Vyuo Vikuu Kenya: Maelfu ya wanafunzi Kenya wapata 'elimu hewa'

wanafunzi waliyofuzu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelfu ya wanafunzi wa baadhi ya vyuo vikuu nchini Kenya huenda wanasomea kozi ambazo hazijaidhinishwa na tume ya kusimamia elimu ya juu, CUE.

Tume hiyo imekataa kuidhinisha kozi 133 ambazo zinsomewa na wanafunzi 10,000 ambao wanakabiliwa na hatari ya kuachia katikati masomo kutokana na kosa ambalo si lao.

Kwa wale ambao tayari wamekamilisha kozi hizo ambazo hazijaidhinishwa inamaanisha stakabadi zao hazitatambuliwa na waajiri hali ambayo huenda ikawafanya kukosa kazi.

Baadhi ya wakuu wa vyuo vilivyoathiriwa na hatua hiyo wameikosoa tume hiyo kwa kuwachafulia sifa.

''Hizi kozi tayari zinafunzwa kwa nini CUE inawachochea wanafunzi dhidi ya vyuo vikuu?'' aliuliza mmoja wa chansela ambaye chuo chake kimeathiriwa.

Ripoti ya ukaguzi wa vyuo vikuu hivi karibuni, hata hivyo, imeshutumu taasisi za mafunzo ya elimu ya juu kwa kuanzisha kozi nyingi, ambazo hazikidhi mahitaji ya soko la ajira

''Yale mambo sisi tunafanya hapa, hatuoneshi kuwa kuna kozi ambayo haina maana, tulionesha kwamba kuna kozi ambazo hatujaidhinisha ambazo zinasomeshwa katika vyuo vikuu na vyuo vingine shirikishi'' anasema mwenyekiti wa CUE, Profesa Chacha Nyaigoti Chacha.

Chanzo cha picha, SKY AND SPACE GLOBAL

Prof. Chacha alifafanua kuwa kuna baadhi ya vyuo vikuu shirikishi ambavo zinachukua kozi za chuo mama na kuziita zao bila kupata idhini ya kutoka kwa tume hiyo.

"Huu ni mpango ambao unaendelea na kwa sasa tunashauriana na vyuo vikuu kuhakikisha zinafuata kanuni zilizowekwa''

Ukaguzi huo pia umebaini kuwa vyuo vikuu vimekuwa na tamaa ya kupata fedha kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi wanataka kujiunga nao.

Baadhi ya vyuo hivyo vilitoa taarifa za kupotosha kuhusu uwezo wao wa kufundisha idadi kubwa ya wanafunzi kama walivyopendekeza.

Ripoti hiyo inaonesha kuuwa vyuo vikuu vya uama na vya kibinafsi vilitangaz kuwa na jumla ya nafasi 163,925 za kozi tofauti lakini baada ya ukaguzi wa kina tume ya elimu ya juu ilibaini kuwa ni nafasi 134,075 pekee zilizoidhinishwa.

Huku hayo yakijiri bunge la Kenya limeitisha kikao cha dharura kujadilli hali ya masomo katika taasisi za elimu ya juu nchini.

Mkutano huo ambao umepangiwa kufanyika baadae wiki hii unatarajiwa kuwaleta pamoja washika dau mbali mbali ikiwa ni pamoja na maafisa wa wizara ya elimu,Tume ya kusimamia elimu ya vyuo vikuu na bodi za kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Chanzo cha picha, SIMON MAINA

Maelezo ya picha,

Bunge la Kenya

Masuala megine yanayokabili vyuo vikuu ni njia za kuimarisha elimu na kuhakikisha zinafikia mahitaji ya wanafunzi katika soko la ajira.

Katika ripoti yake ya mwaka 2016 tume ya kusimamia elimu ya juu nchini Kenya ilibaini kuwa ya ukaguzi wa vyuo vikuu vya umma na vile ya kibinafsi vina jumla ya kozi 3,408.

Kozi za kiwango cha shahada zilikua 1,627, ya uzamili 1,162, na kiwango cha uzamifu 518 huku zingine 96 zikiwa za kiwango cha stashahada na vyeti vya chini ya hapo.

Kulingana na ripoti hii mpya vyuo vikuu vya umma vilianzisha kozi zingine 2,752 ambazo ni 81% huku vyuo vikuu vya kibinafsi vikianzisha kozi 655 ambazo ni sawa na ongezeko la 19%.

Makosa makubwa

Katika ripoti nyingine iliyotolewa mwaka jana makosa yaligunduliwa katika kozi zinazosomeshwa katika vyuo vikuu.

Baadhi ya kozi hizo hazikua na wanafunzi wa kutosha.

"Baadhi ya vyuo vikuu vilisomesha kozi bila kuwa na ushahidi kuwa ziliidhinishwa na mamlaka husika," ilisema ripoti hiyo.

Ukaguzi pia umebaini kuwa baadhi ya vyuo vikuu vilibadilisha mtaala na majina ya kozi tofauti na zile zilizoidhinishwa.