Nigeria; Waaangalizi wa kimataifa kuingilia kati uchaguzi mkuu

Wapiga kura walaani kusogezwa kwa uchaguzi katika dakika za majeruhi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wapiga kura walaani kusogezwa kwa uchaguzi katika dakika za majeruhi

Waaangalizi wa kimataifa katika uchaguzi mkuu uliosogezwa mbele nchini Nigeria wametoa wito kwa raia wa taifa hilo kuwa watulivu wakati maandalizi ya uchaguzi yanaendelea.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Mahmood Yakubu, amedai kuwa kuchelewa kwa uchaguzi huo hakuhusiani na ushawishi wa kisiasa kwa namna yeyote.

Hata hivyo Rais wa Muhammadu Buhari na mpinzani wake Atiku Abubakar wameelezea kutoridhishwa kwao na hatua hiyo ya tume ya uchaguzi kusogeza mbele tarehe ya upigaji kura kwa madai ya kutokamiliaka kwa baadhi ya maandalizi muhimu.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Atiku Abubakar amewataka raia kuwa na subira

Atiku Abubakar, ametoa wito kwa wananchi wa Nigeria kuwa watulivu na kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi iliyotangazwa.

Wakati mwenyekiti wa chama cha PDP, Uche Secondu, alisema kucheleweshwa kwa uchaguzi ni hatari kwa demokrasia na vilevile kumshutumu Rais Buhari kujaribu kuendelea kubaki katika nafasi hiyo wakati wanigeria wanataka aondoke madarakani.

Wapiga kura wanasemaje?

Katika maeneo mengi wapiga kura wameonekana wakiwa na hasira na kulalamikia kuchelewa kwa uchaguzi huo.

Haki miliki ya picha Reuters

Bwana Yakubu amesema uamuzi huo umechukuliwa baada ya 'ukaguzi wa makini' wa 'mpango ya namna uchaguzi utakavyofanyika', akiongeza kwamba kuna 'jitihada kubwa za kuhakikisha kuna uchaguzi wa huru, haki na wa kuaminika'.

Amesema ni muhimu kuchelewesha uchaguzi huo kuipa tume nafasi ya kukabiliana na masuala muhimu na pia "kusalia na hadhi katika uchaguzi", lakini hakutoa ufafanuzi zaidi.

Katika wiki mbili zilizopita ofisi kadhaa za tume hiyo ya uchaguzi ziliteketezwa moto, huku maelfu ya vifaa vya kunakili kadi , na kadi za upigaji kura zikiharibiwa.

Pia kumekuwa na taarifa ya uhaba wa vifaa vya upigaji kura katika baadhi ya majimbo 36 ya nchi hiyo.

Nigeria imelazimika kushinikiza usalama wake kuelekea katika uchaguzi huu uliokumbwa na ghasia.

Uchaguzi huu ni muhimu kiasi gani?

Mustakabali wa taifa lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika na lenye uchumi mkubwa, umo katika mizani.

Haki miliki ya picha Getty Images

Yoyote atakayeshinda inabidi ashughulikie masuala kama uhaba wa umeme, rushwa, ukosefu wa usalama na uchumi unaojivuta.

Kuna wagombea 73 waliosajiliwa katika uchaguzi wa urais, lakini kampeni zimegubikwa na Rais Muhammadu Buhari, mwenye umri wa miaka 76, na mpinzani wake mkuu, aliyekuwa makamu wa rais Atiku Abubakar, mwenye umri wa miaka 72.

Buhari anasema amejenga msingi madhubuti kwa ustawi, lakini mpinzani wake anasema Nigeria mambo hayaendi sawa.

Wote wanatoka eneo la kaskazini mwa nchi lenye idadi kubwa ya waislamu. Wakati wote wana umri wa miaka 70, zaidi ya nusu ya idadi jumla ya watu Nigeria, milioni 84 waliosajiliwa kupiga kura wana umri wa chini ya miaka 35.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii