Acacia Mining: Kampuni ya uchimbaji madini yalimwa faini ya milioni 300 kwa uchafuzi wa mazingira Tanzania

Haki miliki ya picha ACACIA

Kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia Mining imetozwa faini ya Sh300 ($130,000) kwa tuhuma za uchafuzi wa mazingira katika mgodi wake wa North Mara.

Acacia na serikali ya Tanzania wamekuwa kwenye mahusiano magumu toka mwaka 2017. Serikali imekuwa ikiituhumu kampuni hiyo kwa kukwepa kodi, udanganyifu na kusafirisha mchanga wenye madini nje ya nchi kinyume na sheria.

Acacia imekanusha madai hayo wakidai kila wakifanyacho ni kwa mujibu wa sheria za Tanzania na mikataba ya ndani na ya kimataifa waliyoafikiana.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na kampuni hiyo Alhamisi, Januari 10, kampuni hiyo inadai kuwa bado haijapokea kielelezo chochote juu ya uchafuzi huo wa mazingira.

"Mgodi haujapokea kielelezo chochote au takwimu za vipimo vya uchafuzi kulingana Katazo la Uchafuzi wa Mazingira. Kwa sasa mgodi unafanya tathmini ya kitaalamu juu ya uchafuzi unaodaiwa kufanyika," imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Haki miliki ya picha IKULU TANZANIA
Image caption Mgogoro kati ya Acaccia na Tanzania uliibuka Machi 2017 baada ya Rais John Pombe Magufuli kuzuia makontena ya mchanga wa madini, makinikia, ya kampuni hiyo kusafirishwa nje ya nchi.

Mwaka 2017 serikali ya Tanzania ilidai kuwa inaidai Acaccia dola bilioni 190 abazo ni kodi kampuni hiyo ilikwepa kulipa toka ilipoanza shughuli zake nchini humo.

Japo Acacia ilakana, kampuni mama ya Barrick Gold ilikubali kufanya mazungumzo na serikali ya Tanzania na kufikia makubaliano ya kuanza upya kwa kuaminiana.

Vilevile kampuni hiyo iliahidi kutoa Dola za Kimarekani milioni 300 kama malipo ya kuonesha nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kutokana na biashara ya kampuni hiyo. Kwa mujibu wa jarida la biashara la Uingereza la Financial Times, kampuni hiyo bado ingali ikitafuta pesa hiyo.

Haki miliki ya picha IKULU TANZANIA
Image caption Mkurugenzi wa Barrick Prof Thornton aliahidi 2017 kutoa Dola za Kimarekani milioni 300 kama malipo ya kuonesha nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato, lakini Finacial Times wanaripoti kuwa pesa hizo hazijalipwa bado.

Tayari baadhi ya maafisa wa kampuni hiyo wanakabiliwa na mashtaka mahakamani nchini Tanzania kwa kutuhumiwa kutenda makosa ya uhalifu wa kiuchumi, biashara haramu ya fedha, udanganyifu, na ukwepaji kulipa kodi.

Vigogo hao ni pamoja na Mkurugenzi mtendaji wa Acacia Mining, Asa Mwaipopo ,Deogratias Mwanyika aliyekuwa makamu wa rais wa kampuni ya Barrick Gold na mkurugenzi wa mawasiliano wa kampuni ya Bulyanhulu mine Alex Lugendo mwenye umri wa miaka 41.

Januari 9 Rais wa Tanzania alimuapisha waziri mpya wa Madini, Dotto Biteko na kuelezwa wazi kutoridhishwa na utendaji wa wizara hiyo hususani katika udhibiti wa utoroshaji wa madini.

Magufuli amemtaka Biteko na taasisi zilizo chini ya wizara yake kushirikiana na Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania kuanzisha vituo vya ununuzi wa madini ili kudhibiti utoroshaji na kuiwezesha Benki Kuu kuwa na hifadhi ya dhahabu.

"Tumewaruhusu wawekezaji na wachimbaji wadogo wachimbe dhahabu, Je Wizara ya Madini mmeshajiuliza dhahabu inayochimbwa inauzwa wapi? Na je kama wanachimba na wanauza sisi tunapata asilimia ngapi? Hili suala ni la Wizara ya Madini, halikuwa suala la Bunge kujiuliza, wala halikuwa suala la Waziri Mkuu au Rais kujiuliza.

"Kwenye sheria ya madini nina hakika kuna mahali imeelekeza kuanzishwa kwa vituo vya kuuzia madini, je vimeanzishwa vituo vingapi? viko wapi? Kwa sababu vingeanzishwa vituo hivi tungejua dhahabu inayosafirishwa, wapi imeuzwa na inawezekana tungekuwa na taarifa za kila wiki, lakini hakuna" amesemaRais Magufuli.

Mada zinazohusiana