Jeshi la Polisi Uganda laidhinisha jitihada za kuangamiza ufisadi

Polisi Uganda Haki miliki ya picha ISAAC KASAMANI

Jeshi la polisi nchini Uganda limeazimia kujiondoa kutoka kwenye orodha ya taasisi zinazoongoza katika ufisadi Uganda.

Kufuatia uzinduzi wa mpango mkakati wa kupambana dhidi ya maovu hayo, wakuu katika jeshi hilo wanatoa ahadi kuwa watawaadhibu vikali maafisa watakaopatikana wakihusika katika vitendo vya ulaji rushwa.

Taarifa za kila mwaka kuhusiana na masuala ya ufisadi huiweka polisi ya Uganda katika nafasi ya kwanza katika maovu hayo.

Hii imejenga sifa mbaya kwa jeshi hilo miongoni mwa wananchi ambao wamendelea kupoteza imani kama wanaweza kutendewa haki kisheria kupitia taasisi hiyo.

Lakini sasa jeshi hilo limefungua ukurasa mpya kwa kuzindua mkakati mahususi wa kuelimisha askari wake kujiepusha na vitendo hivyo na wafahamu majukumu yao kulingana vyeo vyao.

Edward Ochom, naibu Inspekta wa polisi amefafanua, 'Hata dhamana ya polisi unakuta miaka iliyopita, askari polisi ambaye hata hana cheo anamuachia mtu kwa dhamana. Sasa tunasema hapana.

'Aliye na mamlaka ya kutoa dhamana ni mkuu wa kituo cha polisi, mkuu wa upelelezi, au naibu wake. Hili ni miongoni mwa mikakati ambayo tunaweka pamoja na maafisa wetu, kufanya usimamizi badala ya kuachia maafisa wa chini kufanya wanavyotaka. Nafikiri hili litatekelezwa na kupunguza vitendo vya ufisadi katika jeshi la Polisi,' ameongeza Ochom.

Haki miliki ya picha SUMY SADURNI

Mkakati huo uliotayarishwa kwa usaidizi wa shirika la maendeleo la umoja mataifa UNDP unatoa mwongozo jinsi polisi watakavyofuata sheria mbalimbali za nchi katika kutekeleza majukumu yao.

Miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa ili kuwashawishi askari polisi kutoshiriki ulaji rushwa, ni pendekezo la kuwaongezea mishahara pamoja na kuboresha maslahi yao na ya familia zao.

Aidha mazingira bora ya kutendea kazi yatazingatiwa.

Kwa jumla kitengo chote cha kisheria ikiwemo mahakama na magereza huelezewa kuhusika katika vitendo vya ulaji rushwa uliokithiri.

Ni kwa ajili hii ndipo kuna mashaka kama polisi pekee itaweza kujirekebisha bila taasisi hizo nyingine kuwa na mikakati kama yao.

Haki miliki ya picha Getty Images

Rushwa katika idara za serikali

Sheria kadhaa na taasisi zimeidhinishwa kwa miaka mingi Uganda ikiwemo ya ukaguzi wa serikali kuchunguza na kuwaadhibu wanaofuja mali za umma.

Mwishoni mwa mwaka jana 2018 Rais Yoweri Museveni wa Uganda alizindua kitengo kipya cha kupambana na rushwa nchini Uganda chini ya uongozi wa Luteni Kanali Nakalema na hasa katika idara zote za Serikali.

Rais Museveni alieleza kuwa jukumu la kupambana na rushwa liko kwa wananchi, ambao amewataka kuwasiliana na kitengo hicho kipya kitakacho hudumu moja kwa moja chini ya ofisi yake.

Uganda imeorodheshwa katika nafasi ya 151 kati ya mataifa 180 yaliochunguzwa kwa rushwa katika ripoti ya Februari 2018 ya shirika la Transparency International.

Ni ya tatu iliyokithiri ufisadi Afrika mashariki baada ya Sudan kusini na Somalia.

Wakosoaji wanalitaja hilo kama donda sugu lililo ishara ya tatizo kubwa katika vita dhidi ya rushwa Uganda.

Shirika la Transparency International linaeleza katika ripoti yake hiyo kwamba pasi kushughulikiwa, huenda nchi hiyo isipige hatua.

'Katika ripoti kuhusu utoaji huduma kwa taifa mwaka 2015' iliyochapishwa na idara ya takwimu Uganda (UBOS) - Idara ya polisi nchini humo ndio iliyoorodheswha kuwa yenye ufisadi mkubwa na 'idadi kubwa ya walioshiriki katika utaifiti wa ripoti hiyo walikubaliana na hilo'.

Katika mapendekezo yaliotolewa wakati huo, kuna haja kubwa ya kushinikiza utekelezaji wa sheria dhidi ya ufisadi nchini.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii