Watoto watatu wauawa na viungo vyao kunyofolewa katika mzingira ya kutatanisha Simiyu, Tanzania

Anthony Mtaka Haki miliki ya picha Anthony Mtaka
Image caption Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka ameiambia BBC kuwa uchunguzi wa mauaji hayo bado unaendelea.

Watoto watatu wameuawa na sehemu zao za siri kunyofolewa mkoani Simiyu, kando ya Ziwa Victoria nchini Tanzania.

Tukio la kwanza la mauaji hayo limetokea mwezi Oktoba mwaka jana na la mwisho mwezi huu, Februari 2019.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka ameithibitishia BBC kutokea kwa visa hivyo, akisema wananchi wanayahusisha mauaji hayo na ushirikina lakini serikali bado inachunguza undani wake.

Watu wanne wamekamatwa wakihusishwa na matukio hayo.

Matukio hayo ya Simiyu ni muendelezo wa visa vingine vilivyotokea mkoani Njombe, kusini magharibi mwa nchi hiyo ambapo watoto 10 wameuawa kufikia sasa.

Matukio yote ya Simiyu yametokea katika kata ya Lamadi wilaya ya Busega na tofauti na Njombe, yamehusisha watoto wakike tu.

Kwamujibu wa gazeti la Mtanzania, tukio la mwisho lilikuwa Februari 8 ambapo wili wa mtoto Joyce Joseph (8) uliokotwa vichakani baada ya kupotea kwa siku mbili. Disemba 13, mwili wa mtoto Milembe Maduhu (12) uliokotwa ndani ya jengo ambalo ujenzi wake haujakamilika na Oktoba 10 Susana Shija (9) alikutwa ameuawa na viungo vyake kukatwa.

Huwezi kusikiliza tena
Muaji Njombe: "Matumaini ya mama yaliokatizwa kwa mwanawe aliyeazimia kuwa Daktari

"Tayari watu wanne wanashikiliwa na majalada ya uchunguzi yamefunguliwa kwa baadhi ya washukiwa (ambao hawajakamatwa)...kuna imani za kishirikina zinazohusishwa na mauaji haya, wengine wanaamini yanachochewa na biashara ya madini, wengine uvuvi...lakini serikali bado inaendelea kuchunguza undani wake na hivi karibuni tutatoa taarifa rasmi."

Mtaka pia amesema hatua za haraka zimechelewa kutokana na uelewa mdogo wa jamii husasni katika kutoa ripoti ya matukio hayo, lakini kwa sasa udhibiti wa kiulinzi umeimarishwa.

"Wananchi pia wameeleza kuwa hawana imani na polisi wa eneo hilo. Hiyo ni changamoto ambayo pia tutaishughulikia ipasavyo...Pia wametaka kupiga kura ya kuwataja wale wanaowashuku kuhusika na matukio hayo. Tumewakubalia na kesho (Alhamisi) kura hiyo itapigwa, lakini majina yatakayotajwa tutayachukulia kama ushahidi wa awali na hatua zote za kiuchunguzi zitafuatwa," amesema Mtaka.

Haki miliki ya picha JAMES FESTO
Image caption Washukiwa watatu wa Njombe wamefikishwa mahakamani jana kujibu mashtaka ya mauaji

Tayari washukiwa watatu wa Njombe wamefikishwa mahakamani jana kujibu mashtaka ya mauaji.

Mratibu wa Jukwaa la Mashirika ya Kutetea Haki za Watoto Erick Giga ameieeza BBC kuwa matukio ya Njombe na Simiyu yanazaa hofu kubwa ambayo inabidi ishughulikiwe ipasavyo.

"Kuna changamoto za uelewa ambapo hapa elimu inatakiwa kutolewa kwa watoto shuleni na majumbani kuhusu hali hatarishi na nmana gani ya kujikinga nazo. Wazazi pia wanatakiwa kufuatilia kwa karibu usalama wa watoto wao.Pia kuna chamgamoto za kiusalama, kuanzia kuripoti matukio na kufanyiwa kazi na vyombo vya usalama. Kama wadau wote hao watatimiza wajibu wao ipasavyo basi hali itaimarika."