Komla Dumor Award 2019: Kumtafuta nyota chipukizi wa uandishi habari Afrika

Huwezi kusikiliza tena
BBC inazindua tuzo ya Komla Dumor 2019

BBC inamtafuta nyota chipukizi wa uandishi habari Afrika kwa tuzo ya BBC World News Komla Dumor Award, sasa katika mwaka wa tano.

Waandishi habari kutoka maeneo tofuati barani Afrika wanakaribishwa kuwasilisha ombi katika tuzo hiyo, inayonuia kufichua na kuendeleza vipaji vipya kutoka Afrika.

Mshindi atahudumu kwa miezi mitatu katika makao makuu ya BBC mjini London ambako atapata mafunzo na uzoefu wa kazi.

Mwisho wa kuwasilisha maombi in Februari 26 2019, saa 23:59 GMT.

Tuzo hiyo iliidhinishwa kumuenzi Komla Dumor, mwandishi habari wa aina yake raia wa Ghana na mtangazaji wa BBC World News, aliyefariki ghafla akiwa na umri wa miaka 41 mnamo 2014.

Tuzo ya mwaka huu inazinduliwa kutoka mji mkuu wa Nigeria, Lagos.

Itapewa kwa mtu mwenye sifa za aina yake, anayeishi na kufanya kazi Afrika, aliye na mchanganyiko wa ujuzi mzito wa uandishi habari, haiba akiwa hewani na talanta ya kipekee katika kuelezea taarifa za Afrika aliye na azma na uwezo wa kuwa nyota wa siku zijazo.

Kando na kupata fursa ya kwenda BBC mjini London, mshindi pia atapata fursa ya kusafiri barani Afrika kutoa taarifa - ambayo itasambazwa kote barani na duniani.

Washindi wa awali:

Mwandishi habari kutoka Kenya, Waihiga Mwaura alishinda tuzo ya mwaka jana na aliripoti kutoka Togo kwa mradi wake kuhusu vijana wavumbuzi wanaogeuza taka za elektroniki kuwa roboti.

Waihiga amesema pia kwamba ungeweza kuhisi saa zote "ari kubwa katika namna ambavyo Komla alielezea taarifa za Afrika".

Image caption Mwaura ni mwandishi mashuhuri nchini Kenya

"Azimio lake kutaka kubadili mtazamo kwa Afrika ni mojawpao ya sababu iliyomfanya akawa tofauti na watangazaji wengine wa kimataifa," mshindi wa tuzo hiyo 2018 alisema.

"Nahisi nafasi hii ya kuwa BBC - kufanya kazi na marafaiki na wafanyakazi wenzake Komla - imenisaidia kuendeleza kazi nzuri ya Komla, na natazamia siku ambapo waandishi zaidi wa Afrika wa hadhi ya Komla, wataweza kueleza taarifa za kipekee za Afrika kutoka vyombo tofuati vya habari duniani."

Waihiga atashiriki katika uzinduzi wa tuzo ya mwaka 2019, ambapo ataendesha mdahalo wa BBC World Service kuhusu uwezo wa vijana wa Nigeria katika uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumzia katika kuwadia kwa uzinduzi huo, mkurugenzi mkuu wa BBC World Service Jamie Angus amesema:

"Katika karne ambapo uandishi unaoangazia pande zote na wenye uhakika una uzito mkubwa, ni muhimu tuwatafute waandishi wanaofahamu, wanaoelewa na wanaoweza kutathmini taarifa za Afrika kwa wasikilizaji na watazamaji wa kimataifa ili tuweze kutoa picha kamili ya kinachoendelea katika bara.

"Washindi wote wa awali wamedhihirisha kuwa wana uwezo mkubwa, na wameleta mtazamo wa ndani kuhusu namna ya kuendeleza mawasiliano na watazamaji na wasikilizaji nyumbani.

"Tunafuraha sana kuweza kuendeleza sifa ya Komla na tunatazamia kumpata mwandishi mwingine wa aina yake kutoka barani."

  • Kujua iwapo unafuzu kushiriki kwa nafasi hii na kuwasilisha ombi, Bonyeza hapa
  • Unaweza pia kuisambaza taarifa katika mitandao ya kijamii kwa kutumia #BBCKomlaAward.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii