Idadi ya waliofariki katika shambulio Kenya yaongezeka hadi 21

Left: James Oduor. Top centre: Feisal Ahmed Top. Right: Luke Potter Bottom centre: Jason Spindler. Bottom right: Abdalla Dahir Haki miliki ya picha © Various

Idadi ya watu waliofariki katika shambulio la wanamgambo wa Alshabaab, walipoivamia hoteli moja mjini Nairobi imeongezeka hadi 21 kwa mujibu wa serikali.

Mamia ya watu walilazimika kutoroka umwagikaji damu ulioshuhudiwa katika hoteli ya DusitD2 na jengo la kibiashara siku ya Jumanne.

Watu 28 waliojeruhiwa wamelazwa katika hospitali, huku wengine 19 ambao walikuwa hawajulikani waliko, wakipatikana kwa mujibu wa shirika la msalaba mwekundu.

Kundi lililoko nchini Somalia al-Shabab limekiri kuhusika na shambulio hilo, lililozusha operesheni ya saa 19 ya kiusalama.

Rais Uhuru Kenyatta Jana Jumatano alitangaza kwamba washambuliaji hao wameangamizwa na kwamba operesheni ya uokozi imekamilika.

Kenya imekuwa ikilengwa na kundi la al Shabab tangu Okotoba 2011, wakati taifa hilo lilipotuma vikosi vyake nchini Somalia kupambana na kundi hilo la jihadi.

Miongoni mwa wahanga wa shambulio hilo ni pamoja na mmoja aliyeponea shambulio la kigaidi la 9/11 , Shabiki sugu wa soka, na marafiki wawili wa dhati.

Haya ndiyo tunayoyafahamu kuwahusu kufikia sasa:

Feisal Ahmed na Abdalla Dahir

Haki miliki ya picha Family

Feisal Ahmed, mwenye umri wa miaka 31, na Abdalla Dahir, wa miaka 33, washauri waliofanya na kampuni ya kimataifa Adam Smith International (ASI), walikuwa wakila chakula cha mchana pamoja katika mgahawa wa Secret Garden uliopo katika sehemu ya chini ya hoteli hiyo wakati mlipuaji wa kujitoa muhanga alipojilipua.

Rafiki na jamaa zao wamewaeleza Ahmed na Dahir kama marafiki wasiotengana.

"Walikuwa na uhusiano wa karibu sana," Shemegi yake Ahmed Abdullahi Keinan ameliambia shirika la habari la Reuters.

"Walikuwa na uhusiano wa karibu sana kiasi cha watu hata kusema watakufa pamoja."

Haki miliki ya picha Family
Image caption Abdalla Dahir (kushoto) na Feisal Ahmed (kulia) wanasemekana kuwa na ukaribu sana

Walikuwa wakifanya kazi katika wakfu wa ustawi wa Somalia uliosimamiwa na ASI "kuleta amani na ustawi kwa nchi ya Somalia", ASI imesema katika mtandao wake.

Mkewe Ahmed inaarifiwa ni mja mzito.

Akaunti ya Dahir katika mtandao wa kijamii wa LinkedIn inasema alikuwa anapenda sana kupiga picha na "kuangazia kuhusu watu walio katika hatari hususan waathiriwa wa vita wasiokuwa na sauti, katika kuuelimisha ulimwengu kuhusu athari kubwa za vita".

Wamezikwa pamoja jana Jumatano.

Jason Spindler

Haki miliki ya picha Jason Spindler

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya teknolojia, raia wa Marekani aliponea shambulio la kigaidi la Septemba 11 katika jengo la World Trade Centre mjini New York mnamo 2001 alikuwa miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo.

"Ni kwa moyo mzito, inabidi nitangaze kifo cha kakangu Jason Spindler aliyefariki asubuhi hii katika shambulio la kigaidi Nairobi, Kenya. Jason alikuwa manusura wa shambulio la 9/11 na ni mpambanaji. Najua aliwapa tabu sana!" kakake Jonathan aliandika katika ujumbe kwenye Facebook.

Spindler alikuwa akifanya kazi katika benki ya uwekezaji Salomon Smith Barney katika jengo hilo la World Trade Center wakati jengo hilo lilipo poromoka baada ya shambulio la 9/11 shirika la AFP linaripoti.

Muanzilishi mwenza na mkurugenzi mtendaji huyo wa I-Dev International - kampuni inayolenga uvumbuzi wa kifedha kupunguza umaskini - alikuwa akifanya kazi Kenya katika mradi wa kusambaza umeme katika maeneo ya mashinani.

Katika mahojiano na shirika la habari la NBC Marekani, mamake Sarah Spindler amesema Jason alikuwa anajaribu "kufanya mageuzi mazuri katika nchi za kimaskini kuingia katika masoko yanayoinukia"

James Oduor

Haki miliki ya picha James Oduor Cobra/Facebook

Kwa jina la utani "Odu Cobra" aliloitwa na rafiki zake, James Oduor alifariki mkesha wa siku yake ya kuzaliwa na alijulikana kwa kupenda sana soka.

Alifurahia sana mechi za mitaani na ameanzisha ukurasa wa mashabiki kwenye mtandao wa YouTube, Wadau TV, mwaka mmoja uliopita.

Alikuwa rafiki wa mhariri wa BBC Larry Madowo katika chuo kikuu aliyeandika ujumbe huu kwenye Twitter, "Alikuwa mojawapo ya watu wazuri , aliye na ucheshi niliyewahi kumtambua. Pumzika salama, Odu, nind maber [Kwa lugha ya Kijaluo - pumzika kwa amani]. Dunia i njema kutokana na uhai wako."

Kwa mujibu wa wanaomkumbuka na kutuma risala zao katika ukurasa uliofunguliwa kumuenzi, alikuwa shabiki sugu wa timu ya Manchester United katika ligi kuu ya England na aliichezea timu ya mtaani.

Alifanya kazi pia kwa kampuni ya vifaa vya elektroniki ya LG iliyo na makao yake katika jengo hilo lililoshambuliwa la Dusit.

Katika ujumbe wake wa mwisho kwenye Twitter, Oduor alisema alisikia milio ya "risasi na milipuko ya mfululizo" na akaeleza kwamba yeye na wenzake wamekwama.

Taarifa ya LG Electronics ilimtaja kama "mfanyakazi mzuri sana, lakinivpia binaadamu wa kweli aliyetia moyo".

Luke Potter

Haki miliki ya picha Gatsby Africa

Raia wa Uingereza Luke Potter alifanya kazi katika shirika la misaada la Gatsby Africa kama mkurugenzi wa miradi barani Afrika.

Katika mtandao wa kampuni hiyo ameeleza kuwa yeye ni mpenda michezo ya maji, na kutembea na kuzungumzia kujivinjari nje ya mji. Alihamia Nairobi hivi karibuni kutoka Uingereza.

"Naamini pakubwa kwa jamii kutoa nafasi sawa iwezekanavyo kwa kila mtu na kwamba hata wakati kuna ushindani ki uchumi na ni muhimu kujenga taifa, ustawi wa muda mrefu hauwezi kufikiwa hadi pale faida itakapogawanywa," alisema katika mtandao huo.

Gatsby Africa imesema katika taarifa yake alitumika miaka 10 "kusaidia baadhi ya watu walio maskini na katika hatari duniani".

"Tunasikitika na familia yake, mpenzi wake, binti yake na rafiki zake," Kampuni hiyo iliongeza.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii