Mawimbi kutoka anga za juu: Nadharia tano kuhusu chanzo chake

A nebula of stars Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption A nebula of stars

Mawimbi ya redio kutoka mifumo ya nyota na sayari iliyo mbali sana na dunia imenaswa na darubini Canada.

Mawimbi hayo ya redio yaendayo kwa kasi sana (yanayofahamika pia kama FRBs kwa maana ya Fast Radio Bursts) yanapofika kwenye darubini zilizo duniani huangaza kwa milisekunde chache, na kisha kutoweka.

Wataalamu wa anga za juu wamekuwa wakipokea na kutambua mawimbi kama hayo mara kadha katika kipindi cha miaka kumi iliyopita - na wiki hii wametangaza kugundua mawimbi zaidi.

Miongoni mwa mawimbi yaliyonaswa ni mawimbi adimu, ambayo hujirudia badala ya kuangaza mara moja pekee.

Bado haijabainika mawimbi haya hasa yanatoka wapi. Kuna nadharia tano kuu kuyahusu, ambazo tunaziangazia hapa

1. Nyota inayozunguka kwa kazi

Nyota zinapolipuka na kuangamia, masalio yake yanaweza kuwa nyota za nutroni ambazo zinazunguka kwa kasi sana.

Nyota ya nutroni huwa ni nyota ambayo ina nguvu nyingi sana za sumaku na ambayo inazunguka yenyewe kwa kasi sana. Nyota za nutroni ni kitu kwenye anga za juu ambacho si kikubwa sana (nusu kipenyo chake ni kilomita 30 hivi) na kina uzani wa juu sana, na kimeundwa na nutroni (neutron) ambazo zimebanana sana).

Wataalamu wa anga za juu wanaamini kwamba nyota hizo zinazopatikana eneo lenye nguvu nyingi za sumaku zinaweza kutoa mawimbi kama hayo ya redio.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mchoro wa nyota ya nutroni

"Kitu kama nyota ya nutroni kinalingana vyema kabisa na tukio hili kwa kweli," anasema Dkt Ingrid Stairs, ambaye ni mtaalamu wa fizikia ya anga za juu katika Chuo Kikuu cha British Columbia (UBC) mjini Vancouver, Canada.

"Lakini fizikia inayotumika ndipo kuzalishwe mawimbi haya ya kasi yenye nguvu sana ya redio ni jambo ambalo kufikia sasa hatujalifahamu."

Unaweza kusoma pia:

2. Kuungana kwa nyota mbili

Tukio la kugongana kwa nyota mbili za nutroni kunaweza pia kusababisha mawimbi kama hayo.

Kwa mujibu wa Shriharsh Tendulkar ambaye ni mtaalamu wa anga za juu wa Chuo Kikuu cha McGill jijini Montreal, Canada hii ni moja ya nadharia kuu zinazotumiwa kueleza tukio hili.

Lakini hili linaeleza maana tu wakati ni mawimbi yanayotolewa mara moja tu, kwani nyota zote mbili huangamia baada ya kugongana.

"Ni tukio la maangamizi - haliwezi kueleza mawimbi ya redio ya kasi yanayojirudia," anasema.

Mengi ya mawimbi ya redio ya kasi ambayo yamenaswa na darubini katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita ni mawimbi ambayo hutokea mara moja tu na kutoweka.

Lakini kina mawimbi mara mbili ambayo yamenaswa ambayo ni tofauti - ni mawimbi ambayo yanaangaza na kujirudia mara kadha. Kwa mawimbi hayo, nadharia hii ya kuungana kwa nyota haiwezi kutumika kuyaeleza.

3. Blitzar

Blitzar ni nyota ya nutroni ambayo inazunguka yenyewe kwa kasi sana, na kwa sababu ina uzani mkubwa sana, inaporomoka yenyewe na kuacha kitu kama shimo ombwe, ambalo kwa Kiingereza huitwa 'black hole'. Tukio hilo la kuporomoka kwa nyota hiyo linaweza kuzalisha mawimbi hayo.

Pia, tukio hili mwisho wake huwa ni kuangamia kwa nyota hiyo, na kwa hivyo hilo haliwezi kutumiwa kueleza mawimbi hayo yanayojirudia.

4. 'Black hole'

Mashimbo ombwe ya anga za juu, au Black hole yametumiwa sana katika nadharia nyingi - kuanzia kwa nyota ya nutroni kutumbukia kwenye shimo ombwe la anga za juu hadi kwa shimbo lenyewe kuporomoka au kitu kisichofuata fizikia ya kawaida (dark matter) kugonga shimo kama hilo au kutumbukia eneo kama hilo.

Haki miliki ya picha NASA/JPL-Caltech
Image caption Wazo la black hole

5. Viunge wa anga za juu

Ingawa baadhi wanaamini mawimbi haya ni ya kawaida tu na yanatokana na maumbile, kuna wengine wanaoamini huenda ni ishara za shughuli ama juhudi za viumbe wengine wanaoishi maeneo mengine anga za juu.

Au pengine mawimbi yenyewe yawe ni chombo hicho cha anga za juu?

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Darubini za redio zina uwezo wa kunasa mawimbi ya redio yaendayo kwa kasi sana

Dkt Stairs anasema uwezekano wa hili kutokea ni nadra sana.

"Mawimbi haya hutokea kote anga za juu na kutoka maeneo ya umbali tofauti - ni lazima yawe yanahusishwa na mifumo tofauti ya nyota na sayari," aliambia BBC.

"Kwa kweli, haiwezekani kwamba kunaweza kuwa na falme au himaya au jamii za viumbe wa anga za juu ambao wote wanaamua kutumia njia moja ya mawasiliano (kutuma mawimbi ya redio) - ni jambo ambalo kwa kweli uwezekano wake ni finyu mno."

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii