Je, Tundu Lissu ni 'adui' wa Tanzania?

Tundu Lissu

Gumzo ni kubwa kila kona ya taifa letu. Kuanzia mitandao ya kijamii hadi vyombo vikubwa vya habari vya ndani ya nchi na kimataifa.

Vyombo vyote vinamzungumzia Tundu Lissu, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Mnadhimu wa Kambi Rasmi Bungeni na mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Baada ya kufanya mahojiano na BBC nchini Uingereza na DW nchini Ujerumani, Lissu alivuka bahari ya Atlantiki kuelekea Marekani.

Akiwa kwenye mdahalo katika kipindi cha Straight Talk Africa nchini Marekani, Lissu alikabiliana vikali na Balozi wa Tanzania nchini humo, Wilson Masilingi.

Lissu ameshiriki kwenye mdahalo wa 'uhuru wa kujieleza' katika Chuo Kikuu cha George Washington, ulioitishwa na Mkurugenzi wa Jennifer Cooke wa Taasisi ya Uhusiano wa Kimataifa na Masomo ya Kiafrika nchini Marekani.

Kote huko ameendelea kuihusisha serikali ya rais John Magufuli kwa shambulio la risasi zaidi ya 30 dhidi yake, na kuutuhumu kuminya kwa makusudi demokrasia na uhuru wa kujieleza.

Midahalo hiyo imeendelea kukoleza moto wa gumzo kumhusu Lissu, baina ya pande zinazomuunga mkono na kumpinga.

Katibu Mkuu wa chama tawala CCM, Dkt Bashiru Ali akiwa kwenye ziara ya kikazi wilayani Kilosa mkoani Morogoro alisema Lissu anaugua ugonjwa wa deko hivyo ni muhimu kwa kutibiwa ugonjwa huo.

Dk. Bashiru amekuwa kigogo wa kwanza ndani ya chama tawala kutoa kauli ya kisiasa kuhusiana na ziara anayofanya Tundu Lissu ughaibuni.

Haki miliki ya picha IKULU, TANZANIA
Image caption Waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania Kangi Lugola amemtaka Lissu kurejea nchini humo ili kusaidia upelelezi wa shambulio dhidi yake.

Naye waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania Kangi Lugola amemtaka Lissu kurejea Tanzania ili kusaidia uchunguzi wa kesi yake.

Tayari bungeni kumeshatolewa hoja ya kutaka mshahara wake uzuiliwe kwa kile kilichoitwa kuzurura nje ya nchi na kutukana bunge na serikali.

Spika wa Bunge, Job Ndugai ameonekana akikubaliana na pendekezo hilo.

Na hata kabla alishaonya juu ya wa kufutwa ubunge wake kwa kile kilichoelezwa utoro bungeni, jambo ambalo limetafsiriwa kuwa la kisiasa zaidi.

Makundi mawili ziara za Lissu

Tundu Lissu alishambuliwa watu wasiojulikana hadi leo ambapo alimiminiwa risasi takribani 16 mwilini mwake. Tukio hilo lilifanyika mchana wa tarehe 17 mwezi Septemba mwaka 2017 jijini Dodoma. Umetimia mwaka mmoja na miezi minne sasa, huku suala la uchunguzi likiwa ni kitendawili kisicho na jawabu.

Hatua ya Lissu kufanya ziara inaweza kumwongezea wafuasi kwenye siasa na kupandisha umaarufu wake huku akiwa ameshatanagza nia ya kugombea urais katika uchaguzi ujao wa mwaka 2020 iwapo cahama chake kitakubaliana na kumpa jukumu hilo.

Kundi la kwanza linamwona Lissu kama msaliti wa taifa na baadhi wametoa kauli za kisiasa kuwa ni mhaini.

Haki miliki ya picha BUNGE, TANZANIA
Image caption Spika Ndugai amesema atafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kushughulikia hoja ya kusitisha mshahara wa Tundu Lissu.

Kundi linalompinga Lissu wanatumia Ibara ya 28 kifungu cha 4 cha Katiba ya Tanzania ambayo inatamka "uhaini kama unavyofafanuliwa na sheria utakuwa ni kosa la juu kabisa dhidi yua Jamhuri ya Muungano."

Kundi la pili wanasema ziara za Lissu zinasimamiwa na Ibara ya 18 (kifungu cha A hadi D) ya Katiba ambayo inampa uhuru na haki ya kutoa maoni juu ya jambo lolote bila kuvunja sheria nyingine.

Kundi hili wananukuu pia Ibara za 16 (kifungu cha kwanza) ambacho kinatamka "kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na unyumba wake, na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasilianbo yake ya binafsi,".

Aidha, kundi hili linaongezea kutumia ibara ya 17 kiufungu cha kwanza ambacho kinaeleza kila raia anayo haki ya kwenda kokote na kuingia, pamoja na kifungu cha 2(a) na (b)(i-iii).

Vilevile Ibara ya 29 kifungu cha 2 inaelezwa "kila mtu katika Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kupata hifadhi sawa chini ya sheria za Jamhuri ya Muungano,".

Lissu anapita njia ya Tsvangirai

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Morgan Tsvangirai enzi za uhai wake akiwa kiongozi wa upinzani Zimbabwe aliwahi kufanya ziara za kimataifa na kueleza madhila yanayoukumba upinzani nchini mwake.

Bila kujali kuwa anachofanya Lissu ni sahihi au si sahihi. Bila kujali matamshi anayotoa mbele ya kamera za televisheni kupitia vipindi mbalimbali, bado Tundu Lissu, anapita njia ambayo katika duru za kisiasa zimefanywa mara nyingi na wanasiasa na ujumbe wake ndiyo matokeo yanayofikirisha zaidi na kuibua mijadala juu ya hoja zake.

Duru za kisiasa barani Afrika zinalikumbuka jina la mwanasiasa mahiri Morgan Tsvangirai. Huyu alikuwa Rais wa Chama cha upinzani cha MDC kilichokuwa ngome ya kambi ya upinzani na kikichuana na ZANU PF katika chaguzi mbalimbali nchini Zimbabwe. Yeye na katibu wake wa wakati huo Tendai Biti walitengeneza kambi yenye nguvu kisiasa nchini Zimbabwe.

Katika chaguzi mbalimbali, kama vile mwaka 2000, 2002, 2005 na 2008 ambapo Morgan Tsvangirai, alichuana na Robert Mugabe bila mafanikio.

Tsvangirai alitembelea nchi za Ufaransa, Uingereza na Marekani. Malengo ya ziara hiyo yalikuwa kuwaomba wafadhili wakate misaada na kuweka vikwazo dhidi ya iliyokuwa Serikali ya Robert Mugabe na chama cha ZANU-PF kutokana na hali mbaya ya uchumi, siasa za hofu na vitisho, kudhalilishwa wapinzani na mengineyo yaliyo kinyume cha demokrasia.

Ndiyo kusema njia anazopita mwanasiasa Tundu Lissu ni zilezile zilizotumiwa na marehemu Morgan Tsvangirai.

Mustakabali wa Lissu

Huwezi kusikiliza tena
Tundu Lissu: 'Chama kikisema mimi nafaa, niko tayari kuwa rais Tanzania'

Swali moja kubwa ambalo kila mmoja anatakiwa kuuliza ni; uchunguzi wa shambulio dhidi ya Tundu Lissu umefikia hatua gani au wapi? Ikumbukwe, umetimia mwaka mmoja na miezi minne tangu kutokea shambulio dhidi ya Tundu Lissu jijini Dodoma, lakini vyombo vya dola havijatoa matokeo ya uchunguzi.

Ndiyo kusema hatuwezi kuvisingizia vyombo vya dola kuwa havikufanya uchunguzi kwakuwa tutavikosea heshima.

Hata kama si kila taarifa za uchunguzi zinapaswa kufika kwa umma, lakini kwanini imeshindikana hata bashraf ya suala lenyewe kuelezwa kinaga ubaga?

Inawezekana matamshi au hoja za Tundu Lissu zinaweza, na pengine si tu kukera wenye mamlaka bali pia hata wafuasi na watu wengine kwa kuwa yanazungumzwa nje ya nchi yetu, lakini swali kuu ambalo lingeweza kuondoa maudhi au kero hiyo ni uchunguzi wa shambulio hilo au ukweli na uwazi.

Pamoja na chama na serikali kutupiwa matope ya kila namna, inawezekana kabisa wangesafisha kuondoa matope hayo kwa kutoa taarifa za uchunguzi wa awali na kufikisha kwa umma. Kwahiyo kundi linalomlaumu Tundu Lissu linapaswa kufikiri, je kama wangelikuwa wao wangefanya nini kwa maumivu yote aliyopitia?

Lengo ni kusimama kwenye ukweli kuwa kila raia anatakiwa kulindwa na kupatiwa hifadhi kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania Ibara ya 29 kifungu cha 2 "Kila mtu katika Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kupata hifadhi sawa chini ya sheria za Jamhuri ya Muungano."

Aidha, tunapaswa kufikiri pia, Tundu Lissu kama mwanadamu ni lazima awe na maadui bila kujali kazi yake ya siasa, kwani kuna mahusiano mengine yanatuhusu katika maisha. Lakini sakata lake limehusishwa na harakati za siasa na haki za binadamu ambalo linagusa ubunge wake na kama mwanasiasa. Ukweli ni kwamba, hatua aliyofikia Lissu ni matokeo ya kukata tamaa juu ya kutatuliwa sakata lake, ambalo lina nafasi kubwa kulisafaisha taifa na serikali ya nchi yetu.

Wataalamu wa saikolojia wanaweza kutusaidia kwa kusema, Lissu amefikia kilele, yaani "liwalo na liwe au sina cha kupoteza". Anawajibika kulinda maisha yake na anahitaji watu ili afanikishe hilo, hii ni kanuni rahisi tu. Kumtarajia Tundu Lissu aseme mema ya serikali yetu ya Tanzania kwa madhila yaliyompata ni sawa na kusubiri meli katika uwanja wa ndege.

Mada zinazohusiana