Trump alivunja mazungumzo hayo baada ya spika wa bunge Nancy Pelosi na kiongozi wa wengi bungeni Chuck Schumer kushikilia kuwa hawana nia ya kufadhili mpango wake wa kujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico.

Trump alitaja mkutano kati yake na viongozi hao kama hatua ya "kupoteza muda".

Wafanyikazi 800,000 wa serikali huenda hawatalipwa mishahara yao kwa mara ya kwanza tangu huduma muhimu za serikali zilipoanza kusitishwa.

Baada ya mkutano huo rais aliandika maneno "bye-bye" katika mtandao wake wa Twitter akiashiria kuwaaga viongozi wa Democrats.

Nje ya Ikulu ya Marekani pande zote mbili zimekuwa zikizona baada ya mkutana kati ya rais Trump na viongozi wa Democratic kuvunjika.

Bi Pelosi, ambaye ni spika wa bunge la Marekani amesema kuwa wafanyikazi wa umma wanatatizika kwa sababu hawatapokea mishahara yao kutokana uamuzi huo wa rais Trump.

"Rais anaonekana kutojali," alisema. "Anafikiria pengine watawaomba baba zao pesa zaidi. Lakini hilo haliwezekani."

Bwana Schumer ameambia wanahabari kuwa rais aliondoka ghafla katika mkutano baada ya spika Pelosi kusema kuwa hataidhinisha sheria yoyote.

Kiongozi huyo wa Democratic katika bunge la seneti alisema kuwa: " rais [Trump] alimuuliza Pelosi, 'Je utakubali kuidhinisha ufadhili wa ukuta wangu?' Akasema hapana.

"Ni hapo alisimama na kusema, 'Basi hatuna la kujadiliana,' na kuenda zake.

"Kwa mara nyingine tulijionea hasira za kitoto kwa sababu hakupata alichotaka."

Seneta huyo wa New York pia alisema kuwa bwanaTrump"aliwagongea meza", lakini makamu wa rais Mike Pence aliingilia kati kutuliza hali.

"Rais alitoka kimya kimya katika chumba cha mkutano," alisema kiongozi wa wengi bungeni kutoka chama cha Republican Kevin McCarthy.

"Sikumuona rais akipaza sauti wala kurusha mkono." alisema kiongozi huyo huku akitaja tabia ya Democrats kuwa ni ya"kuibisha".

Japo viongozi wa Republican na rais Trum awanasisitiza kuwa chama hicho"kimeungana kabisa" nyuma ya pazia, baadhi ya maseneta wenye msimamo wa kadri hawajaridhishwa na suala hilo.

Bwana Trump ameomba ufadhili wa dola bilioni 5.7 kujenga ukuta wa chuma katika mpaka kati ya Marekani na Mexico ili kutimiza ahadi aliyotoa wakati wa kampeini yake ya urais.

Lakini Democrats - ambao mwezi uliyopita walichukua udhibiti wa bunge wamekataa kuidhinisha fedha hizo.

Purukushani la siku ya Jumatano linajiri siku moja baada ya hotuba ya kwanza ya rais kwa taifa ambapo alisema suala la mpaka wa Marekani na Mexico ni tisho kwa usalama wa taifa

Bi Pelosi na bwana Schumer walighadhabishwa na tamko hilo la rais wakisema kuwa ni tishio feki.

Trump ametisha kutangaza suala hilo kama janga la kitaifa"mzozo", katika juhudi za kukwepa mchakato wa bunge ili kujenga ukuta huo.

Mashirika 9 ya serikali yanakabiliwa na hatari ya kufungwa kwa kukosa fedha za kuendesha huduma tangu Desemba 22.

Kura mpya ya maoni inaashiria kuwa nusu ya Wamarekani (51%) wanamlaumu rais Trump kwa kulemaza huduma za serikali lakini 77% ya wapiga kura Republican wanataka fedha za kujenga ukuta.

Katika mitandao ya kijamii, wafanyikazi wa serikali wamekuwa wakielezea hali ngumu inayowakabili kutokana na mzozo huo.

Baadhi ya wanatafakari kutafuta kazi mpya ili kujikimu kimaisha.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wahamiaji wa Honduras wakitembea kuelekea Marekani kupitia mpaka wa Mexico

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii