Rais Uhuru Kenyatta amejitenga na baadhi ya wanasiasa Jubilee wanaompinga naibu wake

Kenyatta na Odinga wamekuahidi kuwaunganisha Wakenya Haki miliki ya picha Reuters

Dhoruba kali iliyokikumba chama tawala cha Kenya Jubilee imeanza kutilia shaka iwapo demokrasia ya vyama vingi imeshika mizizi ama ni siasa zisiokuwa na misingi ya vyama ambazo zimeendelea kuwepo hata chini ya mfumo wa vyama vingi.

Dhoruba hii inatokana na matamshi ya hivi karibuni yaliyotolewa na aliyekuwa naibu mwenyeketi wa kitaifa wa chama cha Jubilee, David Murathe kuwa alikuwa ameanzisha juhudi za kuhakikisha kuwa Naibu Rais wa Kenya William Ruto angefaulu katika juhudi zake za kupata uongozi wa nchi katika uchaguzi ujao, 2022.

Rais Uhuru Kenyatta ambaye pia ni kiongozi wa chama tawala cha Jubilee alimejitenga na baadhi ya wanasiasa katika chama chake cha Jubilee wanaompinga naibu wake, Bwana Ruto, kuchukua hatamu za uongozi wa nchi badala yake akisema kuwa chama chake cha Jubilee kina mipango yake kuhusiana na siasa za urithi wa kiti cha Urais mnano mwaka wa 2022.

Hata hivyo, cheche za matamshi ya hisia kali kutoka kwa wendani wa Naibu Rais William Ruto ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama tawala cha Jubilee nchini Kenya kwa upande mmoja na wale wanamuunga Rais Kenyatta kwa upande mwingine zimeendelea.

Bwana Murathe alijiuzulu wadhifa wake na kudai kuwa hangeweza kufanya kazi kwenye chama tawala pamoja na aliyekuwa akimpinga na kueleza kuwa angekwenda mahakama ya juu zaidi kuhakikisha kuwa amezima azma ya Naibu Rais wa Kenya, Bwana William Ruto.

Majibizano yaliyotokana na matamshi ya Bwana Murathe na shutuma za pande mbali mbali zimepelekea kuonekana kufanya chama cha Jubilee kutokuwa imara kwa sababu ya tofauti kuhusiana na uongozini chamani.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Makamu wa Rais William Ruto (mwenye kofia)

Huku haya yakiendelea, baadhi ya wendani wa naibu Rais William Ruto walitisha kuleta hoja ya kutokuwa na imani na Rais Kenyatta wakidai kuwa alikuwa amekwenda kinyume na makubaliano ya viongozi hao wawili kusaidiana katika kuhakikisha kuwa kila mmoja wao anaiongoza Kenya kwa miaka kumi kila mmoja.

Hata ingawa baadhi ya viongozi hao walidai kutia saini kuhakikisha kuwa hatua hiyo ingefaulu, huenda wasifaulu kwa sababu idadi inayohitajika kuunga mkono mswaada kama huo bungeni huenda wasiipate. Aidha, wengi wa wabunge wa upinzani huenda wasiwaunge mkono katika hatua hiyo.

Yanayoendelea kwenye vyama vya kisiasa nchini Kenya yanatilia shaka misingi ya vyama hivyo na iwapo muundo na usimamizi wa vyama vya kisiasa nchini Kenya unasaidia katika kushiriki kwa vyama hivyo katika kuendeleza demokrasi nchini Kenya kwa kuzingatia maoni na maono ya Wakenya ni jambo la kutiliwa shaka.

Ni dhahiri kuwa malengo ya vyama hivi na wananchi wa kawaida ni mambo yaliyo katika dunia mbili tofauti: Vyama vya kisiasa vikitafuta uungwaji mkono kushika hatamu za uongozi na kwa upande mwingine, wananchi wa kawaida wakijitafutia mahitaji yao ya kila siku

Kwa kuwa uchaguzi mkuu huwa kama kufa kupona nchini Kenya, wanasiasa wamekuwa wakivitumia vyama vya kisiasa kuhakikisha wanaendeleza malengo yao ya kisiasa na kinafsi; sababu moja inayoeleza ni kwa nini huwa kuna ghasia kila mara katika teuzi za vyama wakati wa uchaguzi mkuu na wakati mwingine baada ya uchaguzi mkuu.

Haki miliki ya picha AFP/GETTY
Image caption Upigaji kura Kenya

Wengi wanakubaliana kuwa ghasia za kisiasa ndani na nje ya vyama vya kisiasa zina misingi yake katika siasa za Rais mstaafu Daniel Moi ambaye alishikilia hatamu za uongozi hadi mwaka wa 2002 na aliyetumia mbinu ya tenga utawale sana wakati aliposhinikizwa kuanzisha mfumo wa vyama vingi nchini Kenya.

Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyuama vingi nchini Kenya, wataalamu wa siasa za Kenya wanaeleza kuwa vyama vingi vilivyoundwa wakati huo na hata sasa vimekuwa na misingi ya kikabila jambo ambalo limekuwa likitatiza maendeleo ya demokrasia ya vyama nchini Kenya.

Kwa hakika, chama kikuu cha upinzani nchini Kenya, Orange Democratic Movement(ODM) kiliundwa kutokana na kura ya maamuzi ya mwaka 2005 ambapo wale wote waliopinga kura ya maamuzi akati huu walijumuika na kukiunda.

Hii ndiyo sababu sasa kuna hofu kuwa wale wanaopigania kura ya maamuzi kufanywa nchini Kenya kabla ya uchanguzi wa mwaka wa 2022 wana njama ya kuhakikisha kuwa kuna chama kipya cha kisiasa nchini Kenya ili kukitumia kwenye uchaguzi wa 2022.

Hata hivyo, ikukumbukwe kuwa katiba na sheria inayosimamia vyama vya kisiasa nchini Kenya inavipa fursa vyama vya kiasa kupokea fedha kutoka kwa mfuko wa serikali ili kuendeleza shughuli zao ingawa vyama hivi havijakuwa vikifanya hivi baada ya katiba mpya ya mwaka wa 2010.

Ingawa chama tawala cha Jubilee na chama cha upinzani cha Orange Democratic (ODM) ndivyo vyama vikuu vya kisiasa nchini Kenya, havijawahi kuwa na uchaguzi.

Chama kikuu cha upinzani ODM kilipojaribu kufanya uchaguzi wake miaka ya nyuma, kilikumbwa na migawanyiko mikubwa ambayo ilipelekea kuwekwa afisini kwa viongozi wasimamizi hadi leo.

Kiongozi wa ODM ambaye pia ni kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amewahi kushikilia kuwa vyama vya upinzani vinafaa kuwa na uwezo wa kuamua jinsi ya kuwachagua wanachama wake watakaongangania nafasi mbali mbali za kisiasa nchini Kenya bila hata kufanya uchaguzi chamani.

Kando na kutokuwepo na uchaguzi kwenye vyama vya kisiasa ambako kunapelekea kuyumbayumba kwa vyama hivyo baada ya uchaguzi mkuu, baadhi ya vyama hivyo huwa vinaanzishwa katika misingi ya kikabila kutokana na ukweli kwamba wanaovinzisha huwa na misingi hiyo.

Haki miliki ya picha MUSALIA MUDAVADI
Image caption Musalia Mudavadi

Hali hii inawaacha wanachama na chama chenyewe katika hali ngumu ya maisha ya kisiasa.

Hali hii labda inaweza kueleza ni kwa nini vyama hivi huwa havina matawi katika sehemu na kaunti mbali mbali nchini kama sheria ya vyama inavyohitaji vyama kufanya.

Kwa sababu ya kuwa vyama vyenyewe vina wasimamizi na maafisa ambao hawakuchaguliwa, mshikamano wa kuuza sera ya chama ni suala ambalo halijawahi kuonekana nchini Kenya isipokuwa kusikika tu wakati tarehe ya uchaguzi mkuu inapotangazwa.

Haya yanakwenda sambamba na kukosekana kwa nidhamu katika vyama vya kisiasa na viongozi wake kwani misingi ya kuundwa vyama vyenye, malengo na maono ya vyama ni maadili ambayo hayana mguso miongoni mwa wanachama.

Hii ndio sababu wakati mwingine hata viongozi wa vyama nchini Kenya hutofautiana hadharani kuhusiana na sera ambali mbali kwa sababu ya misingi ya uundwaji wake isiyo dhabiti.

Hali kama hii inaonekana katika ushirikiano kati ya chama tawala cha Jubilee na muungano wa upinzani NASA unaonyesha dalili kama hizi maana ni wakuu wa vyama ambao wanaonekana kufanya maamuzi bila kuwasjhirklisha wanachama wake.

Haki miliki ya picha AFP/GETTY
Image caption Kalonzo Musyoka(kulia) na Raila Odinga(kushoto

Kwa mfano, ushirikiano kati ya kiongozi wa Jubilee Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ulipoanza, baadhi ya viongozi wa muungani wa NASA kama vile Moses Wetangula, Musalia Mudavadi na Kalonzo Musyoka hawakuunga mkono kwa kuwa walidai kutojulishwa malengo yake hata ingawa baadaye wameonekana kuunga mkono ushirikiano huo.

Lililo bayana ni kuwa vyama vya kiaisa nchini Kenya kwa sasa vimebaki vyombo vya kutumiwa na viongozi wa kisiasa katika kufikia malengo yao ya kibinafsi na itachukua muda mrefu kwa mfumo wa vyama vingi kuchukua mkondo wa kuendeleza vyama hivyo ili kuchangia ukuaji wa demokrasi na kujali maslahi ya walio wengi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii