Ukuta wa mpakani Mexico: Majimbo yamshtaki Trump kwa kutangaza hali ya dharura

People protest against Donald Trump's National Emergency declaration, February 18, 2019, outside City Hall in Los Angeles

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Kutangazwa kwa hali ya dharura kumechangia maandamano

Muungano wa majimbo 16 nchini Marekani yakiongozwa na California yameushtaki utawala wa Rais Donald Trump kuhusu uamuzi wa kutangaza hali ya dharura ili kukusanya fedha za ujenzi wa ukuta wa mpakani na Mexico.

Kesi hiyo imewasilishwa katika mahakama ya wilaya ya kaskazini katika jimbo la California.

Inajiri siku kadhaa baada ya Trump kuidhinisha hali ya dharura, inayompa nguvu kulivuka bunge na kujipatia fedha kwa ujenzi huo - ambayo ni ahadi kubwa aliyotoa wakati wa kampeni yake.

Democrats wameapa kupinga hatua hiyo "kwa kutumia njia zozote zilizopo".

Mkuu wa sheria katika jimbo hilo la California Xavier Becerra amesema wanampeleka Trump mahakamani "kuzuia matumizi mabaya ya nguvu za rais".

"Tunamshtaki Trump kumzuia dhidi ya kuiba pesa za mlipa ushuru, zilizotengwa kisheria na bunge kwa watu wa majimbo yetu. Kwa wengi wetu, ofisi ya rais sio eneo la vioja ," aliongeza

Kesi hiyo iliyowasilishwa Jumatatu inaanza kwa kusikizwa awali ombi la kutaka kumzuia Trump ashughulikie dharura hiyo aliyoitangaza, wakati kesi ikiendelea kotini, gazeti la Washington Post linaripoti.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Ukuta huo wa Trump unaarifiwa utakuwa na paneli za kunasa miale ya jua ili kutengeza kawi ya bei rahisi

Trump alitangaza mpango huo baada ya bunge kukataa kufadhili ujenzi wa ukuta.

Kesi ya kwanza iliwasilishwa mara moja siku ya Ijumaa. Kundi la kutetea haki, Public Citizen, liliwasilisha kesi kwa niaba ya hifadhi asili, na wamiliki watatu wa ardhi katika jimbo la Texas ambao wamearifiwa huenda ukuta huo ukajengwa kwenye ardhi yao.

Trump alitangaza vipi hali hiyo ya dharura?

Akitoa tangazo hilo katika ikulu ya White House siku ya Ijumaa, rais amesema hali hiyo itaruhusu kupata takriban dola bilioni 8 kwa ujenzi wa ukuta huo wa mpakani.

Hiki ni kiwango kilicho chini ya gharama ya jumla ya dola bilioni 23 zinazohitajika kujenga ukuta huo wenye urefu wa maili 2000 wa mpakani.

Trump alikubali kwamba angeshtakiwa kwa hatua hiyo, na alitabiri kwamba kutangaza kwa hali hiyo ya dharura kutasababisha hatua za kisheria ambazo zina uwezekano mkubwa kuishia katika mahakama ya juu zaidi.

"Tutakabiliana na mzozo wa usalama wa kiatiafa katika mpaka wetu wa kusini ," alisema.

"Kila mtu anafahamu kwamba ukuta unafanya kazi."

Hatahivyo, rais pia alisema kwamba hana haja ya kutangaza hali ya dharura lakini alifanya hivyo kutokana na matumaini ya kupata fedha kwa haraka zaidi, lakini wachambuzi wanasema kauli hii huenda ikamtia mashakani katika kujitetea kisheria.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Kumeshuhudiwa maandamano ya kupinga azma hiyo ya Trump kujenga ukuta mpakani

Dharura ya kitaifa ni nini?

Sheria ya hali ya dharura ya kitaifa imenuiwa kwa nyakati ambapo kunashuhudiwa majanga ya kitaifa. Trump amebaini kwamba kuna janga la uhamiaji katika mpaka wa kusini wa taifa hilo - tuhuma inayopingwa pakubwa na wataalamu wa uhamiaji.

Idadi kubwa ya wahamiaji wanaoingia Marekani kila mwaka ni wale wanaoishi nchini baada ya viza zao kumalizika muda.

Kutangaza hali ya dharura kutampa nguvu maalum rais ambazo zitamruhusu kuuvuka mpangilio wa kisiasa, na ataweza kuelekeza fedha kutoka kwenye ufadhili wa sasa kwa jeshi, au bajeti ya kukabiliana na majanga ili kuulipia ujenzi wa ukuta huo.

Kwa mara nyingi katika tawala zilizopita, hali hiyo ya dharura iliidhinishwa kukabiliana na mzozo wa sera za kigeni - ikiwemo kuzuia ugaidi - mashirika yanayohusishwa kuzuia kupokea ufadhili, au kuzuia uwekezaji katika mataifa yanayohusishwa na ukiukaji wa haki za binaadamu.