Mvutano kuhusu mpaka unavyohatarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Kenya na Somalia

Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Farmajo na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta
Image caption Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Farmajo na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta

Somalia imekanusha tuhuma kwamba imenadi maeneo ya mafuta yaliopo katika mpaka unaozozaniwa kati ya taifa hilo na Kenya.

Katika taarifa yake hapo jana Jumapili , serikali ya Somalia imesema 'haina mipango wala haikuwa na mipango ya kufanya hivyo'.

Taarifa hiyo ilitolewa baada ya kuwepo ripoti za kikao kilichofanyika katika mji mkuu Mogadishu cha maafisa wakuu serikalini akiwemo rais mwenyewe Mohamed Abdullahi Mohamed Farmajo na waziri mkuu Hassan Ali Khayre.

"Somalia kwa sasa haina mpango wala haikuwa na mpango wa kunadi sehemu yoyote katika eneo linalo zozaniwa baharini hadi pale mahakama ya ICJ itakapobaini mipaka ya nchi husika," imeeleza taaifa hiyo rasmi.

Imetoa ahadi kwa Kenya kuwa haitojihusisha katika shughuli zozote katika maeneo yalio kwenye mzozo hadi mahakama itakapotoa uamuzi wa mwisho.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Somalia imeihakikishia Kenya kuwa itasubiri uamuzi wa mwisho wa mahakama ya ICJ

Siku ya Jumamosi jioni, Nairobi ilitangaza kuwa inamrudisha nyumbani balozi wake aliyepo Mogadishu Luteni Jenerali mstaafu Lucas Tumbo, ikidai kuwa uamuzi wa Somalia kupiga mnada eneo moja la mafuta mjini London wiki iliopita ni sawa na uchokozi dhidi yake na mali yake asili.

Vilevile Nairobi ilimrudisha nyumbani balozi wa Somalia nchini Kenya Mohamed Nur katika kile ambacho serikali ya Kenya baadaye ilifafanuwa kwenye vyombo vya habari nchini kuwa ni kutoa fursa ya majadiliano ya kila upande katika suala hilo.

''Kwa kupuuza suluhu ya sheria za kimataifa kuhusu mipaka ama makubaliano ya kisiasa kupitia diplomasia , serikali ya Somalia imeonyesha wazi bado haijakomaa kisiasa'' , amesema katibu wa maswala ya kigeni nchini Kenya Macharia Kamau.

Somalia kupitia wizara ya mambo ya nje, imeelezea masikitiko yake kufuatia hatua hiyo ya Kenya kumrudisha balozi wake pasi kuwepo mashauriano.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Eneo linalozozaniwa linakakisiwa kuwa na mafuta na gesi

Mambo 3 makuu yanayohatarishwa kwa mvutano huu

Kumeshuhudiwa mvutano na malumbano kuhusu mipaka baina ya mataifa hayo mawili katika siku za nyuma.

Baadhi ya wachambuzi wanaona kwamba hili ni jambo lisilohitajika kwa sasa.

Na huenda ni jambo ambalo mataifa yote mawili yanalitambua kutokana pia na kauli ya Somalia kwenye taarifa yake jana ya kukanusha madai hayo ya kupiga mnada mafuta na gesi katika eneo hilo linalozozaniwa, kwa kukiri kwamba 'mataifa hayo "yameshikana katika namna ambayo hayawezi kuvunjika" na kuwa yana uhusiano mzito wa kihistoria na kitamaduni, ambayo Somalia haitaki kuuvunja.

Kwa jumla, ni mataifa yanayotegemeana.

Mchambuzi wa masuala ya Afrika, Ibrahim Aidid, anasema Kenya na Somalia ni mataifa ambayo yameweza kufanya vitu vingi kwa pamoja na kwa ushirikiano mkubwa.

Mataifa hayo mawili yamekuwa yakishirikiana katika masuala ya:

Usalama:

Kenya inategemea ushirikiano mkubwa kutoka Somalia katika vita dhidi ya ugaidi, hususan dhidi ya kundi la wapiganaji wa Alshabaab, ambalo ni tishio sio tu kwa mataifa hayo mawili, lakini pia kieneo.

Wanajeshi wa Kenya pamoja na wanajeshi kutoka mataifa mengine kama Djibouti, Uganda na Ethiopia, chini ya mwamvuli wa kikosi cha kulinda amani Amisom, wamekuwa wakiisaidia serikali ya Somalia katika vita hivyo.

Wanajeshi wa Kenya waliingia Somalia mnamo mwaka 2011, kuwapiga vita wanamgambo wenye uhusiano na mtandao wa al-Qaeda.

Biashara:

'Kenya inapeleka biashara Somalia. Imenufaika pakubwa kifedha kwa bidhaa kwa mfano kama miraa zinazosafirishwa hadi Somalia', anasema mchambuzi wa kisiasa Ibrahim.

Usafirishaji wa miraa au mirungi hadi Mogadishu, ni biashara inayokisiwa kuwa na thamani ya karibu dola nusu milioni kila siku.

'Somalia kwa upande wake, inanufaika kwa biashara ya samaki wanaoingizwa Kenya' anasema Ibrahim.

Uhamiaji:

Maelfu ya wakimbizi kutoka Somalia wamehifadhiwa katika mojawapo ya kambi kubwa duniani ya Daadab iliopo nchini Kenya.

Kambi hiyo ya Dadaab ilijengwa mnamo 1991 kuzihifadhi familia za jamii zilizokuwa zinatoroka mzozo nchini Somalia, na baadhi ya watu wamekuwa wakiishi hapo kwa zaidi ya miaka 20.

Somalia inaitazama Kenya kama mshirika wake mkuu katika kufanya mageuzi ndani ya nchi hiyo.

Na huenda ndiyo mambo yanayostahili kupewa uzito kwa Rais Mohammed Abdullahi Farmajo na Rais Uhuru Kenyatta wanapotathmini na kutafuta suluhu kwa mvutano uliopo sasa, anasema mchambuzi Ibrahim.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii