Marekani: 'Kwa miaka sasa kampuni za China zimekiuka sheria za biashara ya kimataifa'

Kaimu mwanasheria mkuu wa Marekani Matthew Whitaker, Waziri wa Biashara Wilbur Ross (kushoto), Waziri wa Usalama wa ndani Kirstjen Nielsen na Mkurugenzi wa FBI Christopher Wray Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Marekani imewasilisha kesi 23 dhidi ya kampuni ya mawasiliano ya China, Huawei

Marekani imeishtaki kampuni kubwa ya mawasiliano ya China, Huawei na afisaa mkuu wake wa fedha, Meng Wanzhou.

Mashataka hayo ni pamoja na ubadhirifu wa fedha, kupinga utekelezaji wa haki na wizi wa teknolojia.

Kesi hiyo huenda ikazua mgogoro wa kibiashara kati ya Marekani na China hali ambayo itaathiri biashara ya kampuni hiyo.

Kampuni ya Huawei imekanusha madai hayo.

Katika taarifa, Huawei imesema kuwa "imeghadhabishwa na mashtaka dhidi ya yake".

Imesema kuwa haikufanya makosa yote "yanayodaiwa ilitekeleza" na kwamba"haina ufahamu wa kosa alilotekeleza Bi Meng".

Meng ambaye ni binti wa mwanzilishi wa Huawei, alikamatwa nchini Canada mwezi uliyopita kufuatia ombi la Marekani kwa madai ya kukiuka vikwazo vyake dhidi ya Iran.

"Kwa miaka sasa, kampuni za China zimekiuka sheria zetu za biashara ya kimataifa, hatua ambayo inahujumu vikwazo vyetu na mara nyingine kutumia mfumo wa fedha wa Marakani kuendesha shughuli zao haramu. Hili lazima likomeshwe," alisema waziri wa biashara wa Marekani, Wilbur Ross.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Huawei ni ya pili duniani kwa uundaji wa simu nyingi za aina ya smartphone

Mashtaka ni yapi?

Mashtaka hayo yanadai kuwa Huawei iliipotosha Marekani na benki ya kimataifa na kufanya biashara na Iran kupitia kampuni zake mbili za mawasiliano,Huawei Device USA na Skycom Tech.

Utawala wa rais Donald Trump ulirejesha vikwazo vyote dhidi ya Iran vilivyokuwa vimeondolewa chini ya mkataba wa kimataifa wa Nuklia uliyofikiwa mwaka 2015.

Kesi ya pili inadai kuwa Huawei iliiba teknolojia kutoka kwa T Mobile kufanyia majaribio ya kudumu kwa yake, pamoja na kupinga sheria na ubadhirifu wa fedha kupitia mtandao.

Huawei ni mojawapo ya kampuni kubwa ya mawasiliano na usambazaji wa simu duniani, ambayo hivi karibuni iliishinda Apple na kuwa ya pili kwa uundaji wa simu aina ya smartphone baada ya Samsung.

Lakini Marekani na mataifa mengine ya magharibi yana hofu kuwa serikali ya China huenda ikatumia teknolojia ya kampuni ya Huawei kuimarisha uwezo wake wa kijasusi, japo kampuni hiyo inasisitiza kuwa haina ushirikiano wowote wa kibiashara na serikali.

Hatua ya kukamatwa kwa Bi Meng, binti ya mwanzilishi wa Huawei iliikasirisha China.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Meng Wanzhou ni binti ya mwanzilishi wa kampuni ya Huawei

Aklikamatwa Disemba mosi mwaka jana nchini Canada katika mji wa magharibi wa Vancouver kufuatia ombi la Marekani.

Baadae mahakama ilimuachiliwa kwa dhamana ya dola milioni 76.

Uchambuzi wa Karishma Vaswani, mwandishi wa masuala ya biashara barani Asia

Wachina wanaichukulia Huawei kama bigwa wa kimataifa . Kampuni ya kibinafsi iliyopewa jukumu la kuendeleza ndoto ya China ya kuongoza ulimwengu katika masuala ya teknolojia.

Lakini sasa mkono wa sheria wa Marekani unaikabili kampuni hiyo.

Madai ya idara ya haki ya Marekani dhidi ya Huawei ni makubwa ambayo yakithibitishwa yatazua mgogoro mkubwa wa kibiashara kati ya China na Marekani.

Huawei imekuwa ikikanusha madai hayo, huku mkuu wa kampuni hiyo akisema inatumiwa kuendeleza vita vya kibiashara kati ya Marekani na China.

Japo Marekani inasema kuwa mshataka yake dhidi ya Huawei hayana muingilio wowote wa kibiashara, ni vigumu kwa China kukubaliana na hilo.

Mashtaka hayo yanakuja wakati ambapo Marekani na China zinajiandaa kufanya mazungumzo ya hali juu ya kibiashara mjini Washington wiki hii.

Waziri wa Biashara wa Marekani Wilbur Ross amesema kuwa mashataka dhidi ya Huawei "ni tofauti" na mazungumzo ya kibiashara na China.

Hata hivyo mashataka hayo yanaangazia madai ya wizi wa teknolojia ya Marekani, ambayo ni suala tata katika mashauriano ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii