Mkuu wa zamani wa TBC Tido Mhando aondoshewa mashtaka mahakamani Tanzania

Tido Mhando Haki miliki ya picha TBC

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuondeshea mashtaka aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando baada ya kukutikana hana hatia ya matumizi mabaya ya Madaraka.

Ilidaiwa kwamba aliisababishia serikali hasara ya Tsh milioni 887 kutokana na matumizi mabaya ya madaraka, wakati alipokuwa akilitumikia shirika hilo la Utangazaji la Serikali TBC, pamoja na kulitia hasara ya shilingi 897 milioni za Tanzania.

Mwaka mmoja hii leo mahakama hiyo ya Kisutu imemuachia huru Tido baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.

Hukumu hiyo ya Tido Mhando, ambaye hivi sasa ni Mkurugenzi wa Azam Media imesomwa leo katika mahakama ya Kisutu alikofikishwa.

Mnamo Januari mwaka jana, wakili wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) Leonard Swai alimuambia hakimu Victoria Nongwa wa Mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Mhando anatuhumiwa kwa mashtaka matano.

Alidaiwa kutenda makosa hayo mwaka 2008 alipokuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC.

Mhando ni miongoni mwa waandishi wa habari na watangazaji wakongwe wa Tanzania.

Aliwahi kufanya kazi Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC) kama Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili kabla ya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC.

Pia amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanspoti na The Citizen.

Aliwahi pia kufanyia kazi Sauti ya Ujerumani (Deutsche Welle), Sauti ya Amerika, na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) lilipokuwa linafahamika kama Sauti ya Kenya (VoK).

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii