Mpasuko Venezuela : Maduro avunja mahusiano na Marekani baada ya nchi hiyo kutangaza kumtambua kiongozi wa upinzani kama rais wa mpito

Citizens raise their hands as Juan Guaido, President of the Venezuelan Parliament, announces that he assumes executive powers Haki miliki ya picha EPA
Image caption Guaidó 'akila kiapo' cha kuwa rais wa mpito wa Venezuela

Mzozo wa kisiasa nchini Venezuela umechukua sura mpya baada ya Marekani kumtambua rasmi kiongozi wa upinzani Juan Guaidó kama rais wa mpito.

Tayari kiongozi wa nchi hiyo Nicolas Madura amejibu mapigo kwa kuvunja uhusiano baina ya nchi hizo na kuwapa wanadiplomasia wa Marekani saa 72 kuondoka nchini humo.

Hata hivyo, Marekani imesema "rais mstaafu Maduro" hana tena mamlaka ya kuamuru hivyo.

Mataifa saba ya Amerika Kusini Brazil, Colombia, Chile, Peru, Ecuador, Argentina na Paraguay wametangaza kumuunga mkono Guaidó kama rais halali.

Canada pia imetangaza kumuunga mkono huku Umoja wa Ulaya (EU) wakitaka uchaguzi mpya ufanyike.

Nchi za Mexico, Bolivia na Cuba zimetangaza kuendelea kumuunga mkono Maduro.

Maduro aliapishwa kuendelea na awamu ya pili ya urais mapema mwezi huu baada ya uchaguzi wa mwezi Mei mwaka jana ambao ulisusiwa na upinzani na kutuhumiwa kuwa na kasoro kadhaa ikiwemo wizi wa kura.

Nini kilitokea Jumatano?

Jana Jumatano maelfu ya waandamanaji dhidi ya utawala wa Maduro waliingia barabarani kuendelea kushinikiza utawala huo ung'atoke.

Bw Guaidó ambaye ni kiongozi wa bunge alishiriki na kutangaza kuwa maandamano hayo yataendelea mpaka Venezuela ikombolewe moja kwa moja.

Kisha akala kiapo mbele ya umati uliokuwa ukisherehekea katika mji mkuu wa Caracas, "Ninaapa kuchukua rasmi madaraka ya uongozi kama raisi wa mpito." Kiongozi huyo ameahidi kuongoza serikali ya muda na kusimamia uchaguzi huru na wa haki.

Dakika chache baada ya kujitangaza rais wa mpito, rais wa Marekani Donald Trump alitangaza rasmi kuwa nchi yake inaunga mkono hatua hiyo. Tangazo hilo la Trump limeibua hisia kuwa Marekani ilikuwa ikijua jambo hilo lingetokea tangu awali.

Bw Guaidó na Marekani wamelitaka jeshi kuacha kumkingia kifua Maduro, hata hivyo waziri wa ulinzi amelaani hatua ya Guaidó, na kudai ni kibaraka wa Marekani.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Wanaharakati wanadai watu 14 wameuawa kwenye maandamano ya Jumatano

Katika taarifa yake, Trump ameukashifu utawala wa Maduro kama "haramu" na kudai kuwa bunge la nchi hiyo ndio "mhimili pekee halali wa utawala" nchini humo.

"Raia wa Venezuela kwa ushupavu wamepaza sauti dhidi ya Maduro na utawala wake na wamepigania uhuru na utawala wa sheria," imeeleza taaria hiyo.

Trump ameonya kuwa vikwazo vikali zaid vinaweza kuwekwa dhidi ya Venezuela. Pia amewaeleza wanahabari kuwa hafikirii kuchukua hatua za kijeshi lakini japo "mapendekezo yote ya nini cha kufanya bado yapo mezani."

Rais huyo amezitaka nchi nyengine kumuunga mkono Guaidó na tayari Umoja wa Nchi za Amerika (OAS) umetangaza kumtambua Guaidó kama rais. Venezuela ilijitoa OAS mwaka 2017 ikidai umoja huo ulikuwa ukiingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo.

Mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Venezuela yanadai kuwa watu 14 wameuawa kwenye maandamano ya Jumanne na Jumatano.

Majibu ya Maduro

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Maduro akipungia wafuasi wake wanaotaka asalie madarakani

Bw Maduro ameituhumu vikali Marekani akidai kuwa inajaribu kuitawala Venezuela kutokea Washington na kuwatuhumu wapinzani wake kujaribu kufanya mapinduzi.

"Tumeingiliwa mambo yetu ya ndani vyakutosha sasa. Tuna utu wetu na sisi, alaa!" aling'aka Maduro wakati akilihutubia taifa kupitia televisheni kutokea kasri la rais.

Mhariri wa BBC wa Amerika Kusini, Candace Piette,anasema kuwa Rais Maduro kwa sasa anafanya kila linalowezekana kulishawishi jeshi kuwa upande wake,ambapo amekuwa akiwapa vyeo maafisa wa jeshi ili kuhakikisha wanamlinda na kutetea madaraka yake.

Juan Guaidó ni nani?

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Bw Guaidó ameweza kuunganisha makundi ya upinzani ambayo yalikuwa yamesambaratika katika miaka ya hivi karibuni.

Bw Guaidó mwenye miaka 35 hakuwa mtu maarufu mpaka pale mapema mwezi huu alipochukua hatamu za urais wa bunge la Venezuela ambalo linatawaliwa na upinzani.

Baada tu ya kushika madaraka hayo, alidai kuwa ana haki kikatiba kuchukua mamlaka ya urais wa nchi mpaka uchaguzi mpya utakapofanyika.

Akiwa mwanafunzi, aliongoza maandamano dhidi ya rais wa zamani Hugo Chaves ambaye alimteua Maduro kumrithi kabla ya kufariki.

Bw Guaidó ameweza kuunganisha makundi ya upinzani ambayo yalikuwa yamesambaratika katika miaka ya hivi karibuni.

Upinzani ulishinda wingi bungeni mwaka 2015 lakini mwaka 2017 Maduro aliunda chombo kipya, baraza la katiba ambalo ndilo lenye mamlaka ya kutunga sheria.

Kwa nini watu wanaandamana ?

Maduro, ambaye amechukua mamlaka mwaka 2013 baada ya kifo cha Hugo Chavez, amekuwa akishutumiwa vikali ndani na nje ya nchi yake kwa tuhuma za uvunjaji wa haki za binaadamu na kushindwa kusimamia vizuri uchumi.

Kuna upungufu mkubwa wa huduma za kijamii nchini humo ikiwemo dawa na chakula, na takribani watu milioni tatu wanaarifiwa kuihama nchi hiyo.

Mfumuko wa bei wa mwaka ulifikia 1,300,000% kwa miezi 12 kwa mwaka 2018, kwa mujibu wa tafiti ya bunge la nchi hilo.

Hata hivyo wapo wale ambao wanamuunga mkono Maduro na kudai matatizo ya Venezuela yamesababishwa na wapinzani wa mrengo wa kulia wakiungwa mkono na Marekani pamoja na nchi jirani ambazo ni adui.

Wanadai kuwa vikwazo vya Marekani vimeifanya serikali yao kushindwa kulipa madeni ya nchi.