Mgunduzi wa madini ya Tanzanite, Mzee Jumanne Mhero Ngoma amefariki dunia

Jumanne Ngoma mvumbuzi wa madini ya Tanzanite akisisitiza jambo huku mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzanite Founder Foundation Asha Mhero akimsikiliza kwa makini
Image caption Jumanne Ngoma mvumbuzi wa madini ya Tanzanite na mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzanite Founder Foundation Asha Mhero akimsikiliza kwa makini

Mgunduzi wa madini ya Tanzanite, Mzee Jumanne Mhero Ngoma amefariki dunia.

Mgunduzi huyo wa kwanza wa madini ya Tanzanite, aliyagundua madini ya Tanzanite mnamo mwaka 1967.

Inaarifiwa kwamba, Mzee Jumanne alifariki mchana wa leo Jumatano katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili mjini Dar es Salaam.

Mnamo mwaka jana 2018, Jumannne Ngoma alitambuliwa na Rais Magufuli na kumzawadia shujaa huyo milioni 100 kwa ajili ya kumsaidia kujikimu na matibabu baada ya mzee huyo kupooza sehemu ya mwili.

Madini hayo ambayo ni ya kipekee kwa Tanzania, hayapatikani sehemu yeyote duniani.

Haki miliki ya picha AFP

Mauzo ya Tanzanite duniani yanafikia takribani dola za Marekani milioni 50.

Tanzanite ni jiwe lenye miaka milioni mia 6 na liligundulika Mererani, Arusha, kaskazini mwa Tanzania, mwaka 1967.

Inasemekana kuwa na upekee hata zaidi ya almasi.

Mwaka jana, kwa mara ya kwanza Tanzania iliadhimisha miaka 51 tangu kuvumbuliwa kwa madini hayo ya Tanzanite.

Taasisi ya Tanzanite Founder Foundation , iliadhimisha siku hiyo kwa kutoa taarifa na kuudhihirishia ulimwengu kuwa, madini ya Tanzanite ni fahari na urithi wetu Watanzania.

Tanzania ilipoteza takriban shilingi za kitanzania trilioni 188 (dola bilioni 84 za Marekani ) katika kipindi cha miaka 19 kati ya mwaka 1998 na mwaka 2017 kupitia usafirishaji wamakinikia ya dhahabu na shaba.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya tume maalum iliyoundwa kuchunguza madini nchini Tanzania, baada ya uchunguzi kuhusu mchanga wa madini uliokutikana katika makontena zaidi ya 200 katika bandari ya Dar es salaam.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii