Kiongozi wa upinzani Venezuela ajitangaza kuwa rais

Mzozo wa kisiasa nchini Venezuela unaelekea kuwa mgogoro wa kimataifa.
Baada ya maandamano ya kumshinikiza rais Nicolas Maduro kung'atuka madarakani kukumbwa na vurugu, kiongozi mashuhuri wa upinzani Juan Guaido amejitangaza kuwa rais wa mpito.
Bw. Guaido tayari amepata uungwaji mkono kutoka mataifa ya Marekani, Canada, na majirani wa taifa hilo waliyo na ushawishi mkubwa katika kanda ya Amerika kusini kama vile Brazil, Colombia na Argentina.
- Raisi wa Burundi afungua mashtaka dhidi ya televisheni
- Angola yahalalisha mahusiano ya jinsia moja
- Mwanamke ang'atwa na nyoka chooni
Muungano wa Ulaya umetoa wito wa kufanywa upya uchaguzi na kuunga mkono bunge la kitaifa litakalo ongozwa na Guaido.
Urusi na China wamuunga mkono Maduro
Lakini kuna baadhi ya mataifa yanayomuunga mkono rais Maduro ikiwemo Urusi na China.
Moscow imeonya kuwa hatua ya Guaido, moja kwa moja huenda ikasababisha "uvunjaji wa sheria na umwagikaji mkubwa wa damu".
Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ilisema: "Tunaonya kuwa hatua hiyo itakuwa na athari mbaya"
Huku hayo yakijiri msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China, Hua Chunying, amesema kuwa China inapinga ''muingilio'' wa nje katika mzozo wa Venezuela.
"China inaunga mkono mikakati ya kulinda uhuru wa Venezuela wa kujitawala" alisema.
"China itaendelea kushikilia msimamo wake wa kutoingilia masuala ya ndani ya matifa mengine'."
Uturuki, Iran, Mexico, Cuba na mataifa mengine pia yana muunga mkono Maduro.
Kwa mujibu wa msemaji wa mamlaka ya urais wa Uturuki Ibrahim Kalin, Rais Recep Tayyip Erdogan amempigia mwenzake Nicolas Maduro na kumhakikishia kuwa Uturuki itasimama nae: ''Ndugu Maduro, Simama imara, tuko nawe kwa hilo.''
Msemaji huyo alitumia hashtag #WeAreMADURO.
Venezuela ilikata uhusiano na Marekani
Lakini hali ya taharuki inayoshuhudiwa katika ulingo wa siasa za kimataifa huenda isibadilike huku maafisa wa Marekani na Venezuela wakitupiana cheche za maneno.
Muda mfupi baada ya Rais Donald Trump kumtambua Guaido kama kiongozi wa muda wa Venezuela, Maduro alisema kuwa amekomesha mara moja uhusiano wa kidiplomasia na wa kisiasa na Marekani.
Alisema "Wafanyikazi wote wakidiplomasia na ubalozi wa Marekani nchini Venezuela" wana saa 72 hours kuondoka nchini humo.
Akijibu tamko hilo waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo, amesema kuwa Marekani haitafanya mashauriano ya uhusiano kidiplomasia kupitia serikali ya Maduro isipokua Guaido.
"Hatuoni kuwa rais wa zamani Nicolas Maduro ana mamlaka yoyote ya kisheria kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Marekani au uwezo wa kuwafurusha maafisa wetu kutoka nchini humo ," ilisema taarifa hiyo.
'Hatua zote za kukomesha mzozo zipo mezani'
Rais Trump aliwahi kutamka hadharani kuwa anaunga mkono "hatua ya kijeshia" nchini Venezuela mwaka 2017 na pia hakuchelea kugusia tena suala hilo katika mahojiano yake na wanahabari katika ikulu ya White House.
"Hatujafanya maamuzi lakini hatua zote za kukomesha mzozo nchini humo zipo mezani," Trump alisema.
Vyombo vya habari nchini Marekani vinaripoti kuwa Trump huenda akaiwekea vikwazo Venezuela, kwa kulenga sekta kuu ya mafuta ambayo ndio chanzo cha mapato ya kigeni kuwajumuisha maafisa wakuu zaidi wa taifa hilo katika orodha ya viongozi waliyowekewa vikwazo.
Hatua hiyo itaathiri uwezo wa Venezuela kulipa madeni ya mabilioni ya madola kutoka Urusi na China.
- Jeshi la Zimbabwe 'liliwatesa waandamanaji'
- Viungo sita vya mwili ambavyo havihitajiki tena na binadamu
Mwezi uliyopita akiwa mjini Moscow, Maduro na mwenzake Vladimir Putin, walikubaliana kusaini mkataba wa Urusi kuingiza ngano nchini Venezuela, na kandarasi ya thamani ya dola bilioni sita katika sekta ya mafuta na uchimbaji madini .
Venezuela pia imekuwa mnunuzi mkuu wa salaha za kijeshi kutoka Urusi.
Muda mfupi baada ya mkutano wa Moscow,Ndege aina ya Tupolev -160 za kuangusha mabomu kutoka Urusi zilitua Venezuela hatua ambayo iliighadhabisha Marekani.
'Juhudi za pamoja'
Makabiliano ya moja kwa moja kati ya Urusi na Marekani kuhusu mzozo wa Venezuela yanaweza kuzuiliwa kupitia jukumu la majirani zake katika mzozo huo.
Mwezi agosti mwaka 2018 rais wa Venezula Nicolás Maduro alisema kuwa amenusurika jaribio la kumuua kwa kutumia ndege isiyokuwa na rubani iliyokuwa na vilipuzi.
Bw Maduro aliilaumu Colombia na vikundi vingine vyenye uhusiano na Marekani kwa njama hiyo ya kutaka kumuua.
Aliongeza kuwa hana shaka kuwa rais wa Colombia Juan Manuel Santos alihusika na jaribio hilo.
Serikali ya Colombia ilikanusha madai hayo.