Bunge la Angola laifuta sheria inayokataza mahusiano ya jinsia moja

Mapenzi ya jinsia moja Haki miliki ya picha Getty Images

Bunge la Angola limeifuta sheria ambayo ilikuwa inatafsiriwa kama inapinga mahusiano ya kimapenzi kwa watu wa jinsia moja.

Serikali ya nchi hiyo tayari imekataza ubaguzi wa watu kulingana na hali zao za mahusiano; yeyote anayemnyima mtu kazi au huduma kutokana na uhusiano wao wa kimapenzi anahatarisha kufungwa jela kwa kipindi cha mpaka miaka miwili.

Angola ni koloni la zamani la tatu la Ureno barani Afrika kufuta sheria zinazokataza mahusiano ya watu wa jinsia moja, Visiwa vya Sao Tome na Cape Verde.

Hata hivyo hakuna mtu yeyote anayefahamika ambaye alishawahi kufungwa ama kukamatwa kama sehemu ya utekelezaji wa sheria hiyo iliyofutwa. Angola inatazamwa kama nchi ambayo watu wake wengi hawana mtazamo hasi na matendo ya mapenzi ya jinsia moja.

Nchi nyingi za Afrika zina sheria kali zinazopingana na mahusiano ya watu wa jinsia moja.

Haki miliki ya picha Clare Spencer
Image caption Angola inatazamwa kama nchi ambayo watu wake wengi hawana mtazamo hasi na matendo ya mapenzi ya jinsia moja

Uganda:

Mapenzi ya watu wa jinsia moja iliharamishwa nchini Uganda chini ya sheria za ukoloni katika kifungu kinachokataza mtu kufanya ngono kinyume na kawaida.

Waziri wa maadili nchini Uganda Simon Lokodo, mwezi uliopita alisema shughuli zote za wapenzi wa jinsia moja ni haramu na kinyume na tamaduni za watu wa Uganda.

Wanaharakati wa kupigania haki za wapenzi ya jinsia moja nchini Uganda wanasema kuwa watu walio wapenzi wa jinsia moja wanastahili kuendelea na shughuli zao ikiwa watahitaji kufanya hivyo.

Serikali hatahivyo kupitia wizara ya maadili nchini humo inasema kuwa haitawafumbia macho wale wanaoshabikia mapenzi ya jinsia moja na kujaribu kusambaza harakati hizo zinazotazamwa kuwa za haramu nchini.

Haki miliki ya picha Getty Images

Kenya:

Mapenzi ya jinsia moja ni kinyume na sheria Kenya na mtu anaweza kuadhibiwa kwa hadi miaka 14 gerezani.

Mnamo 2016, shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu limegundua kwamba wapenzi wengi wa jinsia moja wanaoishi nchini Kenya wanakabiliwa na 'wasiwasi wa usalama kila siku'.

Afrika kusini:

Mwaka 2006 Afrika ya Kusini ilikuwa nchi ya kwanza Afrika na ya tano duniani kuruhusu ndoa za wapenzi wa jinsia moja. Hata hivyo, si wote wanaokabiliana na hatua hiyo, na nje ya miji mikubwa wapenzi wengi wa jinsia moja wanakumbana na mashambulizi na kutengwa na jamii zao.

Jiji la Cape Town ndiyo sehemu pekee nchini humo ambao wapenzi wa jinsia moja wapo salama zaidi na wamekuwa wakifanya tamasha la kila mwaka la kuionesha na kujitangaza uwepo wao.

Haki miliki ya picha MAKONDA INSTAGRAM
Image caption Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda aliidhinisha operesheni maalum kuhakikisha kuwa watu wanaofanya 'biashara chafu za ngono' wanachukuliwa hatua za kisheria

Tanzania:

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, kufanya mapenzi 'kinyume na maumbile' ni kosa la jinai ambalo mtu akikutwa na hatia adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 au maisha jela.

Hatahivyo wadadisi wanaona taifa hilo kwa kiasi fulani limelegeza kamba juu ya mahusiano hayo ya mapenzi ya jinsia moja kufuatia hatua ya serikali kujitenga na kampeni ya kuwakamata na kushtaki wapenzi wa jinsia moja iliyoidhinishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.

Makonda aliidhinisha kamati maalum aliyoieleza kuwa ni ya kuhakikisha kuwa watu wanaofanya biashara chafu za ngono wanachukuliwa hatua za kisheria.

Katika miaka ya hivi karibuni serikali ya Tanzania imevifunga vituo kadhaa visivyo vya kiserikali kwa madai ya kuchochea ushoga kwa kutoa elimu ya mahusiano ya jinsia moja.

Zambia:

Vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, ni haramu nchini Zambia.

Wadadisi wanasema kuwa watu wengi, wanaamini kuwa ni kinyume na imani zao

Vitendo kama ulawiti na uhusiano wa mapenzi kati ya wanawake, vina adhabu ya miaka 15 au kufungwa maisha jela.

Msumbiji:

Msumbiji imehalalisha mapenzi ya jinsia moja, na kuwa moja wapo wa nchi chache Afrika zinazohalalisha mapenzi ya jinsia moja.

Sheria hiyo iliyowekwa na wakoloni wa nchi hiyo Ureno iliondolewa na bunge la nchi. Watetezi wa haki za wapenzi wa jinsia moja, wametaja hatua hiyo kama ushindi mkubwa.

Sheria ya awali ilitupiliwa nje na mahakama ya kikatiba.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii