Uhamiaji: UN unasema watu 6 hufariki kila siku wakivuka bahari ya Mediterranean

Migrants rest on board the Sea Watch 3 off the coast of Siracusa, Italy, January 27, 2019. Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Baadhi ya wahamiaji wakisubiri kutoka pwani ya Sicily Jumapili

Takriban wahamiaji sita walifariki wakivuka bahari ya Meditarenia kila siku mwaka jana, ripoti ya Umoja wa mataifa inasema.

Italia iliangazia idadi ya chini ya vifo kwa jumla mwaka jana, kutokana na idadi ndogo ya watu waliovuka bahari hiyo.

Lakini idadi ya watu waliofariki kutoka Libya iliongezeka na kuwa mtu mmoja kati ya 14 waliowasili mwaka 2018, kutoka mtu mmoja kati ya 38 waliofariki mwaka uliotangulia.

Ripoti hiyo imejiri wakati nchi 7 za Ulaya zilikubaliana kumaliza mzozo kuhusu wahamiaji 47 waliookolewa, na ambao wamekwama katika boti la misaada kwa siku 12.

Shirika la misada kutoka nchini Ujerumani, Sea Watch, Liliipeleka Italia katika mahakama ya Ulaya ya haki za binaadamu baada ya kuwaokoa wahamiaji hao kutoka bahari ya Meditarenia karibu na Libya mnamo Januari 19.

Serikali ya Italia, ambayo imechukua msimamo mkali kuhusu maboti ya wahamiaji, ilikataa kuruhusu boti hilo la Sea-Watch 3 kutia nanga, kwa hivyo limesalia kutoka pwani ya Sicily.

Waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte leo Jumatano amesema wahamiaji hao 47 wataruhusiwa kushuka baada ya 'orodha ya mataifa ya urafiki', ikiwemo Italia, kukubali kuwapokea.

Ni kwanini idadi ya vifo imeongezeka?

Waziri wa mambo ya ndani Italia Matteo Salvini amelizungumzia suala la serikali kupinga uhamiaji ambayo ilikuwa ajenda kuu katika kampeni ya kuchaguliwa kwake.

Katika barua iliyochapishwa katika gazeti la Italia, Corriere Della Sera, siku ya Jumanne, aliandika: " Mnamo 2018 kulikuwa na idadi ndogo ya vifo, Wahamiaji 23,370 waliruhusiwa kushuka kwenye boti, ikilinganishwa na 119,369 mwaka uliotangualia. Mkondo huo ulithibitishwa pia wiki za kwanza mwaka 2019."

Lakini ripoti ya sasa kutoka shirika la Umoja wa mataifa linalowashughulikia wakimbizi (UNHCR) imeangazia viwango vilivyoongezeka vya vifo miongoni mwa waliosafiri, kama chanzo, na vinavyoangazia matatizo yanayoyakabili mashirika ya kibinaadamu ya uokozi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Januari 9, Kundi jingine la wahamaiji wakisherehekea habari kwamba wataruhusiwa kushuka katika boti

"Huenda kupungua kwa uwezo wa kutafuta na kuokoa ikijumlishwa na muitikio ambao haukuratibiwa na haukutarajiwa katika kuwaruhusu wahamiaji kushuka kutoka kwenye maboti, kumechangia ongezeko la vifo,"ripoti hiyo imesema.

Takriban watu 2,275 walifariki walipokuwa kwenye safari mnamo 2018 - kwa wastani watu 6 kila siku.

Idadi ya vifo iliongezeka hususan katika njia kuelekea Uhispania, ambako ilikuwa mara nne zaidi ya idadi iliyokuwepo 2017.

Wahamiaji wanakabiliwa na nini Libya?

Ripoti hiyo inasema Italia kukataa kupokea wahamiaji waliookolewa kutoka pwani ya Libya, iliangalia na na kupungua kwa jitihada za uokozi na kuwasaka kutoka Meli za Ulaya - na badala yake, kumeongezeka 'kuzuiwa kwa meli' na kikosi cha maji nchini Libya.

Lakini ripoti hiyo, imeeleza kwamba waliishia kuwekwa katika vizuizi, ambako walikaa katika hali 'mbaya'.

"Waliozuiwa wengine walipewa chakula kichache, na kuna ripoti za mlipuko wa kifua kikuu," ilisema.

Kwa waliookolewa na meli za Ulaya, ilishutumu ukosefu wa muitikio ambao haukuratibiwa katika kushughulikia hatma zao.

Imependekeza kwamba jitihada za kuwasaka na kuwaokoa zishinikizwe - lakini pia imehimiza "umoja" kwa mataifa ya Ulaya kuruhusu kuhamishwa kwa wanaotafuta hifadhi kwenda katika mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya, kupunguza mzigo kwa wale wanaoshughulikia idadi kubwa za maombi ya hifadhi.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii