Watetezi wa haki wanasema ni hatua kubwa ya kukomesha ubaguzi wa kijinsia.

Dhanya Sanal Haki miliki ya picha Dhanya Sanal
Image caption Dhanya Sanal alikua mwanamke wa kwanza kukwa mlima

Mwanamke mmoja nchini India amefanikiwa kuukwea mlima ambao hupandwa na wanaume pekee kwa sababu za kidini.

Dhanya Sanal alifikia kilele cha mlima Agasthyakoodam kufuatia uamuzi wa mahakama uliotolewa mwezi Novemba mwaka jana katika jimbo la kusini mwa Kerala.

Wanaume wa jimbo hilo wanapinga wanawake kukwe mlima huo kwasababu ya sanamu ya kihindi inayohusishwa na utakatifu.

Bi Sanal, 38, aliiambia BBC kuwa maandamano ya watu hayakumzuia kuukwea mlima huo.

Watetezi wa haki wanasema hatua hiyo ya Sanal, ni ushindi mkubwa katika harakati ya kukomesha ubaguzi wa kijinsia.

Bi Sanal anasema alikua tayari ''kubadili msimamo wake'' kama wanaume wa jamii yake wangelimzuia.

Anasema japo alikumbana na maandamano dhidi yake hakuna mtu yeyote aliyemzuia kuendelea mbele na safari.

Mwezi Novemba mwaka jana mahakama kuu mjini Kerala iliamua kuwa wanawake wanaweza kuukwea mlima huo wa urefu wa futi 6,128I.

Mahakama hiyo ilisema kua hatua ya kuwazuia wanawake inazingatia masuala ya kijinsia baada ya makundi ya wanawake kuwasilisha kesi mahakamani kupinga mila hiyo

Kundi hilo lilimpongeza Bi Sanal kwa hatua yake ya kuamua kuukwea mlima.

"Tumepiga hatua kubwa katika harakati ya kukomesha ubaguzi wa kijinsia mjini Kerala," Divya Divakaran, mmoja wa kundi hilo aliiambia BBC.

Haki miliki ya picha Sali Palode
Image caption Mlima Agasthyakoodam

Mlima Agasthyakoodam ambao uko magharibi mwa Ghats, ni wa pili kwa urefu katika eneo la Kerala.

Mahakama kuu ilipuuzilia mbali madai yaliyotolewana wanaume wa jamii zinazoishi chini ya mlima huo kwamba uamuzi huo unakiuka imani yao.

Walisema kuwa wanaabudu wanabudu sanamu kwa jina Agastya, na kwamba wanawake hawaruhusiwi kufika karibu eneo hilo kwa sababu ni patakatifu.

Kukwea mlima huo huwachukua watu hadi siku tatu kufikia kilele chake.

"Ni vigumu sana kufanya zoezi hili, unahitaji kufanya mazoezi ya ziada ya viungo kufika kileleni," Bi Sanal aliliambia gazeti la Times nchini India.

Alikua mwanamke wa pekee katika kundi la wakwea mlima 100. Kundi hili liliungana na maafisa wa misitu kike wawili.

Maafisa wameiambia BBC kuwa zaidi ya wanawake 100 wamejisajili kushiriki zoezi la kukwea mlima huo wiki chache zijazo

Haki miliki ya picha Sali Palode

Mapema mwezi huu wanawake wawili waliandikisha historia ya mjini Kerala baada ya wao kuingia hekalu la Hindu licha ya maandamano ya miezi kadhaa ya kuwazuia kuingia.

Kihistoria wanawake ''waliobaleghe'' wamepigwa marufuku kuingia katika Hekalu la Sabarimala - wakiwa na umri kati ya miaka 10 na 50.

Waumini wa dhehebu la Hindu wanaamini kuwa mwanamke aliye na hedhi ni mchafu na kwamba hastahili kushiriki matambiko yoyote za kidini

Hatua ya wanawake hao kuingia katika hekalu hiyo ilisababisha maandamani makubwa kote katika jimbo la Kerala.

Mmoja wao anaendelea kupata matibabu hospitalini baada ya mama mkwe wake kumshambulia kwa kuingia mahali patakatifu.

Siku ya Jumatano maafisa wamesema kuwa waandamanaji waliwazuia wanawake wawili kuingia katika hekalu hilo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii