Ronaldo aing'arisha Juventus, Tottenham hoi

Cristiano Ronaldo Haki miliki ya picha Getty Images

Goli la dakika ya 88 kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Cristiano Ronaldo umeifanya Juventus kujisimika kileleni kwa tofauti ya alama 11.

Mchezo huo ulianza kwa Lazio kuwatangulia Juve katika dakika 59, Juve wakasawazisha kupitia Canselo dakika ya 74 na Ronaldo kupiga msumari wa pili na wa ushindi dakika mbili kabla ya mchezo.

Ronaldo alisajiliwa kwa dau la pauni milioni 99.2 mwaka jana, na tayari ameshaifungia Juventus magoli 17.

Mechi hiyo ilionekana kama Juve wataipoteza, na ingekuwa kipigo cha kwanza msimu huu kwa miamba hiyo.

Timu hiyo inayonolewa na Massimiliano Allegri sasa inaonekana dhahiri kunusa ubingwa wa Serie A kwa mara nane mfululizo baada ya timu inayowafukuzia ya Napoli kutoka sare na AC Milan.

Tottenham yaangukia tena pua

Haki miliki ya picha Getty Images

Tottenham wamejikuta wakitupwa nje ya makombe mawili ndani ya siku nne tu.

Jana wametandikwa goli mbili kwa sifuri na Crystal Palace katika mzunguko wa nne wa michuano ya FA katika uga wa Selhurst Park. Goli hizo zilifungwa ndani ya dakika 35.

Alhamisi iliyopita, Spurs waling'olewa kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Carabao kwa kuchapwa kwa mikwaju ya penati na Chelsea.

Spurs walikosa nafasi ya wazi baada ya Kieran Trippier kukosa mkwaju wa penati muda mfupi kabla ya mapumziko.

Timu hiyo inayonolewa na Mauricio Pochettino sasa wamepoteza mechi tatu katika nne walizocheza hivi karibuni.

Palace wamtwanga kigogo mwengine

Image caption Palace ilipoteza michezo yake mitano iliyopita dhidi ya Spurs

Palace inayonolewa na Roy Hodgson sasa imeshawafunga Manchester City na Tottenham msimu huu na pia imeenda sare na Arsenal na Manchester United.

Kubakia kwenye Ligi ya Premia ndio kipaumbele cha kwanza kwa Palace na Hodgson anaamini kiwango chao cha sasa kitawaongoza kufikia malengo.

Mada zinazohusiana