Je ni vipi unapaswa kumwelezea mtoto taarifa za ugaidi pindi yanapotokea?

Watoto wakiwa katika darasa

Katika nchi za Afrika kumekuwa na matukio kadhaa ya kigaidi hususan tukio la hivi karibuni lililotokea Kenya katika Hoteli ya Dusit D2 na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa.

Miongoni mwa waliofariki ama kujeruhiwa ni wazazi wenye watoto, au hata ndugu wa karibu wa familia zenye watoto kadhaa.

Mtoto anaweza hoji baada ya kusikia shuleni, nyumbani kwa majirani au kwenye vyombo vya habari. Je akihoji, ni namna gani ya kumweleza ili kumsaidia na kumwondoa katika dimbwi la hofu?

BBC imezungumza na Rebecca Theuri mratibu wa kikanda wa masuala ya Ulinzi na uhamiaji kutoka shirika la Save the children ambaye anasema ni vyema wazazi kutoa taarifa kwa watoto wao wenyewe ili kuepuka taarifa zinazoweza kumpotosha mtoto.

"Kama mtu mzima anaathirika kihisia basi kwa mtoto itakuwa hivyo hivyo, kwani watoto wanateseka zaidi.

Wazazi wawasaidie watoto waelewe nini kinaendelea, kisha wawasikilize watoto wana mawazo gani ama wanafikiri nini ili wapate mlango wa kuanzia kutoa taarifa sahihi kisha wawape taarifa sahihi zisizo potosha na kwa lugha isiyoweza kumwathiri mtoto," anasema Theuri

Hata hivyo ameonya kuhusu kuto waambia watoto habari hizo kwani watazitafuta wenyewe.

"Naelewa hofu ya wazazi lakini humlindi mtoto kwa kutomwambia, inategemea na umri wa mtoto kwani baadhi yao tayari wana simu zenye mtandao na ni rahisi kujionea wenyewe yanayo jiri.

Tena ni rahisi kupata taarifa zisizosahihi. Hivyo nawashauri wazazi wawachunguze watoto, wawahoji, wawasikilize na wawape taarifa sahihi taarifa zenye matumaini na za kuwalinda sio kila kitu," anaongeza

Kwa mujibu wa shirika la save the children- Hizi ndio njia za kumsaidia mtoto kuhusu matukio ya kigaidi.

  • Zungumza nao kuhusu ugaidi: Tenga muda wa kukaa na familia yako na kuzungumza tumia maneno rahisi juu ya uwepo wa watu wanaopambana na ugaidi, waondoe hofu.
  • Andaa njia mbadala wanaposafiri: Tambua njia mbadala wakati wa kwenda na kurudi shule, kazini au sehemu yoyote, wafanye madereva au watu katika nyumba yako wazitambue.
  • Pata taarifa sahihi: Sikiliza vyombo vya habari vya ndani na nje. Jifunze maonyo na milio ya hatari itumikayo katika jamii jako. Na jua nini cha kufanya.
  • Ukiona kitu, sema: Ukiona kitu au hali isiyo ya kawaida toa taarifa kwa polisi. Ondoka eneo hilo kama una wasiwasi. Wafundishe watoto kumwambia mtu mzima wakihisi kitu kisicho sahihi.
  • Tafuta mahala salama pa kujihifadhi: Jua chumba au mahali salama ambapo kama familia mnaweza kujihifadhi endapo pametokea ugaidi kisha wajulishe wenzio.
  • Jifunze CPR na huduma za dharura: Jifunze njia za kusaidia kutoa huduma ya kwanza kwani waweza okoa maisha ya mtoto. Si lazima wakati wa ugaidi pekee bali muda wowot.
  • Jifunze kuhusu mipango ya kupambana na hali za hatari: Jua namna shule zimejipanga kupambana na hali ya hatari na jinsi ya kujiokoa. Na kama utatakiwa kumfuata mtoto shuleni au kuna sehemu imeandaliwa.
  • Jipange: Weka vitu vya dharura sehemu ya wazi, jiandae kwa kuandaa vitu muhimu
  • Dhibiti vyombo vya habari: Walinde watoto na vyombo vya habari dhidi ya tukio la kigaidi linapo tokea.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii