Je ni mambo gani yanayomsubiri Felix Tchisekedi anapochukua urais DR Congo?

Felix Tchisekedi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Tshisekedi anaingia uongozini wakati sio kila mtu anamuunga mkono kitaifa na hata kimataifa kutokana na kutiliwa shaka matokeo ya uchaguzi mkuu.

Kwa miaka 18 iliyopita, taifa lenye utajiri wa madini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imeongozwa na mtu mmoja: Joseph Kabila.

Leo anaondoka na kumkabidhi majukumu Felix Tshisekedi, kiongozi wa chama kikongwe cha upinzani nchini anayeapishwa kuwa rais.

Licha ya wasiwasi kwamba kumeshuhudiwa hitilafu katika matokeo ya uchaguzi huo, kuapishwa kwa Tchiskekedi ni ushindi uliosubiriwa kwa muda mrefu na wafuasi wa chama chake.

Ni wakati wa kihistoria kwa upinzani wa nchi hiyo, ambo umekuwa kando kando katika siasa za nchi kwa miongo kadhaa.

Katika hotuba yake hapo jana kwa taifa, rais Kabila amesema hajutii chochote na ametoa wito kwa raia wa Congo wamuunge mkono mrithi wake ambaye ameeleza kwamba anaweza kumfuata wakati wowote kwa ushauri.

Image caption Wapiga ngoma wakitumbuiza umati uliokusanyika katika kuapishwa Tchisekedi DR Congo

Tshisekedi anaingia uongozini wakati sio kila mtu anamuunga mkono kitaifa na hata kimataifa kutokana na kutiliwa shaka matokeo ya uchaguzi mkuu.

Kanisa katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini humo lililotuma waangalizi siku ya upigaji kura, linasema data rasmi hailingani na takwimu walizo nazo.

Muungano wa Afrika (AU) uliitaka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo iahirishe kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu.

Muungano huo unaonuia kuhimiza umoja na demokrasia, ulisema una "shaka kubwa" na matokeo ya awali yaliotangazwa wiki iliyopita.

Mgombea mwenzake Martin Fayulu anayedai kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi huo, amejitangaza kuwa rais wa pekee wa halali.

Sasa ni yapi yanayomsubiri Tchisekedi anapoingia uongozini DRC?

Huwezi kusikiliza tena
Rais Joseph Kabila: Uchaguzi utakuwa huru na wa haki

Majukumu na hata changamoto kubwa zinamsubiri rais mpya Felix Tchisekedi katika nyanja mbalimbali wadadisi wanahoji.

Haya ni baadhi yake:

Maridhiano na mahasimu:

Mchambuzi wa siasa za nchi za maziwa makuu Khalid Hassan, anaeleza la awali na la muhimu kabisa Tchisekedi anahitaji kuleta maridhiano kati ya wadau wa kisiasa nchini Congo.

Hasaa kwa kuzingatia hali na mchakato mzima wa uchaguzi ulivyokwenda na kuhesabiwa kura na hadi kutangazwa mshindi.

Vipi atakavyoweza kulifanikisha hilo? Khalid anaona kwanza ni kwa kujaribu kuonyesha ishara ya kuwepo maridhiano kati yake na wale wanaoonekana kuwa wapinzani wake.

Anaeleza kwamba zaidi ni kwa upande wa mpinzani Martin Fayulu.

Hio ndio hali ya kipekee ambayo anasema huenda ikamsaidia kupata maridhiano na wapinzani wake.

Amani na Usalama

La pili anaeleza ni kuhakikisha raia Congo wana pata ahueni.

Ni zaidi ya miaka 20 sasa hali ya usalama na utengamano haujakuwa wa kuridhisha DRC.

Jambo ambalo hata rais Kabila katika mahojiano na BBC alieleza kwamba katika mambo ambayo angekuwa na muda zaidi kuyashughulikia ni kurudisha amani kwa taifa hilo.

Changamoto kubwa ni kuangalia vipi Tchisekedi anaweza kuleta amani kwa taifa hilo hususan eneo la mashariki ambako kumeshuhudia ghasia na umwagikaji damu mkubwa wa raia, na uwepo wa wanamgambo waliojihami wanaotekeleza mashambulio.

Maelfu ya watu wamelazamika kuyatoroka mapigano na kuyacha makaazi na mali zao. Na hata kwa waliosalia, wanaishi maisha wakihofia usalama yao.

Huwezi kusikiliza tena
Uchaguzi DRC: Ukatili na uhalifu wa asili uliopanda mbegu za vurugu

Uchumi.

Nchi ina utajiri mkubwa lakini raia wa Congo ni masikini kupita kiasi. Hasaa kwa kuzingatia mfumo mzima wa utawala nchini Congo tangu miongo kadhaa. Na pia kwa kutazama na kutathmini ukubwa wa nchi yenyewe na uwezo wa serikali kuweza kukidhi mahitaji ya raia wake.

DRC,kwa ukubwa wake, uchumi wake umegubikwa kwa ukosefu wa miundo mbinu msingi.

Licha ya utajiri mkubwa wa rasilmali, benki ya Dunia inasema takriban 63% ya idadi jumla ya raia nchini humo wanaishi katika umaskini.

DR Congo ina utajiri wa madini kama vile shaba, almasi zinc mafuta, dhahabu, na kadhalika. Lakini licha ya utajiri huu wote, bado maisha ya raia nchini hayajaimarika.

Kuimarisha uhusiano wa kieneo.

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo inapakana na nchi 9. Nchi zote zikabaliwa na changamoto kwa nji amoja au nyingine kiusalama.

Khalid Hassan anaeleza kwamba kando na umuhimu wa kuhakikisha kwamba makundi ya uhalifu yamedhibitiwa lakini pia ina umuhimu mkubwa kwa Tchisekedi kuhakikisha kwamba ana ushirikiano mzuri na wa karibu sana na mataifa majirani zake.

Huwezi kusikiliza tena
UN inavyojaribu kudumisha amani mashariki mwa DRC

'Anastahili kuhakiskiha kwamba hakuna anayemtuhuma mwingine kwamba anahusika kwa kuwapa hifadhi wapiganaji wa chini chini katika upande mwingine' anaongeza Hassan.

Kadhalika ameeleza kuwa ni muhimu kwa taifa hilo kupiga hatua katika nyanja nyinginezo kuhusu kwa mfano, maendeleo na siasa.

DR Congo inahitaji kushirikiana na jirani zake ili mradi inakuwa huru katika maamuzi ya masuala yake, na pia isionekana kama kitisho kwa usalama kwa jirani zake.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii