Je neno Boda Boda limetokea wapi Afrika?

boda Haki miliki ya picha MARCO LONGARI

Chimbuko ya bodaboda ni utashi wa wajasiriamali kuvuka mpaka wa Uganda kwenda Kenya, mwaka 1972 - muda mfupi baada ya Idi Amin kuipundua serikali ya Milton Obote katika 1971.

Uhaba wa vitu muhimu majumbani Uganda, uliwafanya wafanyabiashara kutaka usafiri bora wa kuvusha bidhaa kama sukari na chumvi, masafa ya kilomita moja hivi kutoka Kenya, eneo la Busia.

Boda Boda ikazalika.

Kama biashara ndogo ya faida, bodaboda inavutia vizito na mabepari kwa mikopo;.

Kwa wingi wake, inavutia wenye vyeo na vyama; kwa wepesi wake, inavutia wahalifu.

Kwa hesabu za mwaka 2013, Uganda ilitumia zaidi ya $30m kuagiza pikipiki, siku hizi zinaundiwa nchini.

Haki miliki ya picha MARCO LONGARI

Huku 70% ya Waganda wakitegemea uchukuzi wa umma, teknolojia ya kurahisha usafiri ikizidi kusasishwa, mustakabali wa bodaboda ni mzuri, licha changamoto za utovu wa sheria barabarani, ajali, na uhalifu.

Tangu bodaboda izinduliwe, kama mfumo wa uchukuzi miaka 47 iliopita, sasa ni ya pili kwa ajira, baada ya kilimo.

Kama kiserema katika kilimo, mwanzo duni wa bodaboda, ulikuwa Baskeli.

Neno Boda Boda limetoka wapi?

Asili ya neno bodaboda, mwasisi wa mfumo huo, Pascali Bwire, anasema, ilikuwa utashi wa wafanyabiashara kuvuka kienyeji masafa ya maili moja, kati ya mpaka wa Uganda na Kenya kwa baskeli, kubeba bidhaa kama sukari, chumvi, unga na sabuni mwaka 1972.

Biashara 'nzuri' wakati huo.

Leo bodaboda ime-sasishwa, toka kengele na magurudmu mawili ya spoki, hadi Pikipiki; na si mpakani tu.

Imesambaa mijini na vijijini Uganda. Inakisiwa nusu milioni ziko ndani na kuizunguka Kampala peke yake.

Haki miliki ya picha LUIS TATO

Ni uchukuzi wa uzito na haraka zaidi, kupita njia ya vichochoro, panda na shuka vilima, inafika gari zisikofika.

Maelfu ya wapanda bodaboda, wendeshaji, hasa vijana wanaume, wanapata ajira: kama mwajiriwa, au mshirika, au mfanyabiashara pekee, kama huyu Kasibante.

Yeye anajitegemea; anatumia mfumo wa tangu zamani kupata wateja: watu wamjuaye, simu ya mkononi, na kuota njiani. Teknolojia imeingilia.

Huduma hii mpya, bodaboda za kuitwa, unaendeshwa na mashirika mfano Taxify, Safeboda, Uber.

Inakisiwa zaidi ya bodaboda 10,000 ni wanachama wa mashirika hayo, yakielezwa kama salama, haraka, bei nafuu na ni mustakabali wa bodaboda.

Ingawa yasemwa, kiingiacho mjini si haramu, kampeni ya upinzani, chini ya kundi la Bodaboda Industry Uganda (au BIU) inadai, mpango wa Taxify, Safeboda, Uber na wengineo, kutumia simusmati na app, ni wa kuwatapeli wendeshaji.

Haki miliki ya picha ALEXIS HUGUET

Katika Uganda, 85% ya wendeshaji bodaboda, ni waajiriwa, huwategemea matajiri au wako chini ya shirika.

Mwanzoni bodaboda ilibaini mgawanyo wa kijamii, si tu kiajira lakini pia kiabiria, kama usafiri wa watu wa chini.

Mwimbaji na mtangazaji mashuhuri wa zamani, hayati Elly Wamala, aliyakisi hayo katika wimbo wake, boda-boda:

Ubeti unasema, 'bodaboda hutoza pesa sahili, ili asikukamue na kukufanyia ngumu. Na katika wimbo kusema, hawa ni watu wa manufaa sipendi watetwe; sisi akina-yahe hatumudu gari mpya, bodaboda hakika zimetufaa kabisa; sisi makabwela zimetuponya…'

Ukweli wa mambo, hata wenye vyeo na vyao siku hizi wanapanda bodaboda, kama si kwa lolote jengine, asichelewe endako.

Licha ya kutanuka tasnia ya bodaboda nchini Uganda lakini bado wadadisi wanasema uchumi wa bodaboda unatoa mchango kidogo tu katika ukuaji wa uchumi.

Hilo ni la kuvaliwa njuga na wakuu.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii