Saleh Kiba: Babake msanii wa muziki wa bongo fleva Ali Kiba aaga dunia Tanzania

Ali Kiba
Image caption Msanii wa muziki wa bongo fleva apoteza babaake

Hali ya simanzi na huzuni imegubika familia ya msanii wa bongo Fleva Ali Kiba baada ya babake kufariki dunia mapema leo.

Mzee Saleh Kiba alifariki katika hospitali ya Muhimbili ambapo alikuwa amelazwa.

Kulingana na Gazeti la mwananchi nchini Tanzania ndugu mdogo wa mwanamuziki huyo ambaye pia ni msanii Abdu Kiba alithibitisha habari hizo.

Msanii huyo amesema kuwa msiba unafanyika katika mtaa wa Kariakoo eneo la Muheza ambapo ndio nyumbani kwao.

Kulingana na gazeti hilo afisa wa Uhisiano mwema katika hospitali ya Muhimbili Neema Mwangomo amesema kuwa Mzee Saleh alifikwa na mauti yake saa kumi na mbili alfajiri.

Aliongezea kuwa marehemu alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo tangu tarehe 27 mwezi Disemba.

Haki miliki ya picha Abdu Kiba/Facebook
Image caption Hivi ndivyo Abdu Kiba alivyoandika katika mtandao wake wa facebook kufuatia kifo cha babake

Kifo cha Mzee Kiba kinajiri miezi kadhaa baada ya wanawe ambao wamefanikiwa kama wasanii wa muziki kufanya harusi ya pamoja mjini Dar es Salaam.

Harusi hiyo iliofanyika mnamo mwezi April mwaka uliopita ilihudhuriwa na jamii na marafiki katika biashara ya muziki. Abdu Kiba alimuoa mpenziwe Wahida.

Harusi hiyo ilikuwa ya pili kwa Ali Kiba baada ya kufanya nyengine hapo awali katika eneo la Kongowea mjini Mombasa Kenya na mpenziwe wa siku nyingi Amina Khalef.

Harusi hiyo ya kiislamu kwa jina Nikkah ambapo mwanamume huenda msikitini ili kuoa ilifanywa katika msikiti wa Ummul Kulthum.

Miongoni mwa watu maarufu waliohudhuria harusi hiyo ni pamoja na gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho, Mkewe rais wa zamani wa Tanzania Salma Kikwete msanii Ommy Dimpoz, mchekeshaji Idriss Sultan, msanii Vanesa Mdee na watu wa familia yake.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii