Usafiri Nairobi: Pendekezo la kutotumia magari lapingwa Kenya

Watu watembea kuelekea kazini
Image caption Watu watembea kuelekea kazini

Baadhi ya wakenya na mashirika ya kijamii yamekosoa agizo la wizara ya uchukuzi la kuzindua siku ambayo hakuna magari yataruhusiwa kuingia katikati ya jiji la Nairobi.

Siku ya Jumanne, waziri wa uchukuzi James Macharia alisema kuwa wakaazi wa Nairobi wanatarajiwa kutotumia magari yao kila siku ya Jumatano na Jumamosi kuanzia tarehe 1 mwezi Februari mwaka huu.

Bw Macharia alisema hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano katika jiji la Nairobi.

Wakenya walilalamikia agizo hilo katika mitandao ya kijamii hususan wa Twitter.

'Haiwezekani'

Wengi wao waliokosoa agizo hilo walisema kuwa hawaoni sababu ya kufungia magari na kuwaacha wachuuzi kuuza bidhaa zao katika barabara za jiji na maeneo ya kuegeshea magari.

Shirika la mawakili pamoja na muungano wa waajiri nchini Kenya, FKE pia wamehoji uhalali wa agizo hilo jipya.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, Mkurugenzi mkuu wa FKE Jacqueline Mugo, alisema ''wadau katika sekta ya usafiri hawakushauriwa kabla ya kutolewa kwa agizo hilo.''

Bi Mugo amesema agizo hilo linakanganya kwa sababu ni vigumu kuweka marufuku ya jumla.

"Ni wazo zuri. Hatahivyo, Nairobi haina mfumo imara wa usafiri wa umma.

Wafanyikazi hawawezi kuendesha baisikeli jijini," alisema Bi. Mugo.

Mwenyekiti wa shirika la mawakili nchini Allen Gichuhi, pia ameunga mkono hoja ya Bi. Mugo na kutoa wito kwa serikali kushauriana zaidi na washika dau wengine kabla ya kuanza kutekeleza hilo ambalo huenda likapingwa mahakamani.

Mpango wa awali wa mamlaka ya jiji la Nairobi kupiga marufuku magari ya usafiri wa umma maarufu kama matatu kuingia eneo la kati kati ya jiji uligonga mwamba.

Serikali iko katika harakati ya kuzindua mabasi ya mwendo kasi katika mfumo wa usafiri unaofahamika kama (Bus Rapid Transport) (BRT) kwa lengo la kupunguza msongamano jijini.

Image caption Magari ya usafiri wa umma

Miji iliyofanikiwa kutekeleza mpango huo

Endapo sheria ya siku ya magari kutoingia jiji itaidhinishwa, Nairobi itajiunga na miji ambayo imefungia magari katikati ya jiji.

Nchini Denmark, nusu ya watu katika jiji la Copenhagen wanatumia baisikeli kila siku kuenda kazini.

Jiji hilo linajivunia kuwa na eno la kilomita 322 ambalo limetengewa waendeshaji baisikeli huku aikiandikisha asilimia ndogo ya watu wanaomiliki magari barani ulaya

Katika kanda ya Afrika Mashariki, Rwanda ilizindua mpango wa kutotumia magari kuingia jiji kuu la Kigali kuanzia mwaka 2016.

Kila Jumapili ya kwanza ya mwezi, wakaazi wa Kigali huacha magari yao nyumbani na kutembea, kuendesha baisikeli au kukimbia hadi kazini.‚Äč

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii