Mpasuko Venezuela: Marekani yaliwekea vikawzo vya kiuchumi shirika la mafuta la Venezuela

Gas station in Cupira, Venezuela - 16 December Haki miliki ya picha Reuters

Marekani imeliwekea vikwazo shirika la mafuta la serikali ya Venezuela PDVSA na kulitaka jeshi la nchi hiyo kuyaunga mkono mabadiliko ya amani ya uongozi.

Mshauri wa masuala ya ulinzi wa rais Donald Trump John Bolton amedai kuwa rais wa Venezuela Nicolás Maduro na washirika wake "hawataweza tena kuiba rasilimali za raia wa Venezuela".

Harakati za upinzani nchini humo kuung'oa madarakani utawala wa Maduro zimeshika kasi katika kipindi cha siku za hivi karibuni.

Marekani na nchi zaidi ya 20 zinamtambua kiongozi wa upinzani Juan Guaidó kama rais wa mpito wa nchi hiyo.

Waziri wa Fedha wa Marekani Steven Mnuchin amesema mapato yatakayotokana na uuzwaji wa mafuta kutoka nchi hiyo yatazuiwa kwenda kwenye mifuko ya serikali ya Maduro.

Kampuni hiyo inaweza kuondokana na vikwazo pale itakapomtambua Guaidó kama rais halali.

Venezuela inaitegemea pakubwa Marekani katika mauzo yake ya mafuta - huku ikiuza asilimia 41 ya mafuta yake nchi hiyo. while it remains in the top four crude oil suppliers to the US.

Maduro ametengaza kuwa ameiagiza PDVSA kuchukua hatua za "kisiasa na kisheria ndani ya Marekani na mahakama za kimataifa," ili kilinda kampuni yake tanzu ya Citgo iliyopo Marekani.

Wakati huo huo, Guaidó amesema ataliagiza bunge kuteua wakuu wapya wa shirika la PDVSA na Citgo, akilenga kushikilia rasilimali za nchi hiyo.

Haki miliki ya picha EPA

Vikwazo vya Marekani vinalenga mali za PDVSA zilizomo ndani ya Marekani, na kuwazuia raia wa Marekani kufanya biashara na shirika hilo.

Munchin hata hivyo amesema Citgo inaweza kuendelea na shughuli zake ndani ya Marekani iwapo mapato yake yatawekwa kenye akaunti za benki zitakazofungwa ndani yaa ndani ya Marekani.

Bolton pia amelitaka jeshi la Venezuela kumtambua kiongozi wa upinzani kuwa rais wa muda wa nchi hiyo.

Bolton alitangaza vikwazo hivyo kwenye mkutano na wanahabari ambapo ujumbe wa utata ulionekana kwenye kitabu chake.

"wanajeshi 5,000 kwenda Colombia", lakini bado haijajulikana hiyo inamaanisha nini. Colombia inapakana na Venezuela na inamtambua Guaidó kama rais wa Venezuela.

Bolton alikataa kusema kuwa operesheni ya kijeshi inaweza isifanyike nchini Venezuela.

Msemaji wa Ikulu ya White House alijibu alipoulizwa kuhusu suala hilo kuwa: "Kama rais (Trump) alivyosema, njia zote zipo mezani."

Hata hivyo, afisaa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe aliliambia shirika la habari la AFP kuwa "hakuna kitu ambacho kitaunga mkono kupelekwa majeshi nchini Colombia."

Mapema jana televisheni ya taifa ilimuonesha Maduro akiwa Ikulu na wanadiplomasia wa nchi yake aliowarudisha kutoka Washington DC.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maduro akiwakaribisha nyumbani wanadiplomasia aliowarudisha kutoka Marekani.

Venezuela ilivunja uhusiano baina ya nchi hizo na kuwapa wanadiplomasia wa Marekani saa 72 kuondoka nchini humo mara tu Marekani ilipomtambua mpinzani kuwa rais.

Hata hivyo, Jumamosi walitangaza zoezi hilo lingechukua siku 30.

Mgawanyiko wa mataifa

Urusi, China, Mexico na Uturuki wamejitokeza wazi na kusema wanamuunga mkono Maduro.

Katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika Jumamosi Urusi iliituhumu Marekani kuwa inapanga mapinduzi nchini Venezuela.

Zaidi ya nchi 12 za Amerika ikiwamo Canada zimetangaza kumuunga mkono Guiado kama rais.

Nchi kadhaa za Ulaya zikiwemo Uhispania, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza wamesema watamtambua Guaidó kama raisi iwapo uchaguzi hautarudiwa ndani ya siku nane.

Kwa nini watu wanampinga Maduro?

Maduro, ambaye amechukua mamlaka mwaka 2013 baada ya kifo cha Hugo Chavez, amekuwa akishutumiwa vikali ndani na nje ya nchi yake kwa tuhuma za uvunjaji wa haki za binaadamu na kushindwa kusimamia vizuri uchumi.

Kuna upungufu mkubwa wa huduma za kijamii nchini humo ikiwemo dawa na chakula, na takribani watu milioni tatu wanaarifiwa kuihama nchi hiyo.

Mfumuko wa bei wa mwaka ulifikia 1,300,000% kwa miezi 12 kwa mwaka 2018, kwa mujibu wa tafiti ya bunge la nchi hilo.

Hata hivyo wapo wale ambao wanamuunga mkono Maduro na kudai matatizo ya Venezuela yamesababishwa na wapinzani wa mrengo wa kulia wakiungwa mkono na Marekani pamoja na nchi jirani ambazo ni adui.

Wanadai kuwa vikwazo vya Marekani vimeifanya serikali yao kushindwa kulipa madeni ya nchi.


Mada zinazohusiana