Bata Trevor : Kisiwa cha Niue kinaomboleza kifo cha bata aliyekuwa peke yake nchini humo

Trevor the Duck Haki miliki ya picha Trevor the duck/Facebook
Image caption Trevor amefariki baada ya kushambuliwa na mbwa

Trevor, ambaye alikuwa akifahamika kama bata mpweke zaidi duniani amefariki baada ya kushambuliwa na mbwa kwenye kisiwa kimoja cha mbali kwenye bahari ya Pasifiki.

Trevor alikuwa maarufu sana kwenye kisiwa kidogo cha Niue kutokana na kuwa ndege pekee wa aina yake kuishi kwenye kisiwa hicho.

Aliwasili kisiwani hapo mwaka 2018, hata hivyo haijulikani ni kwa namna gani alifika kisiwani hapo.

Alikuwa akiishi kwenye dimbwi lililokuwa pembezoni mwa barabara, na alikuwa akihudumiwa na kupewa chakula na wenyeji wa eneo hilo.

"Alionekana hapa Niue mwezi Januari 2018 baada ya kutokea gharika kubwa, tunaamini alipaa ama alipeperushwa mpaka kufika hapa," amesema Rae Findlay, mkuu wa chama cha wafanyabiashara wa Niue ambaye pia alifungua ukurasa wa Facebook wa bata huyo .

"Inaaminika kuwa ametokea New Zealand lakini kuna uwezekano akawa ametokea Tonga ama kisiwa kingine cha bahari ya Pasifiki.

Katika maisha yake mafupi na ya furaha kisiwani Niue, Trevor aliishi kwenye dimbwi.

"Hakuna mito, chemchem ama maziwa hapa, hivyo Trevor alichagua kuishi kwenye dimbwi," Bi Findlay ameiambia BBC.

Japokuwa ametambulika kama bata mpweke, maisha yake hayakuwa ya kipweke kabisa.

Dimbwi la Trevor lilikuwa likikaguliwa mara kwa mara na watu waliokuwa wakimjali. Kikosi cha zimamoto cha kisiwa hicho kilikuwa kikijaza maji dimbwi hilo pale maji yalipokuwa yakikauka.

Haki miliki ya picha Trevor the duck/facebook
Image caption Pale dimbwi la Trevor lilipokuwa likaukiwa na maji...
Haki miliki ya picha Trevor the duck/Facebook
Image caption ...kikosi cha zimamoto kilikuwa kikiiingia kazini kwa kujaza maji

"Alikuwa kawaida yake kupaa katika maeneo jirani na kula vyakula ambavyo alikuwa akipatiwa, mapeasi, mahindi na shayiri," amehadithia Bi Findlay.

Kulikuwa na maoni kutoka baadhi ya watu waliotaka aletwe bata mwingine wa kuishi na Trevor lakini dimbi lake lilikuwa dogo la kumtosha yeye pekee.

Hata hivyo alikuwa na urafiki na jogoo, tembe na weka - ndege wa asili wa kisiwa hicho - ambao wote walikuwa wakiishi karibu na dimbi hilo.

"Baada ya mwaka mzima wa kuwa na mifuko ya shayiri kwenye begi langu, nitakumbuka kila mara nilipokuwa nasimama kumlisha Trevor nilipokuwa nikienda na kutoka kazini. Alikonga nyoyo za watu wengi, na atakumbukwa sana."

Mada zinazohusiana