Ufaransa imemuita mjumbe wa Italia kwa kauli hii kuhusu ya Afrika

Luigi di Maio ameishutumu Ufaransa kwa kushinikiza uhamiaji kwa kuharibu uchumi wa mataifa ya Afrika Haki miliki ya picha EPA
Image caption Luigi di Maio ameishutumu Ufaransa kwa kushinikiza uhamiaji kwa kuharibu uchumi wa mataifa ya Afrika

Ufaransa imeilalamikia Italia kutokana na matamshi ya naibu waziri mkuu wa nchini hiyo Luigi di Maio aliyesema kuwa ufaransa imekuwa ikinyonya rasilmali za mataifa ya Afrika yaliyokuwa koloni zao ili kulipa madeni ya ufaransa.

Siku ya Jumapili Bw. Di Maio alidai kwamba kwa kufanya hivyo Ufaransa ndio iliyochangia pakubwa kuongeza idadi ya wahamiaji wanaokurupuka Ulaya baada ya kushindwa kuhimili athari mbaya za kiuchumi makwao kutokana na kufilisiwa na Ufaransa.

Naibu waziri mkuu huyo wa chama tawala cha Five Star Movement (M5S) kinachoendeleza siasa kali za mrengo wa kulia japo hakufafanua, ameitaka EU kuichukulia hatua kali Ufaransa.

"Umoja wa Ulaya unapaswa kuichukulia hatua Ufaransa na mataifa mengine yote yaliyo na tabia za kama Ufaransa za kuifilisi Afrika na kushia kusababisha janga la wahamiaji wa kiuchumi, Waafrika wanapaswa kuwa Afrika, sio chini ya maji ya bahari ya Mediterenia," Alisikika akifoka.

Matamshi hayo yanakuja wakati Umoja wa mataifa umetoa taarifa nyengine tena ya kusema zaidi ya watu 170 wanahofiwa kufariki katika mikasa miwili tofauti ya hivi punde ya mashua zao kwenda mrama baada ya kufunga safari hizo hatari.

Kwa mtazamo wa Bw. Di Maio, Ufaransa, ingekuwa na uchumi wa 15 kwa ukubwa duniani badala ya wa 6, iwapo hawangekuwa wanatumia mali za Afrika kujineemesha wao.

"Watu wanaihama Afrika leo hii kwa sababu mataifa ya Ulaya na hasa Ufaransa hawajaacha kuyakandamiza mataifa ya Afrika kiuchumi kama mwendelezo wa ukoloni waliokuwa wakiufanya ."

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Zaidi ya wahamiaji 4,200 wanaarifiwa kuvuka kuingia Ulaya katika siku 16 za kwanza mwaka 2019

Duru za Ufaransa zilizonukuliwa na vyombo vya habari vya Uitaliano zimetaja matamshi ya Bw. Maio kuwa "kauli za uhasama usio na sababu ikizingatiwa uhusiano mzuri na wa ushirikiano baina ya Ufaransa na Italia ambao wote ni wanachama wa Umoja wa Ulaya".

Kufikia jana Jumatatu balozi wa Italia nchini Ufaransa, Teresa Castaldo, aliitwa na serikali ya rais Emmanuel Macron kujibu maswali ibuka kuhusu sintofahamu hiyo.

Hata hivyo Bw. Di Maio, ambaye pia ndiye waziri wa maswala ya Kiuchumi na ajira wa Italia kamwe hajaonesha dalili za kujutia kutoa kauli hizo tata.

Amezidi kuilaumu Ufaransa kwamba inaendelea kuzihadaa na kuyapunja mataifa ya kiafrika yaliyokuwa koloni zake hasa yale yanayoendelea kutumia sarafu ya CFA franc, ambayo inadhibitiwa kupitia mabenki na Idara ya hazina kuu ya serikali ya Ufaransa.

"Kutokana na hatua ya Ufaransa kuendelea kuchapisha sarafu ya CFA franc kwa mataifa 14 ya kiafrika, hapo ndipo wanapoupunja na kudidimiza uchumi wa mataifa hayo.

Matokeo yake raia wengi wa kiafrika wanatoroka makwao kama wakimbizi na kuishia kufariki katika bahari ya Mediterenia na wanaopona kuingia kwetu Ulaya kwa kutumia njia zisizo halali. Tatizo hilo litatatuliwa tu iwapo Ulaya itakuwa na ujasiri wa kukabiliana na ukoloni mambo leo unaoendelea sasa'' Di Maio amezidi kufafanua.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Balozi wa Italia nchini Ufaransa, Teresa Castaldo, aliitwa na serikali ya rais Emmanuel Macron kujibu maswali

Ufaransa kwa upande wake unadai sarafu hiyo ya CFA franc kwa mataifa husika ya Afrika ndio inayoleta utulivu katika uchumi wa nchi wanayoitumia.

Takwimu za Shirika la kimataifa linalohusika na maswala ya uhamiaji The International Organisation for Migration (IOM), zinaonesha zaidi ya wahamiaji wapatao 4,216 walivuka na kuingia Ulaya kupitia bahari katika kipindi cha siku 16 za mwezi huu wa kwanza wa Januari 2019 - ikiwa ni mara mbili idadi ya wakati kama huo huo mwaka jana.

Hata hivyo kuna wale pia waliolaumu biashara haramu ya ulanguzi.

Naibu waziri mkuu mwengine wa Italia Matteo Salvini, kupitia akaunti yake ya Facebook amesema '' Iwapo bandari, fuo za mataifa ya Ulaya zitaendelea kuwa wazi, basi walanguzi wa biashara ya kusafirisha watu kinyume cha sheria, wataendelea hata kama matokeo yake ni kuendeleza vifo vya wahanga hao".

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii