Ripoti ya Freedom House: Kenya yapanda juu ya Tanzania kwa 'uhuru wa kidemokrasia'

Uhuru na Raila Odinga
Image caption Ushirikiano wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ambao uliifanya kenya kuwa katika picha tofauti ulichangia kujipatia alama 48.

Tanzania imepoteza nafasi yake kama taifa lenye uhuru wa kidemokrasia katika eneo la Afrika mashariki kwa Kenya na sifa yake sasa inaonekana kwamba inashindana na maeneo yenye hatari kisiasa duniani , ripoti mpya imesema.

Kulingana na gazeti la The Citizen nchini Tanzania, Dar imeshuka nafasi saba katika kipindi cha mwaka mmoja , na kupata alama 45 kwa jumla ikilinganishwa na alama 53 katika utafiti wa awali ambao ulikuwa umeiweka juu ya mataifa yote sita ya jamii ya Afrika mashariki EAC.

Lakini 'Uhuru' katika ripoti hiyo ya dunia 2019 iliotolewa siku ya Ijumaa unaonyesha kwamba Kenya ilio na alama 48 ndio inayoongoza katika uhuru wa kisiasa miongoni mwa mataifa ya Afrika mashariki.

Kulingana na gazeti hilo Kenya ilijipatia alama kama hizo katika ripoti iliotolewa ya 2018.

Kulingana na ripoti hiyo Burundi ina alama 18 na imetajwa kuwa taifa la mwisho lenye uhuru wa kisiasa ikifuatiwa na Rwanda yenye alama 23 na Uganda ilio na alama 37.

Hatahivyo licha ya tofauti hiyo ya alama , Tanzania na Kenya ni miongoni mwa mataifa yaliopo katika orodha yenye na uhuru mchache wa kisiasa katika utafiti huo.

Orodha nyengine ni zile za mataifa yalio 'huru' na yale 'yasio huru' huku Uganda, Burundi na Rwanda zikiorodheshwa miongoni mwa mataifa yasio na huru kisiasa.

Utafiti huo uliofanywa na shirika la Freedom House, hatahivyo umeiweka Tanzania miongoni mwa mataifa 10 inayoyaangazia mwaka 2019 .

Kulingana na The Citizen Tanzania , Freedem House ni shirika huru lililo na makao yake nchini Marekani linalopigania uhuru na demokrasia duniani.

Mbali na Tanzania , mataifa mengine yaliopo katika rada yake ni pamoja na Armenia, Brazil, Cambodia, Cameroon, China, Ethiopia, Iraq, Poland na Sri Lanka.

Freedom House linasema kuwa mataifa yalio katika orodha hiyo ni yale ambayo yalipata maendeleo ambayo yaliathiri mwelekeo wake wa kidemokrasia.

Ukamataji wa viongozi wa upinzani Tanzania

Ripoti hiyo inasema kuwa kushuka kwa Tanzania kunashirikishwa na serikali yake kukamata viongozi wake wa upinzani, kuzuia maandamano dhidi ya serikali na kuweka sheria ambazo zinaimarisha nguvu za chama tawala katika siasa za mashinani 2018.

Uganda ilishuka kutoka taifa lenye 'Uhuru kiasi' hadi lile lisilo na Uhuru kutokana na jaribio la rais Yoweri Museveni kuzuia uhuru wa bkujieleza , ikiwemo uchunguzi kupitia vyombo vya mawasiliano mbali na ukandamizaji kupitia kuiwekea kodi mitandao ya kijamii.

Ushirikiano wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ambao uliifanya Kenya kuwa katika picha tofauti ulichangia kujipatia alama 48.

Ripoti hiyo vilevile inaishirikisha Rwanda na ukamataji wa viongozi wa upinzani pamoja na tishio linalotolewa kwa vyama hivyo na rais Kagame.

Pia inasema kuwa uongozi wa Kagame wa kiimla umeathiri vibaya demokrasia nchini humo.

Nchini Burundi , inasema kuwa uongozi wa rais Pierre Nkurunziza umeendelea kuwanyamazisha wapinzani na kukiuka katiba.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii