Je wapiganaji wa al-Shabab kutoka Somalia wana malengo gani?

Wapoiganaji wa Somalia al-Shabab Haki miliki ya picha AFP

Kundi la wapiganaji la al-shabab linakabiliana na serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Somalia na limefanya misururu ya mshambulizi katika eneo zima.

Kundi hilo linalohusishwa na al-Qaeda limefurushwa katika miji mingi lililodhibiti lakini linasalia kuwa hatari.

Neno al-Shabab linamaanisha vijana kwa lugha ya kiarabu.

Lilijitokeza kutokana na kundi lenye ititakadi kali la Muungano wa mahakama za kiislamu nchini Somali ambalo lilikuwa likidhibiti mji wa Mogadishu 2006, kabla ya kufurushwa na vikosi vya Ethiopia.

Kuna ripoti kadhaa za wapiganaji wa Jihad wa kigeni wanaoelekea Somalia kusaidia al-Shabab, kutoka mataifa jirani pamoja na Marekani na Ulaya.

Limepigwa marufuku kama kundi la kigaidi na Marekani pamoja na Uingereza na linaaminika kuwa na kati ya wapiganaji 7000 na 9000.

Al-Shabab linahubiri Uislamu wa madhahabu ya Wahhabi kutoka Saudia huku raia wengi wa Somali wakiwa wa madhahabu ya Sufi.

Limeweka sheria kali za Kiislamu katika maeneo linayodhibiti , ikiwemo kumpiga mawe hadi kufa mwanamke anayetuhumiwa kuzini mbali na kuwakata mikono wezi.

Je kuna uhusiano gani na wana Jihad wengine?

Haki miliki ya picha AFP

Katika kanda ya video iliotolewa mwezi Februari 2012 , kiongozi wa al-Shabab wakati huo Ahmed Abdi Godane alisema kuwa aliahidi kumtii kiongozi wa al-Qaeda Ayman al-Zawahiri.

Pia kumekuwa na ripoti kadhaa kwamba kundi la wapiganaji wa al-Shabab huenda limeazisha ushirikiano na makundi mengine ya wapiganaji barani Afrika, kama vile Boko Haram nchini Nigeria na al-Qaeda katika kundi la Islamic Maghreb wenye makao yao makuu katika jangwa la Sahara,

Al-Shabab lilijadili iwapo lijiunge na kundi la wapiganaji wa Islamic State lilipochipuka mnamo mwezi Januari 2014.

Mara ya kwanza lilipinga wazo hilo na kusababisha kuvunjika kidogo.

Kwa sasa kundi la al-Shabab linaongozwa na Ahmad Umar anayejulikana kama Abu Ubaidah.

Marekani iliahidi kutoa $6m (£4.5m) kwa habari iliopelekea kukamatwa kwake.

Je al-Shabab ni hatari kwa kiasi gani?

Haki miliki ya picha AFP

Serikali ya Somalia imelaumu kundi hilo kwa mauaji ya takriban raia 500 wa Somalia katika shambulio la bomu lililoegeshwa ndani ya lori kubwa katika mji mkuu wa Mogadishu mwezi October 2017.

Lilikuwa shambulio baya la bomu kutokea katika eneo la mashariki ya kati. Kundi la al-Shabab hatahivyo halikukiri kutekeleza shambulio hilo.

Kundi hilo lilikiri kutekeleza shambulio kubwa katika kambi moja ya kijeshi katika eneo la el-Ade nchini Somalia mwezi Januari 2016, na kuwaua wanajeshi 180 kulingana na aliyekuwa rais wa taifa hilo Hassan Sheikh Mohamud.

Jeshi la Kenya lilipinga idadi hiyo lakini likakataa kutoa idadi ya wanajeshi waliouawa.

Pia limetekeleza mashambulio kadhaa nchini Kenya ikiwemo mauaji ya wanafunzi katika chuo kikuu cha Garissa , karibu na mpaka na Somalia.

Jumla ya watu 148 walifariki wakati wapiganaji walivamia Chuo hicho mapema alfajiri na kuwalenga wanafunzi Wakristo.

Mwaka 2013, wapiganaji wake walivamia duka la jumla la West Gate jijini Nairobi na kusababisha vifo vya takriban watu 67.

Wakati wa mechi ya kombe la dunia kati ya Uhispania na Uholanzi, lilishambulia kilabu moja ya mpira wa raga pamoja na mkahawa katika mji mkuu wa Uganda ,Kampala na kuwaua watu 74 waliokuwa wakitizama mechi hiyo.

Je kundi la al-Shabab linadhibiti kiwango gani cha Somalia?

Lilifurushwa kutoka mji mkuu wa, Mogadishu, mwezi Agosti 2011 kufuatia uvamizi uliotekelezwa na wanajeshi 22,000 wa muungano wa Afrika na kuondoka katika bandari muhimu ya Kismayu mwezi Septemba 2012.

Wakati lilipoondolewa katika bandari ya Kismayu kundi hilo lilipoteza fedha nyingi kwa kuwa lilikuwa likijipatia fedha hizo kupitia uuzaji wa makaaa.

Marekani pia imetekeleza msururu kadhaa wa mashambulio, hatua iliosababisha kuuwawa kwa kiongozi wa kundi hilo Aden Hashi Ayro, mwaka 2008 na mtangulizi wake , Ahmed Abdi Godane.

Mwezi Machi 2017, rais wa Marekani Donald Trump aliidhinisha mipango ya Pentagon kuendeleza operesheni zake dhidi ya al-Shabab.

Marekani ina zaidi ya wanajeshi 500 nchini Somalia na imetekeleza mashambulio 30 mwaka 2017, ikiwa ni mara nne zaidi ya jumla ya mashambulio iliotekeleza miaka saba iliopita kulingana na gazetri la The Washington Post.

Ijapokuwa operesheni hiyo ya Marekani inazidi kudhoofisha kundi hilo la al-Shabab, kundi hilo linaendelea kutekeleza mashambulio ya kujitolea muhanga na limeteka baadhi ya miji.

Muungano wa Afrika unapunguza idadi ya wanajeshi wake-huku wanajeshi 1000 wakiondoka na wengine 1000 wakitarajiwa kuondoka 2018.

Hii inatokana na kupunguzwa kwa ufadhili na muungano wa Ulaya EU kufuatia madai ya ufisadi nadni ya wanajeshi wa muungano wa Afrika AU, unaoshirikisha wanajeshi wa Uganda, Kenya, Burundi na Djibout.

Ni nini kinachoendelea Somalia?

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Somalia haijakuwa na serikali thabiti kwa zaidi ya miaka 20, ambapo eneo kubwa la nchi hjiyo limekuwa katika vita.

Somalia haijakuwa na serikali thabiti kwa zaidi ya miaka 20, ambapo eneo kubwa la nchi hjiyo limekuwa katika vita.

Al-shabab linapata uungwaji mkono kwa kuwaahidi watu usalama. Lakini uaminifu wake ulipigwa teke wakati lilipokataa chakula kutoka eneo la Magharibi ili kukabiliana na ukame uliokumba taifa hilo mwaka 2011.

Huku Mogadishu na miji mingine ikiwa imezungukwa, kuna hisia za matumaini na raia wengi wa Somalia wamerudi nyumbani kutoka mafichoni huku wakileta fedha na ujuzi wao pamoja.

Huduma za kawaida kama vile taa za barabarani, dhobi na usafishaji wa mji umeanza katika mji wa Mogadishu.

Lakini taifa la Somalia bado ni hatari na limegawanyika katika kufanya uchaguzi wa kidemokrasia - huku wa mwisho ukiwahi kufanyika 1969.

Hivyobasi bunge lake na rais wake huchaguliwa kupitia mfumo mgumu, huku viongozi wa kiukoo wakichukua jukumu muhimu.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii