Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa amaliza muda wake wa usuluhishi wa mgogoro Burundi

Benjamin Mkapa Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa 'amemaliza' muda wake wa usuluhishi wa amani ya Burundi

Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa amemaliza kipindi chake cha usuluhishi wa mgogoro wa kisiasa nchini Burundi na wala hajajiuzulu, ofisi yake imesema.

Awali taarifa zilizagaa kuwa Mkapa amejiuzulu majukumu hayo kwa kupewa ushirikiano finyu kutoka kwa uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao ndio ulimpa Mkapa jukumu la usuluhishi.

Mzozo wa kisiasa nchini Burundi ulianza mwaka 2015 baada ya rais President Pierre Nkurunziza kugombea na kushinda urais kwa awamu ya tatu.

"Muda wake wa usulihishi umefikia tamati, hajajiuzulu," msemaji wa Mkapa, Makocha Tembele ameiambia BBC Idhaa ya Kirundi.

Tembele ameiambia BBC kuwa rais Mkapa amewasilisha ripoti yake ya mwisho juu ya usuluhishi wa mgogoro huo kwenye mkutano wa Viongozi wa Nchi wananchama wa EAC mapema mwezi huu jijini Arusha.

Kwa mujibu wa msemaji huo sasa kazi inabaki kwa rais wa Uganda Yoweri Museveni kuendelea na sehemu inayofuata ya usuluhishi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Mgogoro wa Burundi umepelekea kumwagika kwa damu baada ya vikosi vya serikali kukabiliana kwa silaha za moto na waandamanaji wa upinzani.

Baadhi ya wanausalama pia wamekuwa wakijihusisha na upinzani na jaribio la mapinduzi nchini humo lilifanyika na kufeli.

Takribani watu 1,000 waliuawa baada ya jaribio hilo la mapinduzi nchini humo na maelfu wengine kukimbilia nchini jirani kama wakimbizi.

Mustakabali wa suluhu

Mazungumzo hayo yaliyokuwa yakiongozwa na Mkapa kwa wachambuzi wengi yanaonekana kutofikia matarjio yaliyokuwapo awali.

Bado serikali na makundi ya wapinzani nchini Burundi wapo katika hali ya uhasama.

Serikali ya Burundi mara kadhaa pia imekuwa ikiacha kupeleka wawakilishi wake kwenye vikao vya mazungumzo ya suluhu.

Image caption Mzozo ulianza baada ya rais Nkurunziza kugombea awamu ya tatu ya uongozi.

Jitihada hizo za kuwapatanisha mahasimu wa kisiasa Burundi zimekuwa zikiendeshwa na EAC lakini suala hilo nalo linaweza likwa na ugumu kwa siku za usoni.

Burundi imekuwa ikiishutumu Rwanda kuwa nchi adui inayowawezesha wapinzani wake kwa hali na mali.

Rwanda chini ya rais wake Paul Kagame ndiyo mwenyekiti wa EAC kuanzia mwezi huu wa Februari.

Rwanda mara zote imekuwa ikikanusha madai hayo ya Burundi na kusisitiza mgogoro huo ni wa ndani na utasuluhishwa na Warundi wenyewe.

Mwaka jana Burundi ilibadili katiba yake na kuondoa ukomo wa madaraka kwa cheo cha rais.

Hata hivyo, Nkurunziza ametangaza nia ya kutokugombea tena uongozi wa nchi hiyo mwakani 2020.