Uganda yathibitisha kumtimua mkurugenzi mtendaji wa MTN Wim Vanhelleputte

MTN Uganda Haki miliki ya picha ISAAC KASAMANI

Mamlaka nchini Uganda zimethibitisha kuwa zinafanya uchunguzi kuhusiana na madai ya wafanyakazi wa kampuni kubwa ya mawasiliano nchini humo MTN kuhitilafisha usalama wa nchi.

Hii ni baada ya mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Wim Vanhelleputte kutimuliwa na kurudishwa nchini Ubelgiji alikotoka katika hali ya kutatanisha.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali Ofwono Opondo, bw. Wim Vanhelleputte alikiuka masharti yaliyoko kwenye kibali chake.

''Vanhelleputte alipuuza maagizo ya ulinzi chini Uganda na kwa kukutana kisiri na wafanyikazi wenzake watatu waliofukuzwa humu nchini'' alisema bw. Ofwono.

Hata hivyo msemaji wa serikali ameshauri usimamizi wa MTN kwenda mahakamani ikiwa wanahisi kwamba wafanyakazi wao hawakutendewa haki.

Lakini kampuni hiyo, inayohudumu Afrika na katika mashariki ya kati, inasema haikupewa sababu maalum kwanini mkurugenzi wao huyo ametimuliwa.

Polisi imesema kuwa itaendelea na uchunguzi na ikiwa kuna mfanyakazi mwengine wa MTN atakayepatikana na hatia ya kuhujumu usalama wa nchi kuchukuliwa hatua.

Taarifa ziliibuka Alhamisi kwamba bwana Wim Vanhelleputte alipelekwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa na kulazimishwa kuabiri ndege iliyokuwa ikiondoka Uganda.

Msemaji wa polisi anasema hii inafuatia hali inayohusu usalama wa kitaifa.

Na ndio sababu sawiya iliyotolewa baada ya kutimuliwa kwa wafanyakazi watatu wa nje katika kampuni hiyo ya MTN Uganda waliotoka nchini Rwanda Ufaransa na Italia.

Haki miliki ya picha ISAAC KASAMANI

Kwa wakati huo, Bi Elsa Mussolini, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Mobile Financial Services, alisema alitimuliwa kwa tuhuma kwamba alikuwa anafadhili shughuli za kiongozi wa upinzani Bobi Wine.

MTN pia iligubikwa katika mzozo wa umma na serikali kuhusu kupewa kibali kipya cha kuhudumu nchini.

Rais Yoweri Museveni alihoji kwanini mkaguzi mkuu aliweka malipo ya kupata kibali kipya kuwa cha thamani ya dola milioni 58 kutoka dola milioni 100 million.

Mwezi uliopita, rais Museveni alikutana na mkurugenzi mtendaji wa kundi la kampuni za MTN Rob Shuter kando kando mwa mkutano wa kimataifa wa uchumi - World Economic Forum huko Davos.

Baada ya mkutano huo, rais alituma ujumbe kwenye twitter kwamba kampuni hiyo inahitaji kuorodhesha hisa zake katika soko kuu la hisa Uganda kuhakikisha kwamba baadhi ya faida zake zinasalia katika nchi hiyo.

Aliishutumu kampuni hiyo pia kwa kutotangaza kwa uhalisi kiwango chake cha mawasiliano ili kukwepa kodi.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii