Tundu Lissu aendelea 'kuminyana' na vigogo wa Tanzania akiwa nje ya nchi

Tundu Lissu

Mbunge wa Singida Mashariki aliyepo kwenye matibabu ughaibuni, Tundu Lissu, ameendelea kuzua gumzo nchini Tanzania juu ya madai yake dhidi ya serikali ya nchi hiyo.

Lissu alishambuliwa na watu wenye silaha za moto mwezi Septemba 2017 ambapo alimiminiwa zaidi ya risasi 30 kwenye gari lake huku 16 zikimpata mwilini.

Toka wakati huo, Lissu na viongozi wengine wa upinzani wamekuwa wakilihusisha shambulio hilo na kazi yake ya siasa.

Wakati wa shambulio, Lissu hakuwa tu mnadhimu wa kambi rasmi bungeni Tanzania bali pia raisi wa chama cha wanasheria nchini humo. Kwa kutumia kofia zake zote mbili, mwanasiasa huyo machachari alikuwa mwiba mkali wa ukusoaji wa serikali ya Magufuli.

Lissu alikuwa miongoni mwa wanansiasa wa upinzani waliopendelea kumuita Magufuli kuwa 'Dikteta Uchwara' ama kwa lugha ya kingereza'Petty Dictator'.

Baada ya shambulio hilo, alikimbizwa Nairobi kwa matibabu kisha Brussels Ubelgiji toka mwezi Januari mwaka 2018. Huko kote aliendelea kusisitiza kuwa serikali ya Magufuli ilikuwa na mkono kwenye shambulio dhidi yake.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Lissu amekuwa nje ya Tanzania kwa matibabu toka Septemba 2017, amsema tarejea nyumbani atakaporuhusiwa na madaktari wake.

Lissu pia amekuwa akilituhumu bunge chini ya Spika Job Ndugai kwa 'kumtelekeza' na kushindwa kulipia matibabu yake nje ya nchi.

Hivi karibuni, Lissu ametoka nje ya Ubelgiji na kufanya mahojiano katika vituo vya televisheni vya kimataifa akianzia BBC katika kipindi maarufu cha Hard Talk na baadae Ujerumani katika telavisheni ya DW.

Huko kote, mwanasiasa huyo hakumung'unya maneno juu ya mashambulizi yake kwa serikali ya Magufuli. Akisema mpaka sasa hakuna uchunguzi unaondelea wa kesi yake na hakuna hata mtuhumiwa mmoja aliyetiwa nguvuni na polisi.

Gharama za matibabu

Haki miliki ya picha Bunge, Tanzania
Image caption Spika Ndugai amekanusha madai za Lissu kuwa hajalipwa na Bunge

Alhamisi ya wiki iliyopita, Spika Ndugai aliliambia bunge kuwa si kweli kuwa chombo hicho kimtelekeza Lissu.

Ndugai alidai dai kuwa hadi mwishoni mwa Desemba 2018, Lissu alikuwa amelipwa Sh207.8 milioni pamoja na Sh43 milioni zilizotolewa kama mchango wa matibabu yake na wabunge wenziwe na kufanya jumla kuu ya fedha alizolipwa kuw Sh250milioni.

Hata hivyo, Lissu alimjibu Ndugai na kunukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema bunge la Tanzania halijawahi kutoa hata senti moja kugharamia matibabu yake.

Lissu amekiri kulipwa Sh43 milioni zilizotolewa na wabunge wenzake kama mchango wao na kwamba kiasi kingine alicholipwa kinachofanya jumla ya fedha hizo kufikia Sh250 ni mishahara na stahiki zake, lakini siyo gharama za matibabu.

Uchunguzi wa polisi

Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk Abdallah Possi ameaingia kwenye majibizano na Lissu baada ya mbunge huyo kutoa matamko yake nchini humo, kwa kumtaka Lissu kurejea Tanzania kutoa ushirikiano na polisi.

Dk Possi alisema Serikali inafuatilia suala hilo ndiyo maana Rais John Magufuli alishatoa tamko kulaani tukio hilo na kutuma baadhi ya viongozi kumjulia hali jijini Nairobi na hata ughaibuni alipo kwa sasa.

"Rais alitoa taarifa ya kulaani tukio hilo na kuagiza uchunguzi wa kina wa haraka. Kwa nyakati tofauti Rais amemtuma makamu wake, Rais mstaafu na viongozi wengine wa Serikali kumtembelea Lissu akiwa hospitali akiwa Dodoma, Nairobi na Brussels," alisema Dk Possi katika tamko lake.

Aliongeza kuwa uchunguzi ulishaanza mara tu baada ya kutokea tukio hilo lakini umeshindwa kuendelea kwa sababu ya kutopata ushirikiano kutoka kwa mbunge huyo.

Lissu ameimbia BBC na DW kuwa atarejea Tanzania pale tu madaktari wake watakapomruhusu na kudai serikali ya Magufuli itawajibika kumhakikishia ulinzi wake.

Akimjibu balozi Possi Lissu amesisitiza kuwa hakuna uchunguzi uliofanyika wa kushambuliwa kwake.

Kuhusu kutoa ushirikiano kwa polisi amesema sheria za Tanzania zinaruhusu kuomba msaada wa kupatikana kwa ushahidi iwapo mtuhumia yupo nje ya nchi, na kudai serikali ya Tanzania haijawahi kuwasiliana na serikali ya Kenya na ya Ubelgiji ili kupatiwa msaada wa kuhojiwa yeye na dereva wake.

Mada zinazohusiana