Ernest Bwire: Afungwa maisha kwa mauaji Kenya, lakini hajakata tamaa

Bwire
Image caption Ernest Bwire kwa sasa ana miaka 56, kati ya hiyo 29 ameiishi akiwa gerezani.

Ernest Bwire aliwasili Kenya kutoka kwao Uganda akiwa na matumaini makubwa ya kujiendeleza kikazi, lakini yote hayo ni ndoto sasa.

Kwa miaka 29 sasa Bwire amekuwa akitumikia kifungo jela.

Kwa sasa yupo gereza la Kamiti liliopo kilomita 16 kutoka katikati mwa jiji la Nairobi ambako anatumikia kifungo cha maisha kwa mauaji.

Kufikia sasa Bwire ndiye aliyetumikia kifungo cha miaka mingi zaidi nchini Kenya.

Hata hivyo anasema hana hatia kwani hakuhusika na mauaji.

``Huyo kijana aliyenyongwa Nairobi nilikua rafiki mkubwa wa familia yao, na nisingeweza kufanya tendo hilo, lakini nimeikubali hali yangu ya sasa. Kwanza nilihukumiwa kunyongwa kisha baadae wakanihurumia nikafungwa maisha,'' Bwire anasema alipozungumza na John Nene wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC huko Kamiti.

Maisha ya Jela

Alianza kifungo chake katika jela kuu ya Naivasha, kilomita 100 kutoka Niarobi.

``Nilipokua huko nilifanya kazi yangu ya ualimu nikifunza wafungwa wenzangu somo la Kiingereza,Kifaransa na Jiografia. Nilikua pia mwenyekiti wa shule ya wafungwa huko,'' anasema Bwire.

Baada ya mwaka mmoja katika jela ya Naivasha, Bwire alihamishwa hadi jela kuu ya Kamiti. Aliendelea na kazi yake ya ualimu katika shule ya msingi na ya upili ya Kamiti.

Hatimaye alipandishwa cheo akawa naibu wa msimamizi wa shule hiyo. Kutokana na bidii na kazi yake nzuri, Bwire sasa ni msimamizi mkuu wa shule hiyo.

``Nina furaha sana kushikilia cheo hiki cha mkuu wa shule. Ni kazi ninayoipenda sana,'' anasema Bwire akiwa mchangamfu na haonyeshi uchungu wowote wa kuwa gerezani. Kiafya yuko sawa, na ni mtu maridadi kwa usafi.

Kwa mavazi, Bwire hana sare za kawaida zenye mistari zinazovaliwa na wafungwa wote. Anavalia sare ya rangi ya samawati (buluu) ya wafungwa waliopandishwa cheo kusimamia wenzao kutokana na nidhamu yao na utiifu gerezani.

`Mimi na wenzangu wengine 15 ni Trustees (wafungwa wanaoaminika). Tunaishi vizuri. Tuko na sehemu yetu ya kulala.Tuna magodoro mazuri, choo kisafi na tunaoga na maji moto pia, sio baridi tu.''

Image caption Bwire amekuwa ndani ya gereza la Kamiti kwa miaka 28 iliyopita.

Je, siku yake huanza vipi? Bwire anasema kwa kawaida huwa anaamuka saa kumi na moja za asubuhi kila siku ama mapema zaidi.

``Nikishaamka kwanza nachukua kama saa moja hivi kuomba. Tangu niingie hapa nimeokoka pamoja na wenzangu wengi hapa. Ninajiombea mwenyewe, wafungwa wenzangu, naombea Kenya na Rais Uhuru Kenyatta Mungu ampe hekima kuongoza taifa hili kwa njia nzuri. Sote hapa ndani tunampenda Uhuru kwa roho yake safi na uongozi bora.''

Akishamaliza maombi anapata kifungua kinywa. Zaidi Bwire hunywa uji na siku moja moja akiwa na pesa ananua mkate.

Kutoka hapo anaanza kazi yake ya usimamizi wa shule, akisema huwa hana muda wa kupumzika hadi wakati wa chakula cha mchana.

``Mbali na kazi za ofisi ninafunza Kiingereza na Jiografia kidato cha nne na cha kwanza. Napenda kufundisha sana, na wanafunzi wangu wananipenda ninavyowafunza,'' anasema Bwire.

``Kutokana na mafunzo yangu mazuri, baadhi ya wanafunzi hunitembelea siku ya wageni. Hii siku huwa nzuri sana kwa sababu wanakuja na vyakula tunakula pamoja na ninasahau kwa muda kifungo changu cha maisha.''

Bwire anapongeza wakuu wa jela ya Kamiti na maaskari wanaowasimamia humo ndani kwa kuwatunza vizuri na kuzungumza nao kama binadamu.

``Siku hizi jela sio kama zamani. Kulikuwa na madai mengi ya wafungwa kuteswa. Tangu Makamu wa Rais wa zamani wa Kenya Moody Awori aanzishe usimamizi bora gerezani mambo yamebadilika. Hamna ukatili tena. Tunakula vizuri na kutazama runinga pia.''

Kuhusu miaka hiyo 29 aliyotumikia gerezani, Bwire anasema:`` Kama si imani yangu na uvumilivu ningekua siko lakini kwa vile nimeokoka na ninamuamini Mungu sana nimeweza kuishi vizuri lakini jela kama mjuavyo sio mahala pa furaha manaake huna uhuru wako ukiwa ndani.

Mbali na ualimu Bwire amesomea ushonaji, na ana vyeti vya masomo ya Bibilia, kompyuta na masuala ya maisha kwa jumla.

``La mhimu zaidi nililojifunza hapa ndani ni kuwa mvumilivu. Naomba nyote ambao mko nje muwe na uvimilivu kwa biashara zenu, ndoa na maisha kwa jumla. Nina imani kuna siku itafika nifunguliwe milango hapa niwe huru kama raia wengine.''

Familia

Bwire ana umri wa miaka 56 sasa na hana mke wala mtoto.

``Nilifungwa nikiwa na miaka 25. Wakati huo nilikua sijaoa wala sikuwa na mtoto wa nje. Kwa sasa sifikirii mambo ya kuoa ama kuwa na watoto kwa sababu ninamtumikia Mungu gerezani. Endapo Mungu atanipa uwezo wa kuoa nikitoka nisawa tu maanake nguvu niunazo na kutokana na yote niliyojifunza hapa ndani nitakua mume mzuri sana kwa mke wangu.

``Ninachokosa zaidi gerezani ni kuonana na watu wangu, ndugu na dada zangu na watu wa ukoo. Wazazi wangu walifariki. Wakipata nafasi watu wangu kutoka eneo la Tororo nchini Uganda huja kunitembelea. Hiyo huwa ni siku kubwa sana kwangu yenye furaha tele.''

Kuna baadhi ya wasomaji mtajiuliza je wafungwa wa kifungo cha maisha waliokua gerezani Kamiti kuanzia miaka ya sitini hadi tisini wako wapi? Maanake ni dhahiri hao ndio wangekua gerezani kwa miaka mingi zaidi kuliko Bwire.

Kulingana na mkuu wa jela kuu ya Kamiti George Dianga, wafungwa hao waliachiliwa huru baada ya kukata rufaa ama wakafaidika na msamaha wa Rais wa Kenya ambaye huwa ana uwezo wa kuwaachilia huru baadhi ya wafungwa walioonyesha nidhamu ya hali ya juu na utiifu wakiwa gerezani.

Bwire naye ameshakata rufaa anasubiri kama atakua na bahati ya kuachiliwa huru ama afaidike na msamaha wa Rais wa Kenya ambaye kwa sasa ni Uhuru Kenyatta.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii