Ruth Wacuka: Jinsi kipaji cha ushonaji kilivyobadili maisha ya mwanamke mmoja nchini Kenya

Huwezi kusikiliza tena
Ruth Wacuka Kimani: Mjasiriamali anayejikimu kwa kufuma

Ruth Wacuka mwenye umri was miaka 46 ni mfumaji kutoka jijini Nairobi. Kazi hii amekuwa akiifanya kwa muda wa mwaka mmoja.

Kabla ya kuanza kazi hii ya kufuma, Ruth alikuwa mkandarasi kwa takriban miongo miwili.

Aliacha kazi hiyo baada ya kukumbwa na maambukizi kwenye figo na kuugua kwa muda.

"Nikatembea kwa hospitali tofauti tofauti wala sikupona.Ikafika mahali ikanibidi niuze vitu vyangu vyote ili nigharamie matibabu"

Hali ilipozidi kuwa mbaya,Ruth alilazimika kuhamia jijini Nairobi kwa dadake kwa sababu alihitaji mtu wa kumtunza .

Ugonjwa huo ulimsababisha kupatwa na msongo wa mawazo, lakini kama walivyosema wahenga baada ya dhiki faraja, faraja yake ilimjia kwa talanta yake ambayo aliikuza miaka ya nyuma.

"Nikiwa hapa mgonjwa, wakati sina uchungu,nilikuwa natafuta kitu ambacho ninaweza kufanya ili nisiwaze sana. Siku moja dada yangu aliona nguo ambayo ilikuwa iimefumwa na akaniuliza kama ninaweza kufuma, nikamwambia ninaweza kufuma hata nguo nzuri kushinda hiyo. Akanipatia dola 5 nikanunue uzi …"

Hatua kwa hatua Ruth alianza kufuma nguo na kwa sasa ni kazi ambayo inampatia pato la kila siku.

"Nikashona ya kwanza, nikampata mteja, akaniletea wateja wengine… Yeye ndiye alikuwa mteja wangu wa kwanza, alifanya nikajua kuwa nilikuwa na kipawa ambacho nilikuwa nimekilalia"

Ruth anasema kwamba amekuwa akitumia mtandao kujua jinsi ya kufuma mitundo tofauti tofauti.

"Awali nilikuwa naangalia picha kisha nafuma, pole pole nikaja nikajua kumbe YouTube pia ninaweza pata miundo tofauti tofauti, na hapo ndiyo naweza jua hata vipimo vya nguo za watoto…"

Hata hivyo anasema kwamba anajivunia kazi hiyo kwani ikilinganishwa na kazi ya kuajiriwa, anaifanya wakati wowote na mahali popote.

"Mimi hufuma hata nikitembea, nikiwa kwenye gari, katika barabara za mitaa ambazo hazina msongamano wa magari… Nafuma tu.

Image caption Moja ya gauni la watoto ambalo Ruth amelifuma kwa mkono

"Huwa wengine wananiangalia wanashangaa, mwingine utaona anapata ujasiri anakuja ananiuliza ' Eh na wewe, hii kazi mimi niliona kitambo,hatujaona mtu akifuma kwa sindano. Hii ilikuwa ni kazi ya mama zetu.' Nawaambia basi hii ndiyo kazi yangu. Hii ndiyo inanilisha. Hii ndiyo inaniweka mjini"

Nchini Kenya wanafunzi zamai walifunzwa kufuma katika somo la Sayansi Kimu. Hata hivyo kutokana na kubadilika kwa teknolojia, iliyosababisha kubadilika kwa mfumo wa elimu,watu wengi hawajakuwa wakitumia bidhaa za kufumwa kwa mikono.

Betty Nekesa ni mfanyibiashara jijini Nairobi. Ni mmoja wa wale waliosoma Sayansi Kimu katika shule ya msingi.

"Tulifunzwa kufuma tulipokuwa shule ya msingi. Tulifuma sweta za shule, mifuko ya kubeba kalamu na vitabu na vitambaa vya kurembesha nyumba. Siku hizi tunanunua sweta za shule zilizofumwa na mashine kwenye viwanda, na hauwezi kupata mifuko ya kubeba vitabu iliyofumwa. Somo hilo lilikuwa la manufaa sana kwetu kwa sababu bei ya bidhaa zilizofumwa kwa mashine ni ghali kuliko zile zilizofumwa kwa mikono" Betty anasema.

Image caption Kivazi cha ufukweni kilichofumwa na Ruth Wacuka

Kwa sasa Ruth anawafunza wanawake wenzake kufuma akishirikiana na mwenzake ambaye pia anafuma.

"Kwa sasa tumefunza hapa Nairobi, tulikuwa Mombasa wikendi. Wamama wanajiunga wanatuita, tunaenda tunawafunza. Kuna wale huniita kwa nyumba zao niwafunze. "

Kutumia talanta kujiajiri ni nafasi ambayo vijana wengi hupuuza. Hii ni kukosatokana na ukosefu wa mwelekezobora kutoka kwa wazazi ambao wanaamini ili mtu afaulu maishani lazima asome na apate ajira ofisini.

"Kitu naweza kuwaambia vijana ni mtu akae chini, asahau ako na shahada ya digrii ama shahada zingine zozote. Kama ametembea amekosa kazi,akae chini ajiangalie ni nini anapenda kufanya... Soma pia ukiwa na mawazo wazi ya kwamba si lazima upate hiyo kazi ya daktari, si lazima upate hiyo kazi ya mwalimu, unaweza fanya kitu kingine wewe mwenyewe na kismo hicho umesoma halafu ufanikiwe."

Mada zinazohusiana