Mchezo wa Kamari: Je vijana Uganda wana uraibu?

Betting by mobile phone in Uganda Haki miliki ya picha Getty Images

Michezo ya kamari inaongezeka Afrika mashariki - kwa simu, kwa kompyuta na katika maduka ya kamari. Ni biashara kubwa na inaleta mapato ya kodi yanayohitajika pakubwa kwa serikali.

Lakini kuna wasiwasi unaoongezeka Uganda kuhusu athari yake kwa jamii.

Serikali imetangaza udhibiti mpya katika biashara hiyo, ulionuiwa kuzuia shughuli za kampuni za kamari za mataifa ya nje.

"Vijana Uganda wamekwama katika mzunguko wa michezo ya kamari, wanatoa mishahara kidogo wakitarajia watashinda mali nyingi," amesema waziri mdogo wa fedha David Bahati, akizungumza katika hafla aliyoihudhuria kwa niaba aya rais Yoweri Museveni.

"Kuanzia sasa, hakuna kampuni mpya itakayopewa kibali. Kampuni zilizosajiliwa hazitopewa vibali vipya wakati walivyonavyo vikimalizika muda."

Kwa hivyo, je ni kweli kuwa vijana ndio wanaocheza kamari zaidi na je kuna tataizo linalokuwa kubwa kutokana na uchezaji kamari?

Kukuwa kwa michezo ya kamari Afrika mashariki

Katika miaka kadhaa iliyopita, kampuni mpya za uchezaji kamari zimeibuka katika eneo la Afrika mashariki.

Michezo mingi ya kamari huwa kwenye simu, huku michezo kama soka ya ligi kuu ya England yakiwa na umaarufu mkubwa.

Image caption Wengi wanatumia simu kuweka dau

Serikali imeyahimiza makampuni haya yanayoingiza kipato cha kodi na inayooekeza katika ligi za soka.

Lakini rais Museveni, ambaye awali aliyahimiza, makampuni hayo yalioshamiri, sasa anaonekana kubadili kauli yake na kuelezea kwanini ana wasiwasi nayo.

Zaidi ana wasiwasi kuhusu makampuni kukusanya faida nje, badala ya kuekeza upya nchini Uganda.

"Wanachofanya ni kukusanya pesa tu kutoka kwa raia wa Uganda, alafu wanazitoa nje ya nchi," amesema.

Alipoulizwa bungeni kuhusu uwepo wa makampuni hayo ya nchi za nje ya kamari, Bahati amesema: "Kwa kutazama nafasi ndogo iliopo, ni makampuni ya Uganda pekee yatakayoruhusiwa."

Je ni kweli vijana ndio wanaocheza kamari zaidi?

Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa katika mji mkuu wa Uganda, Kampala, umegundua kwamba wengi walioshiriki kamari walifanya hivyo kupata kipato, kujikimu maisha na sio kwasababau za starehe.

Utafiti huo wa taasisi ya Economic Policy Research Centre, imeashiria kwamba 45% ya wanaume Uganda walio na umri wa kati ya miaka 18-30 walijihusisha zaidi na aina fulani ya kamari, ikilinganishwa na takriban robo ya watu wazima wote.

Utafiti huu, umegundua kwamba "wanaocheza kamari kukabiliana na umaskini wana uwezekano mkubwa wa kuwa waraibu kuliko wale wanaocheza kwa starehe".

Kwa mujibu wa EPRC, ni mchezo unaowavutia zaidi wanaume, huku chini ya 4% ya wanawake walioitikia katika utafiti huu wakisema wamewahi kucheza kamari.

Ripoti hiyo pia imekadiria kwamba wanaocheza kamari, wanatumia takriban 12% ya mishahara yao kila mwezi katika michezo ya kamari.

"Hamu ya kutaka akupata pesa haraka kutoka kamari inawashinikiza vijana kujiingiza katika kamari kiasi kwamba baadhi wanatazama mchezo huo kama njia ya kujikimu kimaisha badala ya kutafuta ajira," watafiti wamesema.

Pato la kodi laongezeka

Kuongezeka kwa haraka kwa pato la kodi katika miaka michache iliyopita kutoka sekta ya kamari ni kipimo cha wazi kwamba uchezaji kamari umeongezeka miongoni mwa raia Uganda.

katika miaka minne iliyopita (ikiwemo 2017-18), data ya serikali inaashiria ongezeko la zaidi ya mara nne katika pato la kodi.

Iwapo serikali ya Uganda itaendeleza mipango yake kukatiza uchezaji kamari, ni wazi kwamba hatua hiyo itaathiri pato la nchi.

Haki miliki ya picha Getty Images

Baadhi wameelezea kushtushwa kwao kwamba serikali imechukua hatua hii, hasaa kwa kutazama faida inayopokea sasa kutokana na biashara ya kamari.

Je wasiwasi ni upi wa kijamii?

Shutuma zilizoelekezwa kwa biashara hiyo zinazidi kuongezeka, huku kukiwa na lawama kwamba inaathiri maisha ya vijana sio tu Uganda lakini katika eneo zima.

Haki miliki ya picha Getty Images

Afisa katika duka la michezo ya kamari mjini Kampala, Patrick Lubaale, anadokeza kwamba maelfu ya watu wanategemea ajira katika biashara hiyo.

Na anasema kampuni za michezo ya kamari zimekuwa zikihimiza watu wacheze kwa uwajibikaji.

"Iwapo rais analalamika kuhusu athari mbaya kwa vijana," anasema Lubaale, "tayari tumekuwa tukihamasisha watu kuhusu athari za kutowajibika katika mchezo huu, na watu wanalifahamu hilo - lakini hilo halipaswi kuwa sababu ya kupiga marufuku biashara hiyo."

Lakini suala la uraibu wa mchezo wa kamari miongoni mwa watu walio na kipato kidogo linazidi kuulizwa Uganda.

Waziri wa fedha, Matia Kasaija ametaka liwe kwa kipimo.

"Hautoingia katika matatizo. Utaishiwa na pesa, hautokuwa na chakula, mahali pa kulala, na kitakachofuata sasa ni uhalifu wa kuibia watu."

Hatahivyo, licha ya ahadi ya serikali kutotoa vibali vipya hakujakuwa na ishara ya wazi ambayo makampuni ya kamari Uganda yatafahamu, ni vipi na lini yatakaathirika.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii