Bwana mmoja aliyekamatwa 'akijiibia gari lake' alipwa fidia nono

Lawrence Crosby Haki miliki ya picha CBS Chicago
Image caption Lawrence Crosby inaripotiwa alipigwa makonde na mateke zaidi ya 10 wakati akitiwa mbaroni.

Bwana mmoja ambaye alitiwa nguvuni na polisi jijini Illinois, Chicago Marekani kwa wizi wa gari ambalo ilibainika kuwa ni mali yake amefikia makubaliano ya nje ya mahakama na mamlaka za jiji kumlipa fidia.

Lawrence Crosby, alikuwa mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Northwestern akiwa miaka 25 wakati tukio hilo lilipotokea mwaka 2015.

Mwanamke mmoja alipiga simu polisi wakati Crosby alipokuwa akirekebisha gari yake na kudhania kuwa nimwizi anayejaribu kuliiba.

Mamlaka ya Mji wa Evanston watapigia kura baadae juu ya kiasi gani bwana huyo alipwe lakini wakili wake anasema itakuwa dola milioni 1.25.

Timothy Touhy, ambaye ni wakili wa Dkt Crosby, alitaja kima hicho alipohojiwa na gazeti la Chicago Tribune.

Dkt Crosby, ambaye ni Mmarekani Mweusi ameiambia CBS Chicago kuwa tukio lake litasaidia kuangazia suala la ubaguzi wa rangi nchini humo.

Mwanasheria wa jiji amenukuliwa na runinga ya ABC News akisema: "Malipo haya ya fidia ni kielelezo tu cha nia njema na si kukubali tuhuma."

Kwa mujibu wa Touhy, mteja wake alikuwa akirekebisha gari yake na kuonekana na mwanamke mmoja aliyedhani kuwa analiiba.

Alimfuatilia wakati akielekea kwenye makazi yake chuoni na kisha kuwapigia simu polisi.

Baada ya kusimamishwa na polisi alitoka kwenye gari mikono ikiwa juu lakini polisi walimvamia wakidai hakulala chali mara baada ya kuamriwa kufanya hiyo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Polisi wanadaiwa kumshambulia Lawrence Crosby wakati wakimkamata.

Crosby inaripotiwa alipigwa makonde na mateke zaidi ya 10 wakati akitiwa mbaroni. Kamera ya polisi ilinasa tukio lote.

Maafisa wa polisi waligundua kuwa alikuwa mmiliki halali wa gari hilo lakini wakaendelea kumshikilia wakidaia aligoma kukamatwa.

Msemaji wa polisi wa eneo hilo alitetea matumizi ya nguvu kwenye tukio hilo akidai kuwa walidhani ilikuwa ni kesi ya wizi wa gari.

Dkt Crosby aliachiwa huru na kufutiwa mashtaka yote, hata hivyo alifungua mashtaka dhidi ya jiji na polisi.