Mauaji Njombe: Mtoto mwengine afariki hospitali baada ya kushambuliwa mwezi Disemba

Huwezi kusikiliza tena
Muaji Njombe: "Matumaini ya mama yaliokatizwa kwa mwanawe aliyeazimia kuwa Daktari

Janga la mauaji ya watoto mkoani Njombe, kusini magharibi Tanzania bado linaendelea ambapo mtoto mwengine amefariki dunia wikendi.

Mtoto Meshack Myonga mwenye miaka minne amefariki dunia Jumamosi baada ya kupata majeraha shingoni yaliyosababishwa na watu waliomteka.

Kifo hicho kimetokea katika hospitali ya rufaa ya Mbeya ambako alikuwa akipatiwa matibabu na amezikwa jana Jumapili.

Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la Mwananchi, Myonga alitekwa na mtu asiyejulikana Disemba 23 mwaka jana akiwa nyumbani kwao.

Mtoto huyo alipatikana msituni akiwa uchi huku shingo yake ikiwa inamiminika damu.

Mtoto huyo aliwahishwa hositali baada ya kupatikana na aliruhusiwa kurudi nyumbani Januari 19. Alitakiwa kurejea hospitali Ijumaa ya wiki iliyopita Februari 8 kwa ajili ya kuangaliwa maendeleo yake na kutolewa nyuzi.

Haki miliki ya picha Ikulu Tanzania
Image caption Waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania Kangi Lugola ameapa kukomesha matukio hayo

"Asubuhi (jumamosi) tulikwenda, mtoto akapelekwa chumba maalumu, Ilipofika saa nane mchana niliitwa na madaktari na kunipa taarifa kwamba mwanangu amefariki," amenukuliwa mama wa mtoto huyo Rabia Mlelwa na gazeti la Mwananchi.

"Wakanambia mwanangu koromeo lake lilikuwa limesinyaa na kwa ndani damu ilikuwa inavuja, hivyo alikuwa ni mtu wa kufa muda wowote."

Watoto takribani 10 wameshauawa toka visa hivyo vya kutamausha kuanza kuripotiwa mwezi Disemba.

Miili ya watoto hao imekutwa ikiwa imenyofolewa baadhi ya viungo kama matumbo, vidole, pua na macho. Wauaji hao pia wamekuwa wakinyofoa viungo vya siri vya watoto hao.

Mamlaka nchini Tanzania zimekuwa zikihusisha mauaji hayo na imani za kishirikina, waganga wa kienyeji wanalaumiwa kwa kuwaaminisha watu kuwa viungo vya binaadamu vinavuta bahati na utajiri.

Waziri Mkuu wa wa Tanzania Kassim Majaliwa Ijumaa aliliambia Bunge kuwa tayari watu 29 wameshakamatwa kutokana na matukio hayo, na kusema kuwa uchunguzi bado unaendelea.

Miongoni mwa waiokamatwa ni wafanyabiashara maarufu wa eneo hilo pamoja na waganga wa jadi.

Mada zinazohusiana