Hoteli ya Nairobi: Walioshambulia DusitD2 waangamizwa

Mmojawapo ya maafisa wa usalama
Image caption Shambulio la hoteli ya DusitD2

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema kuwa kuwa vita dhidi ya watuhumiwa wa uvamizi jijini Nairobi vimekamilika na wavamizi wote wameangamizwa.

Wapiganaji walivamia hoteli hiyo iliopo katika eneo la Westlands siku ya Jumanne na kuwaua takriban watu 14.

Maafisa walitangaza kukamilika kwa makabiliano hayo saa chache yalipoanza , lakini ufyatulianaji wa risasi pamoja na milipuko ilisikika tena mapema siku ya Jumatano.

Wakati huohuo washukiwa wawili wamekamatwa na maafisa wa jinai kufuatia shambulio la kigaidi katika hoteli ya DusitD2 iliopo katika eneo la Riverside Jijini Nairobi.

Mkurugenzi wa kitengo cha jinai George Kinoti amesema kuwa washukiwa hao walikamatwa katika eneo la Eastleigh na Ruaka ambapo mmojawapo wa washambuliaji alikuwa akiishi.

Kundi la wapiganaji wa Somalia la al-Shabab lilikiri kuhusika na shambulio hilo.

Haijulikani ni washambuliaji wangapi waliovamia hoteli hiyo. Eneo hilo linamiliki hoteli hiyo pamoja na afisi nyengine.

Kupitia hotuba yake kwa taifa iliopeperushwa hewani na runinga, rais Kenyatta alisema kwamba takriban watu 14 wameuawa lakini wengine 700 waliokolewa kutoka eneo hilo.

Raia wa Marekani ni miongoni mwa waliouawa , idara moja ya Marekani imemtaja kuwa Jason Spindler.

Raia wa Uingereza mwenye uraia mwengine wa mataifa ya Afrika Kusini pamoja na raia mwengine wa Uingereza walijeruhiwa , afisi ya maswala ya kigeni nchini humo imesemna.

"Naweza kuthibitisha kwamba . operesheni ya usalama katika hoteli ya Dusit imekamilika na magaidi wote wameuawa'' , rais huyo wa Kenya alisema.

Tutawatafuta na kuwasaka wale wote waliohusika katika kufadhili , kupanga na kutekeleza kitendo hiki cha kinyama'' , aliongezea, akiapa kuwasaka kwa hali na mali.

''Hili ni taifa linaloongozwa kwa sheria, taifa linalopendelea watu kuishi kwa amani....Nataka kusisitiza kuwa hili ni taifa lisilosahau wale wanaowadhuru watoto wetu''

Baada ya saa 19 za ukatili, ufyatulianaji wa risasi na umwagikaji wa damu pamoja na makabiliano katika hoteli hiyo iliopo katika eneo la Westlands yalikwisha kwa ghafla muda wa alfajiri.

Usiku kucha raia waliokuwa katika hoteli hiyo wakijificha chooni ama ndani ya ofisi walisindikizwa na maafisa wa usalama huku kukiwa na ufyatulianaji wa risasi wakati wa mlipuko wa bomu ulioendelea hadi asubuhi.

Katika barabara zilizojaa watu nje ya majengo hayo marafiki na jamii waliwakumbatia wale waliokolewa na kuvishukuru vikosi vya usalama vya Kenya.

Ambalensi zilizokuwa zimeegeshwa nje ya majumba hayo ziliwachukuwa wale waliokuwa wamejeruhiwa na kuwapeleka hospitalini.

Utalii wa Kenya umeathiriwa tena na shambulizi la kigaidi, tukikumbuka Westgate 2015 na shambulio la chuo kikuu cha Garissa mbali na ushauri mbaya wa kutosafiri kuelekea Kenya unaotelowa na mataifa ya kigeni..

Leo tunawahakikishia Wakenya wote kwamba wako salama.

Shambulio hilo ni kumbusho kwamba wapiganaji wa al-Shabab bado wana uwezo mkubwa wakiwa na uwezo wa kutekeleza shambulio kali katika eneo linalolindwa sana katika taifa jirani.

Je wavamizi walitekeleza vipi shambulio hilo?

Shambulio hilo lilianza mwendo wa saa tisa jioni siku ya Jumanne wakati wapiganaji wanne walirusha mabomu katika magari yaliokuwa yameegeshwa kabla ya kuingia ndani ambapo mmoja wao alijilipua, kulingana na maafisa wa polisi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Washambuliaji wawili walioonekana hapa qwalipokuwa wakiingia

Mwanamke aliyekuwa akifanya kazi katika jumba jirani aliambia reuters: Nilianza kusikia milio ya risasi na kuwaona watu wakitoroka wakibeba mikono yao juu ya vichwa huku wengine wakiingia katika benki ili kujificha.

Kamera za usalama zilionyesha takriban watu wanne waliokuwa wamejihami wakiingia na kufyatua risasi.

Kuna ripoti walionekana wakitembelea eneo hilo katika siku za hivi karibuni.

Kufikia mwendo wa saa tano waziri wa usalama Fred Matiang'i alisema kuwa ,usalama umeimarishwa katika majengo yote yaliokuwa katika eneo hilo.

''Usalama umeimarishwa na taifa lipo salama'' , aliambia wanahabari. ''Ugaidi hautatushinda''.

Lakini saa moja baadaye ufyatulianaji wa risasi na milipuko iliripoitiwa katika eneo hilo.

Kulikuwa na ufyatulianaji mwengine mkali mwendo wa saa moja.

Maafisa wa usalama walilipekua eneo hilo na kuingia ambapo walikutana na wafanyikazi walioogopa. Alafajiri siku ya Jumatano , zaidi ya watu 100 waliokolewa.

Takriban watu 30 wanatibiwa katika hospitali ya Nairobi kulingana na ripoti ya vyombo vya habari.

Hoteli hiyo ya DusitD2 ina vyumba 101. ikiwa katika eneo la Westlands , dakika chache kutoka katikakati mwa jiji la Nairobi ina migahawa kadhaa.

Kenya imeshuhudia visa kadhaa vya mashambulizi katika siku za hivi karibuni-hususan katika maeneo yaliopo karibu na Somalia pamoja na mji mkuu wa Kenya.

Je waliojipata ndani ya hoteli hiyo wanasemaje?

Wakati wapiganaji hao walipoingia katika eneo hilo kulikuwa na mkanganyiko , kwa sababu watu walianza kutoroka na kulazimika kurudi katika jumba hilo waliposhambuliwa na risasi.

Shahidi mmoja Faith Chepchirchir aliambia Reuters: watu walikuwa wakijaribu kukimbia katika lango kuu la hoteli hiyo, lakini baadaye nikaona kila mtu aliyekuwa akielekea katika lango hilo akirudi.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Raia wengi walikwama katika hoteli hiyo kwa saa kadhaa

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii