Bwana mmoja raia wa Niger anasa uwanja wa ndege Ethiopia kwa miezi mitatu

Eissa Muhamad with Israeli flag

Raia mmoja wa Niger ambaye amefurushwa nchini Israeli amenasa uwanja wa ndege nchini Ethiopia toka mwezi Novemba mwaka jana.

Eissa Muhammad, 24, amenasa kwenye kiwanja hicho jijini Addis Ababa baada ya nchi yake kugoma kumpokea.

"Nimekuwa nikikaa hapa (uwanja wa ndege) katika mazingira magumu, hakuna kitu, hakuna kitu kabisa..." Muhamad ameiambia BBC.

Mikasa ilianza kumuandama Muhamad mwezi Aprili mwaka jana baada ya kunaswa akiishi Israeli bila ya kibali.

Kijana huyo alihamia Israeli kutoka Niger mwaka 2011, akiwa na miaka 16 ili kutafuta maisha bora.

Anasema aliwalipa wasafirishaji wa binaadamu ili kumpitisha nchini Libya na Misri kabla ya kuingia Israeli kwa miguu.

Alipofika jijini Tel Aviv, Tel Aviv, Muhamad aliishi kwa kutegemea kazi duni kwenye majumba ya kuishi wanafunzi na kiwanda cha kuzalisha pipi.

Baada ya kushikiliwa kizuizini kwa zaidi ya miezi sita, Israeli ilimpatia hati ya dharura ya kusafiri na kumpakia kwenye ndege ya Shirika la Ethiopia kuelekea Niger kupitia Addis Ababa mwezi Novemba.

Hata hivyo, baada ya kuwasili Niamey, mji mkuu wa Niger, alizuiwa na maafisa wa uhamiaji kuingia wakidai kuwa hati yake ya kusafiria ilikuwa ni ya kughushi.

"Hawakunitaka kuingia Niger. Hawakunikubali kabisa," amesema Muhamad.

Image caption Eissa Muhamad (kati kati) ameishi Israeli bila kibali kwa miaka saba

Baada ya mwezi mmoja wa kuziwa nchini Niger, alirejeshwa Israeli ambako aliwekwa tena kizuizini kwa wiki kadhaa.

"Walinifunga mikono na miguu yangu na kunilazimisha kuingia kwenye ndege na kunirudisha Niger ambapo walinikataa tena."

Hati aliyopewa ya kusafiria na Israeli ikaisha muda wake alipokuwa njiani katika uwanja wa kimataifa wa Bole, Ethiopia baada ya Niger kumkataa tena. Mpaka wa leo bado amenasa hapo.

saada wa chakula

BBC imejaribu bila mafanikio kuwasiliana na wizara ya mambo ya nje ya Niger na ubalozi wake jijini Addis Ababa ili kujua kwanini hawataki kukubali hati ya kusafiria ya raia wao.

Muhamad kwa sasa anatumia muda wake kutembea tembea katika varanda na kumbi za eneo la watu wanaoondoka katika uwanja huo wa ndege.

"Wakati mwengine wafanyakazi wa mashirika ya ndege hunipa chakula. Ni hivyo kila siku na ninawashukuru sana."

Alipokutana na mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza, alikuwa akipata kifungua kinywa katika mgahawa wa shirika la ndege la Ethiopia. Shirika hilo limekuwa likimpatia chakuta toka alipopatwa na masaibu hayo.

Haki miliki ya picha Getty Images

Muhammad, kwa sasa analala kwenye chumba cha kusalia waisilamu katika uwanja huo.

"Hapa ndio sehemu ambayo mie hulala. Na ikiwa watu wapo wengi basi hutafuta kiti nje na kulala," bwana huyo pia amesema hajaoga kwa miezi kadhaa sasa.

"Siwezi kuishi hapa. Nataka kutuma ujumbe huu kwa yeyote atakayeweza kunisaidia, sababu nataka kuondoka mahali hapa...siwezi kuishi uwanja wa ndege kwa sababu sio nyumbani kwangu."

Kisa chake kinafanana na bwana mmoja raia wa Syria ambaye alinasa kwa miezi saba katika uwanja wa ndege nchini Malaysia. Hassan al-Kontar alikuwa akituma video mara kwa mara kutokea uwanjani hapo na kumfanya apate umaarufu na mwezi Novemba akapata kibali cha kuingia nchini Canada.

"Nimepakumbuka sana nyumbani. Kila mtu anakupenda nyumbani kwao. Nyumbani ni nyumbani, lakini haya mazingira ni magumu sana. Unanielewa? ni magumu sana," amesisitiza Muhamad.

Mamlaka ya uhamiaji ya Isreaeli imekanusha kutoa hati ya kughushi ya safari kwa bwana huyo na kusema walimfurusha nchini mwao sababu hakuwa na vibali halali.

"Ni raia wa Niger. Suala lake halituhusu tena kwa kuwa alifurushwa hapa na alipofika Niger hakutoa ushirikiano kwa mamlaka. Hapo Israeli inahusika vipi? Yeye si raia wetu."

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Kumekuwa na malalamiko ya unyanyaswaji kwa wahamiaji kutoka Afika nchini Israeli

'Hataki kubaki Ethiopia'

Muhamad anasisitiza kuwa aliwapa ushirikiano maafisaa kote nchini Niger, Israeli na Ethiopia.

Kwa sasa Ethiopia haina la kufanya zaidi ya kumpa hifadhi. Nchi hiyo ishawapa hifadhi takribani watu milioni moja kama yeye.

Mwezi huu imepitisha sera ya kuwapa elimu na nafasi za kazi wakimbizi.

Hata hivyo afisaa mmoja wa uhamiaji ambaye hakutaja jina lake kutajwa amesema Muhammad amegoma kuomba hifadhi nchini humo.

"Yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuamua. Tunajali utu wake na tutamuendea kujua kama amebadili mawazo yake na kuomba hifadhi ya ukimbizi nchini mwetu. Hiyo ndiyo hatua pekee ambayo tunaweza chukua."

Muhamad amesema hataki kubaki Ethiopia, anachotaka yeye ni kurudi nyumbani Niger ama kuruhusiwa kuendelea na maisha yake Israeli.

Kwa hali ilivyo. mpaka muafaka juu ya suala lake upatikane, Muhammad ataendelea kuishi kama mkiwa ndani ya uwanja wa Bole jijini Addis Ababa.

Mada zinazohusiana