Mauaji ya Watoto: Serikali Tanzania yaapa kuwanasa wauaji, yadai yamechochewa na ushirikina

Waziri Kangi Lugola Haki miliki ya picha IKULU, TANZANIA
Image caption Waziri Kangi Lugola amesema tayari serikali imepata majina ya wote waliohusika katika mauaji ya watoto Njombe.

Serikali ya Tanzania imeahidi kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kuhusika katika mauaji ya watoto mkoani Njombe.

Watoto sita, wakiwemo watatu wa familia moja wenye umri chini ya miaka 10 wamepatikana wakiwa wamefariki katika mazingira ya kutatanisha mkoani humo.

Akizungumza Bungeni leo, Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola amesema tayari wameshabaini baadhi ya wale waliohusika na mauaji hayo na hatua kali zitachukuliwa.

"Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mauaji hayo yametokana na imani za kishirikina...n tayari tumeshawabaini baadhi ya wale ambao wameshiriki. Nawataka watu waache kuichezea serikali. Tutaanza na mkoa wa Njombe," ameonya Lugola.

Lugola hata hivyo hakusema ni watu wangapi mpaka sasa wametiwa mbaroni kutokana na mauaji hayo.

Juzi Jumatatu, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri, aliiambia BBC kuwa mtu mmoja amekamatwa kuhusika na baadhi ya mauaji hayo.

Vurugu Njombe

Siku ya Jumanne, polisi mkoani Njombe walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi walioandamana katika baadhi ya mitaa wakimtaka mtu anayedaiwa kuwa ni mtekaji wa watoto mkoani humo.

UN yalaani mauaji

Umoja wa Mataifa (UN) umetoa tamko kuhusu mauaji hayo ikisema inaungana na serikali ya Tanzania kulaani 'unyama' huo waliofanyiwa watoto.

Tamko lililotolewa na UN leo Jumanne Januari 29, 2019 limekemea mauaji hayo ikieleza kuwa hayakubaliki na kubainisha kuwa watoto wana haki ya msingi ya kulindwa kutokana na vurugu ili waweze kufurahia na kupata mahitaji yao muhimu.

"Umoja wa mataifa unaungana na Serikali ya Tanzania kupinga vitendo hivyo vibaya. Kama UN tupo tayari kusaidia Serikali katika jitihada zao za kukabiliana na tatizo hilo," inaeleza taarifa hiyo ikimnukuu mratibu mkazi wa UN Tanzania, Alvaro Rodriguez.

"Zaidi ya hayo tunatoa wito kwa wadau wote kuungana pamoja kuhakikisha kunakuwa na usalama wa watoto kuanzia katika makazi, shule na maeneo mengine miongoni mwa jamii."

Watoto wanapitia katika aina nyingi za unyanyasaji katika maeneo mengi duniani, "Hili linatakiwa likome," amesema mwakilishi wa Unicef nchini Tanzania, Maniza Zaman.