Mbunge wa Iramba Mwigulu Nchemba amenusurika ajali ya barabarani Tanzania

Mbunge wa Iramba Mwigulu Nchemba Haki miliki ya picha Nchemba/facebook

Aliyekuwa waziri wa maswala ya ndani nchini Tanzania, Dr Mwigulu Nchemba, amenusurika ajali mbaya ya barabarani baada ya gari lake alilokuwa akisafiria kuhusika katika ajali katika eneo la Migori huko Iringa.

Dkt. Nchemba ambaye ni mbunge wa Iramba magharibi alikuwa akisafiri kutoka Iringa kuelekea Dodoma, wakati gari lake lilipopata ajali hiyo katika eneo la Migori kulingana na kamanda wa polisi katika eneo la Dodoma bwana Gilles Murotto.

Picha zilizokuwa zikionyesha gari lake lilivyoharibika zilisambazwa sana katika mitandao ya kijamii mapema siku ya Jumatano zikionyesha vile lilivyoharibika upande wa abiria eneo ambalo Nchemba alikuwa ameketi.

Bwana Nchemba alikimbizwa katika hospitali ya Benjamini Mkapa mjini Dodoma.

Mkurugenzi wa hospitali ya Benjamini Mkapa Alphonce Chandika alisema kuwa Dr Mwigulu alikuwa akilalamikia maumivu katika kiuno chake na mguu wake wa kulia.

''Tumemfanyia vipimo kwa kutumia mashine tofauti ikiwemo ile ya CT Scan'', aliambia gazeti la The Citizen tanzania.

Image caption Rais Magufuli akimpongeza aliyekuwa waziri Mwigulu Nchemba kwa wadhifa wake mpya

Dkt. Mwigulu Nchemba aliwahi kulifanyia kazi baraza la mawaziri la rais Magufuli kabla ya uteuzi wake kutenguliwa na kiongozi huyo.

Licha ya hapo awali kuhamishwa kutoka wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi, hadi wadhfa wake wa mwisho, Nchemba alihudumu kwa miaka miwili katika baraza la Rais Magufuli.

Nafasi ya mbunge huyo wa Iramba aliyechukua nafasi ya aliyekuwa waziri Charles Kitwanga, ilichukuliwa na mbunge mwenzake kutoka Jimbo la Mwibara, Kangi Alphaxard Lugola ambaye amejaza pengo lake.

Mwigulu Nchemba alipata umaarufu kwa juhudi zake za kuzuia maandamano dhidi ya Rais Magufuli.

Alinukuliwa akitishia kuwalemaza waandamanaji na ''kuwakamata hata watakaoandamana wakiwa nyumbani".

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii